KIONGOZI Mkuu wa Waislamu Shia Ithnasheria Tanzania Maulana Sheikh Hemed Jalala, amesema mwezi Mtukufu wa
Ramadhani unafundisha kutii sheria na
kufuata kanuni na taratibu za nchi.
Pia ni
madrasa na chuo cha kujifunza na kuacha yale ambayo jamii inayachukia na kila
mtu kuwa mtiifu.
Kauli hiyo,
ilitolewa jana Dar es Salaam na kiongozi huyo, wakati wa swala ya Idd el Fitr
na kupeana mkono wa Eid mubaraka katika viwanja vya pipo vilivyoko Kigogo.
Sheikh
Jalala, alisema kufunga ni ngome na kuangalia mambo ambayo ni haramu ikiwemo
kufanya usikivu na kuacha maovu.
‘’ Mwezi
mtukufu wa ramadhani ni kutii sheria na kanuni ikiwemo kuacha kunywa pombe na
kuacha mambo ambayo ni haramu ambayo yanaumiza muumini,’’alisema.
Alisema
Mwenyezi Mungu amelazimisha kuswali lakini ukiangalia swala tano ndani ya mwezi
mtukufu wa ramadhani sawabu zake na malipo yake sio kama siku nyingine.
‘’ Mwezi
mtukufu wa ramadhani sawabu zake ni tofauti na siku za kawaida, kwani ni chuo
kinachowatoa wanafunzi ambao masomo yao ni kutii sheria kanuni,’’alisema.
Vile vile
Sheikh Jalala alisema jamii ili iwe na maendeleo ni wajibu wa kila mtu kutii
sheria na kanuni kwani bila kufanya hivyo nchi yoyote haiwezi kuwa na
maendeleo.
‘’ Tukitii
sheria na taratibu za nchi hata vituo vya polisi vitapungua, mahakama ndogo
ndogo hazitakuwepo ambapo amani itakuwa imetawala katika majumba yetu na katika
jamii zetu, hiyo ndio siri ya maendeleo katika jamii yoyote,’’alisema.
Pia alisema
ni wajibu wa kila mmoja kumuomba Mwenyezi Mungu amani na utulivu ulioko uzidi kuboreshwa na yeyote
ambaye anataka amani iliyoko kuipoteza Mwenyezi Mungu amsambaratishe kabla
hajakanyaga ardhi hii.
Alitoa ombi
kwa jamii kuwa maelewano ambayo yalionyeshwa kipindi cha mwezi mtukufu wa
ramadhani uendelee kudumu bila ya ubaguzi wa dini yoyote wala ukabila.
Kwa upande
wa mmoja wa wanakamati mahsusi wa Jumuia ya dhehebu la Shia Ithnasheria nchini,
Sheikh Mulaba Swaleh, alisema siku ya Idd el Fitri ni siku tukufu na takatifu kwani waislamu wote wamemaliza mfungo
huu.
Alisema waislamu walikuwa katika kipindi cha
kujifunza namna ya kumcha Mwenyezi Mungu kwani anawataka kila mmoja kutii
sheria kuweza kuwa waadilifu.
‘’ Neno
uadilifu ni neon ambalo linahusu mambo yote ya kijamii na kiserikali ambapo
mwanadamu anatakiwa kuweka kitu mahala pake ambapo panastahili hivyo sote
tujifunze uadilifu,’’alisema.