Monday, January 25, 2016

Magufuli arejesha Ikulu kuwa mahala patakatifu Baada Ya Mambo Haya

Mwaka mmoja uliopita ungeweza kuamini kuwa Mtanzania aliyetwaa tuzo ya Mwanasoka Bora wa Afrika kwa Wachezaji wa Ndani hatoitwa Ikulu na Rais Jakaya Kikwete kwa ajili ya kupongezwa?
Jibu la swali hilo ni hapana; hasa ukizingatia kuwa wapo wanamichezo na wasanii waliotwaa tuzo ndogo zaidi lakini wakaalikwa katika ofisi kuu hiyo ya nchi kwa ajili ya kukutana na Rais.
Mwaka mmoja baadaye, Rais wa Tano John Magufuli amejikita katika kushughulikia matatizo halisi ya Watanzania na kufunga milango kwa wageni wasio na shughuli muhimu kwenda Ikulu, gazeti hili limebaini.
Ikulu pia imekomesha tabia iliyokuwa imezoeleka ya wageni kujazana kila siku sehemu ya mapokezi kwa ajili ya kwenda kuomba misaada mbalimbali kwa Rais, kama ilivyokuwa imezoeleka kwenye serikali iliyopita.
Gazeti hili lilifanikiwa kufika Ikulu sehemu ya mapokezi na kukuta viti vikiwa vitupu tofauti na awamu iliyopita ambapo mapokezi ya Ikulu ilikuwa ikitaka kufanana na eneo la shughuli hiyo katika hospitali yoyote ya mkoa nchini.
Viti vilijaa hadi kufikia hatua ya wageni hao kukaa kwa kupokezana.
Wakati leo ametimiza siku ya 80 tangu alipoapishwa Novemba 5, mwaka jana, Rais Magufuli amekutana na kufanya mazungumzo na viongozi wachache muhimu, hali inayoashiria kuwa Ikulu sasa ni mahala patakatifu, kama ambavyo Baba wa Taifa, Hayati Julius Nyerere alipata kuusia katika moja ya hotuba zake za kukumbukwa, ya Mei Mosi 1995 jijini Mbeya.
Miongoni mwa viongozi ambao Rais Magufuli amekutana nao Ikulu tangu aingie madarakani ni Sheikh Mkuu, Aboubakar Zuberi, Rais wa awamu ya Pili, Alhaji Ali Hassan Mwinyi, Rais wa awamu ya tatu, Benjamin Mkapa na Kikwete.
Rais Magufuli pia alikutana na Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar, Seif Sharif Hamad, Rais wa Zanzibar, Dk. Ali Mohamed Shein na Makamu wa Pili wa Rais Zanzibar, Balozi Seif Idd kuzungumzia hali ya mkwamo wa kisiasa inayoendelea visiwani humo.
Wengine aliokutana nao kwa mazungumzo Ikulu hivi karibuni ni aliyekuwa Mwenyekiti wa Tume ya Katiba Mpya, Jaji Joseph Warioba, Mwenyekiti wa Jumuiya ya Wazazi CCM Taifa, Abdalah Bulembo, Mkaguzi na Mdhibiti Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG), Profesa Musa Jumma Assad na aliyekuwa Mwenyekiti wa CUF, Profesa Ibrahim Lipumba.
Kutoalikwa Ikulu kwa Samatta ndiko kumedhihirisha kwamba sasa milango ya kwenda kumuona Rais haiko wazi sana kama ilivyokuwa kwenye awamu hiyo ya nne.
Rais Magufuli pia amepokea hati za mabalozi mbali mbali wanaoiwakilisha nchi zao ambao walifika Ikulu kwa ajili ya kujitambulisha.
Januari 7, Samatta alinyakua tuzo hiyo ya pili kwa ubora kwa wachezaji wa Afrika, baada ya Mchezaji Bora wa Afrika ambayo ilikwenda kwa Pierre-Emerick Aubameyang wa Gabon.
Tuzo hizo hutolewa na Shirikisho la Soka Afrika (CAF).
Kama Samatta angetwaa tuzo hiyo mwaka mmoja uliopita kwa mfano, isingekuwa rahisi kupita wiki moja bila Mbwana Sammatta kualikwa na Rais Ikulu.
Rais mstaafu Kikwete, ambaye ni mwenyekiti wa CCM,  ameshakutana na Samatta kwenye Ofisi Ndogo za chama hicho, Lumumba jijini.
Baada ya ushindi wake, Samatta alipokewa na Waziri wa Habari, Utamaduni, Michezo na Wasanii, Nape Nnauye, ambaye alimpa gari lake atumie kwa muda pia.
Miongoni mwa wageni waalikwa wa mara kwa mara wa Kikwete Ikulu ni pamoja na mwanamuziki maarufu wa zamani Ray C ambaye Desemba 10, 2012 alikwenda kumshukuru kwa kumsaidia tiba ya matumizi ya madawa ya kulevya.
Habari ambazo Nipashe inazo, Ray C bado anaendelea kupata tiba ya kuacha dawa za kulevya katika Hospitali ya Mwananyamala jijini Dar es Salaam.
Diamond Platnumz amewahi kualikwa mara kadhaa Ikulu, hata pale alipotwaa tuzo ndogo ambazo zilikabidhiwa kwenye hata klabu za usiku nje ya nchi.
Timu ya Azam imewahi kualikwa Ikulu baada ya kutwaa kwa mara ya kwanza Kombe la Kagame la Afrika Mashariki na Kati, taji ambalo Simba na Yanga zimelichukua jumla ya mara 11 katika historia.
Wachambuzi wa mambo walisema hali hiyo inadhihirisha kwamba Rais Magufuli amejikita katika kushughulikia matatizo ya msingi ya nchi, hasa vita dhidi ya ufisadi wa rasilimali za taifa, upatikaji wa huduma za jamii na uimarishaji wa miundombinu.
Dalili kwamba Ikulu sasa ni mahali patakatifu ilianza kujidhihirisha wakati wa kuapishwa kwa Baraza la Mawaziri mwishoni mwa mwaka jana.
Mawaziri hao waliapishwa bila mbwe mbwe wala shamra shamra kama ilivyozoeleka kwenye awamu ya nne, wahusika wakifika Ikulu bila kuambatana na utitiri wa ndugu na jamaa ambao chini ya Kikwete waliwalaki kwa maua na mashada baada ya kuapishwa.
Kwenye awamu ya nne, baadhi ya wateule walikuwa wakienda kuapishwa Ikulu na wake au waume zao, watoto, ndugu, majirani na jamaa zao na kupata fursa ya kupiga picha na Rais mara baada ya zoezi la kuapishwa.
Utaratibu huo umefutika baada ya Rais Magufuli kuonekana kujikita kwenye masuala ya msingi kama kupanga safu ya uongozi wake kwa kuwafuta kazi watendaji ambao anaona hawawezi kwenda na kasi yake.
Aidha, punde baada ya kuingia Ikulu Novemba 5, mwaka jana Rais Magufuli alifuta kitengo cha mapokezi ya wageni kwenye lango kuu la Ikulu na kuagiza watendaji wa serikali katika ngazi zote kutatua kero za wananchi mahala walipo ili kuwapunguzia usumbufu.
Kitengo cha Lishe kilichokuwepo Ikulu wakati wa serikali ya awamu ya nne kilivunjwa na watendaji wake kurudishwa kwenye Wizara mama walizotoka.chanzo NIPASHE

