Sunday, August 16, 2015

Nasrullah aikosoa Marekani kwa kuitumia Daesh


Katibu Mkuu wa chama cha Hizbullah cha Lebanon amesema kuwa Marekani inalitumia kundi la kigaidi la Daesh kuligawa eneo la Mashariki ya Kati. 
 Sayyid Hassan Nasrullah amesema kuwa Washington na waitifaki wake wanatumia ugaidi hususan kundi la kigaidi la Daesh kama wenzo wa kutekeleza mpango wa kuligawa eneo la Mashariki ya Kati, kuanzia Iraq hadi Syria na hata Saudi Arabia kwa sababu mpango huo unafanyika kwa maslahi ya Marekani na utawala wa Kizayuni. 
Sayyid Hassan Nasrullah ameyasema hayo jana usiku katika hafla ya kuadhimisha mwaka wa tisa wa ushindi wa Muqawama wa Lebanon dhidi ya utawala wa Kizayuni katika vita vya mwezi Julai mwaka 2006. 
Katibu Mkuu wa Hizbullah amesema kuwa upo udharura wa kupinga na kukabiliana na mpango wa kuligawa eneo hili. 
Amesema njama ya kuigawa upya Mashariki ya Kati itasababisha vita vya ndani na vya kikaumu vya muda mrefu, ambavyo matokeo yake yatakuwa uharibifu, maafa na kuongezeka idadi ya wakimbizi.Chanzo Irib

Mawahabi wataka misikiti saba ya Madina ibomolewe

Mjumbe wa baraza la maulamaa wa Saudi Arabia na mmoja wa mawahabi mwenye misimamo ya kufurutu ada ametaka misikiti saba maarufu ya Madina ibomolewe. 
Saleh al-Fawzan, mjumbe wa baraza la maulamaa wakuu wa Saudia na mjumbe wa kamati ya kudumu ya utoaji fatuwa amedai leo kuwa misikiti saba ya kihistoria ya mjini Madina ni bid’a na yote inapasa ibomolewe. 
 Historia ya misikiti hiyo saba inarejea kwenye zama za vita vya Khandaq na iko kwenye bonde la mlima Sala’a magharibi mwa Msikiti mtukufu wa Bwana Mtume Muhammad SAW mjini Madina. 
Misikiti hiyo saba hivi sasa imekuwa moja ya maeneo ya ziara kwa Waislamu kutoka nchi mbalimbali duniani; ambapo mara baada ya kuwasili Madina Waislamu hao huenda kuzuru misikiti hiyo.chanzo Irib.