Hatimaye Mkurugenzi Mtendaji wa Mtandao wa JamiiForums, Maxence Melo
amerejea uraiani akitokea mahabusu baada ya kuachiwa kwa dhamana jana
huku akisema, ameshtakiwa kwa msimamo wake wa kulinda haki za watumiaji
wa mtandao huo.
Melo alipandishwa kizimbani katika Mahakama ya
Hakimu Mkazi Kisutu Ijumaa iliyopita akikabiliwa na kesi tatu kwa
mahakimu watatu tofauti.
Ameshtakiwa kwa kosa la kuendesha mtandao
wa kijamii ambao haujasajiliwa kwa kanuni za tovuti za Tanzania na
kuzuia upelelezi wa polisi.
Katika kesi hizo, Melo alifanikiwa
kupata dhamana kwa kesi mbili, huku akikwama kupata dhamana ya kesi moja
baada ya kushindwa kutekeleza masharti ya dhamana na kulazimika
kupelekwa rumande.
Hata hivyo, jana Melo alifanikiwa kukamilisha masharti na Hakimu Mkazi Mkuu, Godfrey Mwambapa na alimpatia dhamana kwa masharti.
Masharti
hayo ni pamoja na kuwa na wadhamini wawili ambao walisaini bondi ya Sh5
milioni na kutotoka nje ya Dar es Salaam bila kuwa na kibali cha
Mahakama. Kesi hiyo itatajwa tena Desemba 29.
Baada ya kuachiwa,
Melo aliitisha mkutano na waandishi wa habari na kuishukuru wananchi na
watumiaji wa mitandao ya kijamii kwa mjadala wa kutaka aachiwe huru kwa
dhamana, tangu aliposhikiliwa na polisi kabla ya kupandishwa kizimbani.
Melo aliwatoa hofu watumiaji wa mtandano huo na kuwahakikishia kuwa JamiiForums ipo salama na haijachukuliwa taarifa zake.
“Hivyo
Max nimekuwa mfano tu kwani haya ya kukamatwa yanaweza kumkuta mtu
mwingine pia. Kikubwa inatakiwa uhuru wa kujieleza pamoja na kulinda
siri za watumiaji wa mitandao,” alisema Melo.