Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais
Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa Mhe. George Simbachawene amewataka
Watendaji wanaosimamia uendeshaji wa Elimu katika ngazi ya Mkoa,
Halmashauri na Shule kuzingatia kwa ukamilifu ushauri unaotolewa na
Wadhibiti Ubora wa Elimu wanaoutoa kutokana na kasoro kadhaa wanazobaini
katika maeneo wanayoyakagua ili kuhakikisha kuwa watoto na vijana
wanapata elimu bora siyo tu kwa maisha yao ya baadaye bali pia
itakayowawezesha kulitumikia taifa kwa weledi na uadilifu
.
Akifungua kikao cha siku mbili
kati ya Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa( OR-TAMISEMI)
na Maafisa Elimu wa Mikoa,Wakuu wa shule Kongwe na Wakuu wa zilizoungua
moto kinachofanyika mjini Dodoma tarehe 18-19 Agosti mwaka 2016, Mhe.
Simbachawene amesema kushindwa kufanyia kazi kasoro zinazojitokeza au
kutambuliwa na Wadhibiti Ubora ni sawa na kuhujumu jitihada za serikali
za kuwaandalia maisha bora vijana wake.
“Nitumie wasaa huu, kuwaagiza
watendaji wote mnaohusika katika eneo hilo kushughulikia kikamilifu
kasoro zote zinazotambuliwa hususani zile ambazo ziko ndani ya mamlaka
za uwezo wenu na kama ziko juu ya uwezo wenu, basi ziwasilisheni kwa
wakati kwa mamlaka husika. Wizara yangu haitasita kuchukua hatua stahiki
kwa wale wote watakaozembea kutimiza wajibu wao. Alisisitiza Mhe.
Simbachawene.
Mhe. Simbachawene alisema
serikali ya awamu ya tano imeifanya elimu kuwa ni moja ya vipaumbele
vyake na kuwekeza mabilioni ya fedha katika kuendesha na kutekeleza
miradi ya mbalimbali ya elimu kwa kushirikiana na wadau wa maendeleo.
Alisema miongoni mwa mambo ambayo
serikali imeyafanya katika kuboresha elimu nchini ni pamoja na
kuwaendeleza walimu kazini kupitia Mipango mbalimbali, kutoa fedha za
Ruzuku, kutoa fidia ya ada, chakula na maabara kila mwezi, kuwanunulia
pikipiki Waratibu Elimu Kata wote, kutengeneza madawati kwa shule za
msingi na sekondari,kusambaza vitabu kwa darasa la Kwanza pamoja na
kusambaza vitabu vya Sayansi na Hisabati kwa shule za Sekondari.
Mambo mengine aliyoyataja ambayo
yamefanywa na Serikali katika kuboresha elimu kuwa ni pamoja na Ujenzi
wa Maabara, Ukarabati wa shule kongwe, ukarabati wa shule za ufundi,
utoaji wa mafunzo ya uongozi kwa Walimu Wakuu, Wakuu wa Shule na
Waratibu Elimu Kata pamoja na utoaji wa Posho ya Madaraka kwa Walimu
Wakuu wa shule na Waratibu Elimu Kata ambapo alisema kutokana na mambo
hayo hakuna sababu za msingi za shule kutofanya vizuri.
Alisema kwa muda mrefu sasa,
matokeo ya mitihani yanaonyesha kuwa taaluma ya shule kongwe inaendelea
kushuka na baadhi ya shule hizo kuwa za mwisho katika mitihani ya kidato
cha sita ambapo alitolea mfano wa shule za sekondari za Tabata na
Iyunga kuwa za mwisho katika mitihani ya kidato cha sita mwaka 2015 na
shule za sekondari za Kwiro na Azania kuwa za mwisho kwa mwaka 2016.
Aliwataka washiriki wa kikao hicho
kujadili na kuona kuwa jukumu na wajibu wa kutafuta ufumbuzi wa
changamoto mbalimbali zinazoikabili sekta ya elimu kwa ujumla pamoja na
kujadiliana ili kupata mapendekezo ya mbinu na mikakati ya kuondokana na
changamoto za uendeshaji na usimamizi wa shule ambazo hivi sasa
zinaendelea kuporomoka kitaaluma.
Mhe. George Simbachawene aliyataja
maeneo ambayo yanaweza kutoa mchango hasi katika utoaji wa elimu kwa
shule kongwe za sekondari na msingi kuwa ni usimamizi dhaifu katika
ngazi ya shule za kata,kutowachukulia hatua stahiki na wakati walimu
wasio wajibika,kutozifanyia kazi taarifa za ukaguzi, maandalizi duni ya
walimu kabla ya kufundisha pamoja na walimu wa masomo ya sanaa kushindwa
kuwajibika kikamilifu licha ya idadi yao kuwa kubwa.
Alisema matukio ya kuungua kwa
shule kutokana na ajali za moto ambazo zimekuwa zikitokea hivi karibuni
zimekuwa zikiisononesha serikali , wanafunzi, wazazi na watanzania wote
kwa ujumla kwakuwa maeneo yaliyopatwa na majanga ya moto yameathirika
kwa kiasi kikubwa.
“ Taarifa za uchunguzi za awali
ambazo tumekuwa tukizipokea zimeonyesha kuwa chanzo cha ajali nyingi za
moto ni hitilafu ya umeme. Pamoja na taarifa hizo , tumeendelea kupata
mashaka zaidi pale ambapo shule nyingine zilizopatwa na janga la kuungua
moto hazina hata miundombinu ya umeme. Tunashukuru kwa ushirikiano
tunaoupata kutoka kwenye vyombo vyetu vya usalama ambavyo mpaka sasa
vinaendelea na uchunguzi wa kina ili kupata chanzo halisi cha matukio
hayo.
Alisema Mhe. Simbachawene.
Kikao hicho cha siku mbili
kinalenga katika kujadiliana juu ya Usimamizi na Uendeshaji wa shule
kongwe za sekondari za serikali na kuangalia ni kwa jinsi gani kiwango
cha elimu katika shule hizo katika shule hizo kinainuliwa.
Kikao hicho pia kililenga katika
kujadiliana kuhusu matukio ya kuungua kwa moto kwa shule za sekondari za
bweni na zenye hosteli katika sehemu mbalimbali hapa nchini.
Akimkaribisha mgeni rasmi kufungua
kikao hicho, Kaimu Katibu Mkuu Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na
Serikali za Mitaa Bw. Bernard Makali amesema kuwepo kwa udhaifu katika
usimamizi wa elimu katika ngazi ya shule ambao umesababisha ufundishaji
katika shule kongwe kuwa wa kusuasua na kusababisha shule mhizo kushuka
kitaalamu na kushika nafasi za mwisho kwenye mitihani ya kitaifa ambapo
aliwataka washiriki kutumia kikao kupata mbinu sahihi ili kuweza kuinua
kiwango cha ufaulu katika shule za serikali na za binafsi.