Waswahili husema; ‘atafutaye hachoki, akichoka
keshapata!’. Sadakta. Katika kutafuta
kuna kupata na kukosa. Na ikiwa kuna kushindana, basi kuna kushinda na
kushindwa. Vyovyote ilivyo, kushinda ni kupata, na kushindwa ni kukosa daima.
Msemo huu ni
maarufu sana baina ya Waswahili wa kwetu. Lakini umaarufu wa msemo huu umezidi
hasa baada ya siasa za vyama vingi kupamba moto nchini. Ambapo umaarufu mkubwa
msemo huo umezidi kunoga na kupata ladha baada ya chama cha Wananchi CUF kushindwa
uchaguzi mara zote. Kushindwa huko, kukautumia usemi huu kuwa kama kipozeo na
kiliwazo cha kushindwa!
Chama cha CUF
kilipoteza uchaguzi wa mwaka 1995, 2000, 2005 na 2010. Awamu zote hizo, mgombea
pekee alikuwa Maalim Seif Sharif Hamad ambaye hajapatwa kupingwa tangu muda
huo. Kushindwa kuko, lakini kwa bahati mbaya CUF imekuwa ikikataa kabisa kabisa
kuwa inashindwa kwenye chaguzi zote hizo.
Badala
yake, CUF hushikilia kutoa madai haya na
yale na visingizio lukuki. Madai ambayo kwa muda wa miaka ishirini sasa,
yameanza kukosa ladha. Miongoni mwa
madai makuu ya CUF kupoteza uchaguzi ni kudai ‘kuibiwa ushindi’ au ‘kutopewa
uraisi’ na chama tawala CCM.
Madai ya CUF
hapo awali yalikuwa yakiaminika kwa kweli, lakini kwa vile kila siku maneno ni
yale yale, sasa CUF hata wakisema nini, wanaonekana kama debe tupu tu. Haliachi makelele, ilhali halina kitu ndani.
Na CUF kama CUF ni mfano wa debe tupu, kingi maneno, vitendo hamna! Watashindaje
uchaguzi?
Mwaka 1995,
tuseme kweli CUF ilidhulumiwa au tuseme
kuibiwa kama tulivyozowea kuambiwa. Lakini mwizi huiba mara moja, akirudi tena
kukuibia wewe wewe, mahala pale pale tena katika mazingira yale yale, ilhali unamuona na unamjua kama
anakuja kukuibia, ukamwachia akaiba ukitegemea kuonewa huruma, huu ni uzembe
usiostahamilika.
Na ni uzembe wa
aina hii unaoigharimu CUF kila siku na katika kila uchaguzi. Kuna mengi ya
kuikosoa CUF juu ya hili lakini tusiangalie kukosoana, tuwanie kuangalia wapi
tunajikwaa na nini kilikuwa kifanywe.
Nina taarifa
kutoka kwa kada mmoja mkuu wa CCM (jina kapuni) akisema kwamba CCM Zanzibar
hawazidi asilimia 35 ya watu wote au wapiga kura wote iwapo watu wataandikishwa
bila ubaguzi, hata CCM ikiandikisha na mamluki.
Kwa maana kama
hii, ni wazi kuwa CUF ina wingi wa kura na wafuasi. Kauli hii pia
inathibitishwa na viongozi wengine wa CCM akiwamo Bi Asha Bakari Makame. Bi
Asha, amesema Gombani. Akarudi akasema tena katika bunge la katiba kuwa ‘’ikiwa
CUF walishindwa kutawala 1995 hawatawali tena milele nchi hii.’’alieleza.
Kauli ya Bi Asha
haikuishia hapo, akasema na sababu ya kuwa CUF haitashinda pia pale alipodokeza
kuwa ‘nchi hii tumepindua, hatutoi kwa karatasi!’ Haya si maneno ya Asha
Bakari. Ni ahadi na kauli mbiu ya CCM kwa ujumla wake. Huo ndio msimamo wao. Na
kwa hakika wanautekeleza kwa vitendo.