Wakazi Bonde la Mkwajuni wagoma kuondoka

Wakazi wa Bonde la Mkwajuni katika Mtaa wa Hananasifu na Suna, Manispaa ya Kinondoni ambao nyumba zao zilibomolewa, wanaishi kwenye eneo hilo licha ya kuendelea kuathiriwa na mvua.
Wakazi hao ambao hivi karibuni vibanda vyao vilibomolewa kwa amri ya Serikali, wameendelea kubakia na kujenga vibanda juu ya vifusi vya nyumba zilizobomolewa.

Mmoja wa wakazi wa eneo hilo, Nicolata Myanga alisema hawataondoka eneo hilo kwa kuwa Serikali haijawapa viwanja.
“Serikali kama inataka tuondoke ije itege bomu tu hapa tufe, tutakwenda wapi? Tunaambiwa tumepewa viwanja viko wapi? Hivi kweli mimi na uzee wangu huu nimepewa kiwanja naambiwa ondoka nitang’ang’ania hapa ili iweje?” alihoji Myanga mwenye umri wa miaka 68.

Mkazi mwingine wa eneo hilo, Magreth Dimoso alisema hali ya maisha yao inazidi kuwa ngumu kila siku, lakini mbaya zaidi ni kuwa kadri mvua zinavyonyesha hawana pa kukimbilia kwa kuwa hata baadhi ya vibanda walivyojenga vimesombwa na maji.
Mwathirika mwingine wa bomoabomoa hiyo, Anastatus Mponda alisema maisha yao ni magumu kuliko hata ya wakimbizi.

