Wakazi wa Bonde la Mkwajuni katika Mtaa wa Hananasifu na Suna,
Manispaa ya Kinondoni ambao nyumba zao zilibomolewa, wanaishi kwenye
eneo hilo licha ya kuendelea kuathiriwa na mvua.
Wakazi hao ambao
hivi karibuni vibanda vyao vilibomolewa kwa amri ya Serikali,
wameendelea kubakia na kujenga vibanda juu ya vifusi vya nyumba
zilizobomolewa.
Mmoja wa wakazi wa eneo hilo, Nicolata Myanga alisema hawataondoka eneo hilo kwa kuwa Serikali haijawapa viwanja.
“Serikali
kama inataka tuondoke ije itege bomu tu hapa tufe, tutakwenda wapi?
Tunaambiwa tumepewa viwanja viko wapi? Hivi kweli mimi na uzee wangu huu
nimepewa kiwanja naambiwa ondoka nitang’ang’ania hapa ili iweje?”
alihoji Myanga mwenye umri wa miaka 68.
Mkazi mwingine wa eneo
hilo, Magreth Dimoso alisema hali ya maisha yao inazidi kuwa ngumu kila
siku, lakini mbaya zaidi ni kuwa kadri mvua zinavyonyesha hawana pa
kukimbilia kwa kuwa hata baadhi ya vibanda walivyojenga vimesombwa na
maji.
Mwathirika mwingine wa bomoabomoa hiyo, Anastatus Mponda alisema maisha yao ni magumu kuliko hata ya wakimbizi.
Kutokana
na hali ngumu waliyonayo, baadhi yao wamegeuka kuwa ombaomba, kwani
hata mwandishi wa habari hizi alipofika alilakiwa kwa salamu ya kuombwa
Sh1,000 na Jumanne Iddy.
Maimuna Juma aliyekuwa amekaa nje ya
kibanda chake akiwa anambembeleza mwanaye aliyekuwa akilia kwa sababu ya
njaa, alipomuona mwandishi aliomba msaada wa fedha akamnunulie chakula.
Uongozi wa mtaa wanena
Mwenyekiti
wa Mtaa wa Suna, Salumu Hamis alisema kuwa kuna kaya zaidi ya 700
zinaishi sehemu hiyo na kwamba, kati ya jumla ya kaya 900 zilizokuwa
zinaishi hapo, 150 pekee ndizo zilipewa viwanja Mabwepande,” alisema.
No comments:
Post a Comment