Niliposema CUF
wanamalizwa na Uzembe, nilisahau na vitu vingine viwili: Kujua sana na
Kujiamini sana kunakotokana na kulewa sifa. Vitu hivi vitatu ndio mizimu
inayoisumbua CUF miaka yote na kupelekea kushindwa katika kila uchaguzi huku
wakisingizia kuibiwa.
Kuna Uzembe
katika CUF. Uzembe wa awali na wa kilele ni ule uliofanyika mwaka 1995. Mwaka
ambao licha ya vyombo vya habari kadhaa kutangaza ushindi wa CUF Maalim Seif
alijifungia kwake Mtoni akisubiri aje aitwe akaapishwe kuwa Rais. Kusema la
uhaki Maalim alishinda na hili linathibitika kwenye kauli hiyo ya Bi Asha
Bakari. Lakini wapi?
Maalim alikaa
kwake mpaka Nyerere akaja na kuwaambia TUME wamtangaze Salmin kwa sababu Maalim
Seif alikuwa hajawa tayari kuwa Rais. Na hapo ndipo CUF walipojikwaa sio kwa uzembe tu: na kulewa sifa na kujiamini
kwingi.
Wakati CCM
ikitumia chupu chupu ya uchaguzi wa 1995 kujifunza kutokana na makosa, CUF
ilitumia makosa yale yale kama njia yao ya kujipatia ushindi katika chaguzi
zijazo. Kimaumbile, huwezi kutumia makosa kupatia ushindi wa jambo sahihi.
Makosa siku zote hukupa mwanga wa ulipojikwaa lakini hayakufikishi popote
ukiyafuata.
CUF imekuwa
ikirudia makosa yale yale iliyoyafanya
miaka ya nyuma. Makosa yenyewe sio mengi sana
kwani miongoni mwa makosa hayo, ni mbinu wazitumiazo CCM kuwashinda CUF.
CCM, haijatumia mbinu nyingi kuishinda CUF: ‘Wembe wao ni ule ule’ wa ushindi
kwani hawaoni haja ya kubadilisha wakati anyolewaye hajali atanyolewa vipi.
CCM hutumia
wakati wa kuhesabu kura kuongeza zao kwa mujibu wa madai ya CUF. Wakikosa hapo,
huficha visanduku vya kura kwa kutumia vyombo vya usalama na kufanya watakayo
huko na mwisho hugeuza matokeo tu: ya CUF akapewa CCM na ya CCM yakarudi CUF.
Siku hizi kumezuka utaratibu wa kuandikisha mamluki kutoka bara na kuongeza
idadi ya wapiga kura watakaoibeba CCM. Hili liko wazi na linaonekana na kila mtu na hata CUF wenyewe ni mara
kadhaa wamekua wakilisemea kwenye mikutano ya hadhara pia vyombo vya habari
laki ni sawa na kupepea mwiku.
Makosa makubwa
wayafanyayo CUF ukiacha yale ya uzembe wa viongozi wakuu wa chama, utayaona
kwenye mawakala feki na wasimamizi feki wa chaguzi. Mara kadhaa, tunayaona ya
mawakala wa CUF kununuliwa na kuachia visanduku vya kura vikiibiwa. Mara
kadhaa, tumoena mawakala wa CUF wakiambiwa wakapate chakula cha mchana, na
wakiondoka mamluki wa CCM huingizwa wakapiga kura mara mia mia kila mmoja,
wakirudi hamna kitu.
Licha ya hayo,
CUF haijajifunza kitu. Kama ilivyokuwa haijajifunza kitu katika kuchaguwa
wagombea wazuri wa ubunge na uwakilishi, bado ni yayo kwa yayo. Wanachaguana
akina wale wale walima mwani na visirani nakuacha watu ambao wananchi wenyewe
wamewataka.
Kwa mfano,
aliyepitishwa kiti cha Uwakilishi jimbo la Tumbe ni kichaa maarufu na amewahi
kufungwa mara kadhaa. Huyo ndiye mwakilishi wa watu wa Tumbe anaetegemewa kuja
kuleta mabadiliko tuyatakayo. Na wengine wengi, funika kombe mwanaharamu apite.
