Thursday, October 15, 2015

TANZIA.Mwenyekiti wa NLD Dr.Makaidi ambae ni Mwenyekiti mwenza wa UKAWA afariki Dunia

Dk Emmanuel Makaidi alikuwa Mwenyekiti wa Taifa wa Chama cha NLD na ni mhandisi aliyebobea. Alizaliwa Aprili 10, 1941 huko wilayani Masasi mkoani Mtwara. Baba yake mzazi alikuwa ni katekista wa Kanisa la Anglikana.

Mwenyekiti Mwenza wa UKAWA ambaye pia ni Mwenyekiti wa chama cha NLD, Emmanuel Makaidi amefariki dunia leo katika hospitali ya Nyangao huko mkoani Lindi kwa shinikizo la damu
 Alianza elimu katika Shule ya Msingi Namalenga wilayani Masasi kati ya mwaka 1948 – 1952, mwaka 1953 – 1954 alisoma katika Shule ya Kati (Middle school) iitwayo Luatala hukohuko Masasi. Baadaye alijiunga na Shule ya Sekondari ya Chuo cha Mtakatifu Joseph na kusoma kidato cha kwanza hadi cha nne kati ya mwaka 1953 hadi 1956.
Makaidi alisoma darasa la 13 na 14 (kidato cha tano na sita) katika Shule ya Sekondari Luhule, Uganda kati ya mwaka 1957 – 1958. Alipelekwa Uganda si kwa sababu ya kipato cha baba yake, la hasha, alisaidiwa na Askofu wa Anglikana baada ya kuona anafaulu mitihani yake kwa alama za juu sana.
Makaidi aliendelea kufadhiliwa na askofu huyo ambaye alimuunganisha na mashirika mengine na kumtafutia chuo Afrika ya Kusini. Akapelekwa Chuo Kikuu cha Witwatersrand na kuhitimu Shahada ya Uendeshaji na Usimamizi kati ya mwaka 1958 – 1960.
Baada ya kuhitimu vizuri pale Witts, aliendelea kupata ufadhili wa masomo ya shahada ya uzamili, mara hii alielekea Marekani na kusoma masuala ya Menejimenti na Utawala kwa ngazi ya uzamili kati ya mwaka 1960 – 1962. Alisoma pia katika Chuo Kikuu cha Howard kilichoko jijini Washington, Marekani.
Baada ya kurejea nchini akiwa mhitimu wa M.A, Makaidi alianza kazi serikalini mwaka 1966 hadi mwaka 1973 akiwa mchambuzi kazi mkuu, katika kitengo cha Utumishi.
Kati ya mwaka 1974 na 1975 (miaka miwili). Alirudi tena Marekani na kusoma Shahada ya Uzamivu (PhD) katika Sayansi ya Siasa katika Chuo Kikuu cha Howard akipata kuwa karibu na mmoja wa maprofesa nguli duniani, Wamba Dia Wamba. Makaidi ameniambia kuwa hata tabia ya kuandika vitabu na kutunga mambo ya ubunifu, alifundishwa na profesa huyu mahiri.
Aliporejea nchini kwa mara ya pili mwaka 1976 aliendelea na kazi yake pale Utumishi hadi mwaka 1985 alipopewa kazi nyingine kubwa zaidi, akawa Mkurugenzi wa Miundo na Mishahara kwenye kamati iliyokuwa inashughulikia mashirika ya umma nchini.
Wakati anaendelea na kazi utumishi, alipata fursa nyingine ya kusomea stashahada ya Kuchakata Taarifa za Kielektoniki katika Chuo Kikuu cha Trinity, Ireland. Alikwenda huko na kuhitimu mwaka huohuo 1977.
Kabla hajafanya kazi katika kamati maalum ya kusimamia mashirika ya umma akapandishwa cheo na kuwa Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Kazi na Ustawi wa Jamii na mwaka huohuo 1985 akafukuzwa kazi.
Kisa cha Makaidi kufukuzwa kazi serikalini, tena akiwa na wadhifa huo ilikuwa ni kwa sababu ya kuandika kitabu cha Kiingereza chenye jina “mwanasiasa mwenye roho ya shetani”. Serikali ikamzonga vilivyo, ikamtuhumu kuwa kitabu kile kinamtukana Mwalimu Julius Nyerere. Mwisho wa siku “kazi ikaota mbawa”.
Bahati nzuri, mwaka huohuo 1985 akaajiriwa na Shirika la Finwork Directory kuwa Mkurugenzi Mtendaji, kazi aliyoifanya hadi mwaka 1991.
Kuanzia mwaka 1992 hadi mauti yanamkuta, Dk Makaidi hakujishughulisha tena na kazi za serikalini wala mashirika binafsi. Alijiajiri akiwa na kampuni kadhaa zilizoajiri Watanzania wa vipato vya kawaida, lakini pia aliendelea kutoa ushauri wa kitaalamu kwa kampuni za ndani na nje ya nchi huku akiongoza chama cha NLD akiwa Mwenyekiti.
Dk Makaidi alikuwa mwandishi mzuri wa vitabu, alishaandika zaidi ya 10. Amemuacha mjane Modesta Ponela na watoto wanane.Chanzo Jamii forum