Kutokana na hali ngumu waliyonayo, baadhi yao wamegeuka kuwa ombaomba, kwani hata mwandishi wa habari hizi alipofika alilakiwa kwa salamu ya kuombwa Sh1,000 na Jumanne Iddy.
Maimuna Juma aliyekuwa amekaa nje ya kibanda chake akiwa anambembeleza mwanaye aliyekuwa akilia kwa sababu ya njaa, alipomuona mwandishi aliomba msaada wa fedha akamnunulie chakula.
Uongozi wa mtaa wanena
Mwenyekiti wa Mtaa wa Suna, Salumu Hamis alisema kuwa kuna kaya zaidi ya 700 zinaishi sehemu hiyo na kwamba, kati ya jumla ya kaya 900 zilizokuwa zinaishi hapo, 150 pekee ndizo zilipewa viwanja Mabwepande,” alisema.    

Waislamu Nigeria wakumbuka mauaji ya Zaria

Waislamu Nigeria wakumbuka mauaji ya ZariaWaislamu wa Nigeria wamefanya maandamano katika miji mbali mbali ya nchi hiyo kuadhimisha arubaini ya mamia ya ndugu zao waliouawa na jeshi la nchi hiyo katika mji wa Zaria mwishoni mwa mwaka uliopita.
Maandamano makubwa yameshuhudiwa katika mji wa Kano ambapo waandamanaji wamelaani mauaji ya mamia ya Waislamu wafuasi wa Harakati ya Kiislamu Nigeria, huku wakitoa mwito wa kuachiwa huru mwanachuoni wa Kiislamu nchini humo Sheikh Ibrahim Zakzaky.
Aidha maandamano mengine kama hayo yameshuhudiwa katika miji ya Sokoto, Minna na Katsina. Hii ni katika hali ambayo, Binti wa Kiongozi wa Harakati ya Kiislamu ya Nigeria amesema kuwa, familia yao haina taarifa zozote kuhusiana na hatima ya baba na mama yao wanaoshikiliwa na vikosi vya usalama vya nchi hiyo.

Badia Ibrahim Zakzaky amesema kuwa, baada ya kupita siku arubaini tangu kutokea maafa ya Zaria ambapo jeshi la Nigeria liliwauwa mamia ya Waislamu, asasi za kimataifa zimeshindwa kuandaa mazingira ya yeye kukutana na baba na mama yake wanaoshikiliwa na vikosi vya usalama vya Nigeria.

Itakumbukwa kuwa, mwezi Disemba mwaka jana, wanajeshi wa Nigeria waliwavamia Waislamu wa mji wa Zaria, kaskazini mwa nchi hiyo na kuwaua kwa umati mamia ya Waislamu.
Vilevile walimpiga risasi kadhaa na baadaye kumkamata Sheikh Ibrahim Zakzaky, Kiongozi wa Harakati ya Kiislamu ya nchi hiyo.chanzo irib

'Kuwakamata wanajeshi wa Marekani ni ushujaa'

'Kuwakamata wanajeshi wa Marekani ni ushujaa'Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu amesema kuwa, hatua ya hivi karibuni ya jeshi la majini la Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu SEPAH ya kuwakamata wanajeshi wa Marekani walioingia kwenye maji ya Iran kinyume cha sheria katika Ghuba ya Uajemi, ni kitendo cha kishujaa na kilichofanyika kwa wakati unaofaa kabisa.
Ayatullah Ali Khamenei amesema hayo leo Jumapili wakati alipoonana na maafisa wa jeshi la Sepah na sambamba na kuwashukuru wanajeshi hao wa Iran amesema: Kwa hakika inabidi tulihesabu tukio hilo kuwa limefainyika kwa taufiki ya Mwenyezi Mungu ambaye aliwafanya wanajeshi wa Marekani waingie katika maji ya Iran na wanajeshi wetu wachukue hatua ya haraka na ya kishujaa ya kuwatia mbaroni wanajeshi hao na kuwalazimisha kuweka mikono vichwani.
Itakukumbukwa kuwa, boti mbili za Marekani, tarehe 12 Januari 2016 zilikamatwa na wanajeshi wa Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu Sepah baada ya kuingia kinyume cha sheria katika maji ya Iran na kuwatia mbaroni wanajeshi 10 wa Marekani waliokuwemo kwenye boti hizo.
Wanajeshi hao wa Marekani waliachiliwa huru baada ya kubainika kuwa waliingia kimakosa katika maji ya Iran.chanzo irin