Abubakar amepita tena Mgogoni ilhali hana lolote alifanyalo: si jimboni wala si
barazani.
Hivi sasa kuna
uthibitisho wa kutosha kuwa CCM imeandikisha mamluki kadhaa na kuwanyima watu
kadhaa haki ya kuandikishwa kupiga kura. CUF hili hawajaliona kuwa tishio kwao.
Wana uhakika watashindwa kisha waje watwambie, tumeibiwa ilhali wameshindwa kwa
idadi kubwa ya kura mamluki.
Wakati CCM
ikijiandaa kufa kupona, liwalo na liwe, lakini nchi hawatoi, CUF wanaandaa
maandamano makubwa ya kumpongeza Maalim Seif huku CCM wakijifungia ndani
wakipanga mikakati madhubuti ya kuwamaliza wazembe, walewa sifa na wenye
kujiamini bila kuwa ubavu wa kujiaminia kiukweli. Tumeona: wameongeza majimbo
Unguja na kupunguza Pemba watakavyo. CUF inapiga makofi kwa Maalim kurejesha
fomu.
Wakati CCM
wakinadi kuwa hawatoi kwa kura. Viongozi wa juu wa CUF tunaowaamini zaidi akina
Jusa wanaongea maneno yasiyo nafasi hata ndogo kwenye siasa za CCM Zanzibar.
Juzi Jusa nilimnukuu akisema; ‘’Bakora ya kuwapiga CCM ni siasa za kistaarabu
za CUF’’
Umeona wapi
siasa za kistaarabu barani Afrika Jusa? Hivi CCM yuko tayari muuwane lakini
ashinde, unafikiri ustaarabu wako atauelewa? Basi Jusa nikwambie kitu.
Ustaarabu bara umefika juzi na haujaenea hadi leo, uko jina tu kama Uislamu
ulivyo huko hivi sasa. Na CCM ni chama cha huko. Na wao wanasema hawatoi kwa
kistaarabu sharti mpambane kwa sababu wao walipambana. Unaonaje hili?
Nionavyo, CCM
wanachokisema ni kweli kwa sababu kina ushahidi. Hawakutoa 95, 2000, 2005, na
2010. Nina uhakika, kwa viongozi kama hawa wa CUF tulionao akina Jusa Mstaarabu,
CUF kuingia madarakani Zanzibar ni sawa
na ngamia kupenya kwenye tundu la sindano. Tusidanganyane. Wala tusikubali tena
kudanganywa.
Tusidanganyike
kwa sababu, CUF hata baada ya kuona
mambo yote yanayofanywa na CCM kujihakikishia ushindi wa kishindo ambao kwa
hakika upo, bado siku tu, hawajachukua hatua yoyote hile hadi sasa ikiwa
tumebakiwa na takribani miezi minne kufika uchaguzi mkuu. Wao wanaona fahari
kupokelewa kwa makundi ya wanachama wa CUF wasio na vitambulisho vya ukaazi
wala vya wapiga kura, wakadanganyana kuwa watashinda uchaguzi.
Tusidanganywe, maadamu CUF ikiwa ndani ya Serikali
imeshindwa kuleta ushawishi wa kuundwa tume huru ya Uchaguzi, hakuna liwalo.
Tutaishia kumpokea Maalim Seif kurudisha fomu ya urais tu, hatakuwa kamwe.
Hatakuwa kwa sababu hataki awe. Anachokitaka ni hiki tunachokifanya, kumpokea
na kutuchezea akili zetu kwa kutujaza tamaa za kuku lala lala!
Tusidanganyane,
CUF haitashinda kwa sababu inajua inapojikwaa lakini inaendelea kupita hapo
hapo kila siku. Itajikwaa tena na tena na mwisho, itaanguka chini, Na mwisho
wenyewe hauko mbali. Ni mwaka huu. Iwapo hawataacha uzembe, wakapunguza kulewa
sifa, na wakaacha kujiamini bila uhakika wa kupata ushindi, tujiandae tena kuwa
wakimbizi wa kisiasa kama tulivyofanywa 1995 na 2001. Hakuna liwalo!
Chanzo: Mazrui media