Mahujaji wa Tanzania waliofariki dunia Mina wafikia 20

Idadi ya mahujaji wa Tanzania waliofariki dunia katika maafa ya Mina yaliyotokea tarehe 24 mwezi uliopita wa Septemba, imeongezeka na kufikia 20 baada ya kupatikana miili ya mahujaji wengine wanane.
Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa ya Tanzania imetangaza kuwa miili ya mahujaji wengine wanane wa nchi hiyo wamepatikana na kufanya idadi yao kuwa mahujaji 20.
Maafa ya Mina yalitokea sikukuu ya Mfunguo Tatu yaani siku ya Idul Adh'ha, tarehe 24 Septemba, na mamlaka za Saudi Arabia zinalaumiwa kwa kufanya uzembe uliopelekea kutokea maafa hayo.
Wizara ya Mambo ya Nje ya Tanzania imeongeza kuwa, Saudi Arabia inaendelea kufanya uchunguzi na itakuwa ikiipa wizara hiyo taarifa za miili itakayogundulika au mahujaji waliojeruhiwa.
Mashinikizo yameongezeka kutoka kila upande ya kutaka kuundwe kamati maalumu ya kutafuta ukweli kuhusu maafa hayo, na sheria kufuata mkondo wake mbele ya kile aliyehusika na vifo hivyo vya kutisha.chanzo irib

Maadili ya Ashura na Maadili ya Imam Hussein (a.s).

Maadili ambayo yamerejea kwenye uhai kwa matokeo ya kuasi kwa Imam Hussein (a.s) hutajwa kama ifuatavyo: Maadili ya Ashura na Maadili ya Hussein (a.s). Kabla ya kujadili maadili haya ni muhimu kwanza kuelewa madhumuni ya mihanga hii mikubwa ilikuwa ni nini. 
Tukio hili la msiba limekuwa kwenye ndimi zetu tangu karne nyingi na mengi yamesemwa na kuandikwa kuhusiana nalo. Ni vizuri kumuuliza mtangulizi, Kiongozi mwenyewe wa mashahidi, kuhusu madhumuni ya kadhia hii kuliko kuyaendea maoni na maandishi ya wachambuzi mbalimbali, waandishi, watafiti mahatibu, wanachuoni na wasomi, ambao wameelezea mitazamo yao juu ya kadhia hii. 
Lazima tutafakari juu ya maneno ya Imam Hussein (a.s) ili kuona kile alichosema kuhusiana na madhumuni ya kuasi kwake. Wakati wa kuondoka Madina, kwa mikono yake mitukufu, Imam Hussein (a.s) aliandika wosia wa urithi kwa ajili ya ndugu yake Muhammad bin Hanafia (a.s) na akamkabidhi.
Katika wosia huu wa urithi anaelezea madhumuni ya kuasi kwake:
"Siondoki (kutoka Madina) kama muasi, makandamizaji na dhalimu, bali madhumuni yani ni kuutengeneza Umma wa babu yangu. Njia pekee ya kufanya mageuzi haya ni Amr Bil Ma'ruf (kuamrisha mema, kwenye Maadili yajulikanayo) na Nahi Anal Munkar (Kukataza maovu), 
yaani, nataka kuutengeneza Umma kwa njia ya Amr Bil Ma'ruf na Nahi Anal Munkar. Sio kwamba mimi ni mtu wa kwanza ambaye ninafuata njia hii ili kuutengeneza Umma, kabla yangu mimi babu yangu na baba yangu wote walifuata njia hii tu. Nami pia nataka kufuata mwenendo wao wa kufanya Amr Bil Ma'ruf na Nahi Anal Munkar kwa ajili ya kuutengeneza Ummah."Unaweza kurejea: Mawassai Kalimatul Imam Hussein Uk. 290 - 291

Kumbukumbu ya Mwaka Mpya wa Kiislam

Sheikh Hemed Jalala, Mmoja wa Viongozi Wakuu wa Kiroho wa Waislam, Dhehebu la Shia Ithnasheriya Tanzania. Kushoto kwake ni Naibu Mkuu wa Chuo cha Kiislam cha Imam Swadiq (a.s).Leo Masjid Ghadir, Kigogo-Post Dar es salaam


Hawa ni baadhi ya wanahabari wakiwa makini katika kumsikiliza Sheikh Hemed Jalala
Habari Kamili


Tunamshukuru Mwenyezi Mungu kwa kufikia mwaka 1437, baadhi yetu tukiwa wazima, pia Mwenyezi Mungu awape afya wale wenye maradhi na awatie nguvu wale wanyonge.

Usiku wa leo ni tarehe 1 muharram 1437, sawa na tarehe 15 Oktoba 2015. Lakini siku ya leo, watanzania wanaadhimisha siku aliyofariki baba wa taifa hili Mwl. J.K Nyerere (14/Oktoba). Tunatoa mkono wa pole kwa familia ya Mwl. Nyerere, kwa rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na watanzania wote.

Baba wa taifa anakumbukwa kwa mambo mengi katika historia ya nchi yetu. Kama waziri mkuu wa kwanza wa Tanganyika, Kama rais wa kwanza wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Kama miongoni mwa viongozi walioongoza mapambano ya kumuondoa mkoloni Tanzania na afrika kwa ujumla.

Tunafanya haya kwakurejea maneno ya Imam Ali (a.s) katika nahjul balagha, maneno yaliyonukuliwa na aliyekuwa katibu mkuu wa umoja wa mataifa Bwana Koffi Annan (1997-2006) kuwa “ watu ni aina mbili, aidha  ni ndugu yako katika dini au ni ndugu yako katika damu (nasabu). Kwahiyo tunakila sababu ya kutoa mkono wa pole kwa watanzania.

Pili, leo katika historia baada ya maghrib, waislam kwa kuzingatia kalenda ya mwezi (lunar calender) tunaukaribisha mwaka mpya wa kiislam (1437 .H). Katika kuukaribisha, hatuna budi kufahamu pia kuwa mwaka uliopita (1436 H) ulimwengu wa kiislam ulikumbana na changamoto nyingi. 
Kuna haja ya kujifunza kutokana na changamoto hizo. Baadhi ya changamoto hizo ni pamoja na maafa ya mahujaji ambapo maelfu ya mahujaji wamepoteza uhai wao, hatutosita kuzitaka mamlaka husika kuwajibika kwa hilo.

Pili, vita nchini Syria na Yemen ambazo msingi wake mkuu ni kukithiri kwa ubepari /ubeberu ulimwenguni na kuibuka kwa makundi ya kukufurishana (takfiir groups).

Tatu, kumomonyoka kwa maadili miongoni mwa wanajamii hasa baada ya kutangazwa kwa uhalali wa ndoa za jinsia moja kwa nchi za magharibi, hivyo kuathirika kimaadili na kiuchumi kwa nchi nyingi tegemezi.

Tatu, kushuka kwa bei ya nishati ya mafuta duniani ambayo kwa kiasi kikubwa nchi nyingi zilizoathirika ni za ukanda wa ASIA ambazo zinaidadi kubwa ya waislam.

Nne, ni kukithiri kwa mauaji ya watu wenye albinism, hali iliyopelekea wajihisi kuwa ni raia wa daraja la tatu nchini Tanzania.

Tano, kuchomwa kwa baadhi ya nyumba za ibada na kudhuriwa kwa baadhi ya viongozi wa dini nchini Tanzania.

Mwisho, leo (usiku, 15/10/2015 sawa na 1 Muharram 1437) katika ulimwengu wa kiislam, waislam na wapenda haki wote duniani tunakumbuka matukio ya kuuwawa kikatili mjukuu wa Mtume (s.a.w.w), Imam HUSSEIN (a.s). 
Kwa ufupi, Imam Hussein  ni kiongozi aliyeonesha dira ya namna ya kupambana  na DHULMA ulimwenguni kama Mahatma Gandhi (Baba wa Taifa la India) na Rabindranath Tagore walivyomulezea Imam Hussein katika maandishi mbalimbali wakihusianisha mafanikio ya harakati nyingi za kudai haki na Imam Hussein (A.S).

  Kwa huzuni kabisa, tunatoa mkono wa pole kwa Mtume (s.a.w.w) na familia yake (Ahlulbayt), pia kwa waislam wote ulimwenguni na wapenda haki pasina kujali imani zao.

Imam Hussein ni kielelezo cha utu, uadilifu, na amani. Pia ni ishara ya ukombozi wa viumbe na ni kielelezo cha kupinga dhulma ulimwenguni.

Kaulimbiu ya mwaka huu:

IMAM HUSSEIN (A.S) NI DARASA JUU YA UHURU WA BINAADAMU NA UPINGAJI WA DHULMA.



IMETOLEWA Na: Sheikh Hemed Jalala

Mmoja wa Vingozi  Wakuu wa kiroho wa waislam dhehebu la shia Ithnasheriya Tanzania.