Thursday, May 17, 2018

"Mwezi wa Ramadhani ndio Mwezi wa Utakaso wa Nafsi" Maulana Sheikh Jalala

Kiongozi Mkuu wa Waislamu Shia Ithnasheriya Tanzania Maulana Sheikh Hemed Jalala akiongea na Waandishi wa Habari katika kuukaribisha Mwezi Mtukufu wa Ramadhani, Masjid Ghadir, Kigogo Post Dar es salaam.
Amani ya Mwezi Mungu iwe kwenu nyote

Katika kuupokea Mwezi Mtukufu wa Ramadhani, napenda mwezi huu wa Ramadhani wa Mwaka huu tuupokee chini ya kauli mbiu “Mwezi wa Ramadhani ndio mwezi wa kuitakasa Nafsi”
Kwanini mwezi wa Ramadhani uwe ndio mwezi wa kuitasa Nafsi? Kwasababu Mwenyezimungu ndani ya Quran anasema “Mmelazimishwa kufunga kama waliokuwa kabla yenu ili muwe wachamungu”

Kwahivyo unakuta falsafa kubwa ya funga ni watu kuwa wachamungu, na uchamungu ndio kuitakasa nafsi, na Mwenyezimungu amelisifu tendo la kuitakasa nafsi aliposema “ yoyote amabe atajitahidi kuilea nafsi yake basi huyo amefaulu, lakini yoyote amabe atashindwa kuilea nafsi yake huyo amepata hasara”

Na tukiangalia falsafa kubwa na kutumwa mitume ilikuwa ni kulea nafsi, ilikuwa ni kuwalea watu, ilikuwa ni malezi ndio malengo makubwa ya kutumwa mitume, sintosahau maneno ya Mtume Muhammad (s.a.w.w) alipokuwa wamewatuma baadhi ya watu kwenda kwenye mapambano ya vita vitakatifu ndidi ya wapinzani wa Uislamu na wanaomzuia Mtume kueneza Ujumbe (Daawa).
 

Mtume akatuma gurupu kwenda kupigana nao, lakini waliporudi Mtume akawaambia karibuni watu amabo mlikwenda kwenye mapambano madogo, lakini mmerudi yamebakia mapambano makubwa, wakamuuliza mtume mapambano makubwa ni yapi?, 

Mtume akawaambia mapambano makubwa ni kuilea nafsi,kwahiyo malezi ya nafsi kuitakasa nafsi ni jambo kubwa , ni mampambano makubwa aliyobakianayo mwanadamu, tunaamini ya kwamba mwezi wa Ramadhani kama tutauchukuwa ni mwezi wa kulea nafsi zetu, kuna mambo mengi makubwa yatapatikana.

Litapatikana jambo linaloitwa kuwatumikia wanadamu, na hili ni jambo moja kubwa muhimu ambalo kwa ajili hii mitume wametumwa na sisi tupo hapa duniani, fadhila kubwa ni kuwatumikia watu, kwahiyo kama tutazilea nafsi zetu katika mwezi wa Ramdhani tutaweza kuitumikia jamii, kuwatumikia vipi?

 Tutawatumi8kia wanadamu katika kujali mayatima, tutawajali wajane, tutawajali watu wanaoishi katika mazingira magumu, hatutowanyanyapaa watu wenye matatizo yoyote katika mili yao, tutakuwa watu wakwanza kuwajali masikini, tutakuwa watu wa kwanza kuwajali mafakiri, tutakuwa watu wa mstari wa mbele katika kuhakikisha yoyote aliefunga mwezi wa ramadhani hakosi futari, tutahakikisha kwamba majirani tunaokuwa nao na wao wanafuturu vizuri,


Kwahiyo kuitakasa nafsi katika mwezi wa Ramadhani ni jambo kubwa lenye faida nyingi moja ni kuitumikia jamii, Moja katika mambo tunyoyakosa katika jamii zetu ni kutokuhisi majukumu yetu, wakati mwingine tunakwenda ofisini,makubaliano na bosi tuudhurie saa 1 au saa 2 kamili asubuhi, tutahudhura saa 3, hii ni kutokuhisi majukumu yako.

Kuitakasa nafsi moja ya faida zake ni kuhisi majukumu yako uliokabidhiwa , kunawatu amabo wamekabidhiwa majukumu ya kuwatumikia wananchi, hawa kwa sababu ya kuitakasa nafsi zao watajua wajibu wao wakufanya nini na wala hawatazembea.

Kuna watu wanatakikana wajitolee kwa ajili ya nkuwatumika watu, kwasababu ya kuitakasa nafsi wataweza kujitolea, kwahivyo kuitakasa nafsi ni katika mambo makubwa na mazito,
Mwisho ni jambo la mmomonyoko wa maadili leo hapa Tanzania kwetu na duniani kote  moja ya mabo ambayo yanawasumbua wanadamu ni mmomonyoko wa maadili, maadili kuanzia ngazi ya familia mpaka ngazi ya kijamii, mpaka ngazi ya kitaifa, sehemu zote hizo maadili yamesambaratika.


Kuilea nafsi, kuitakasa nafsi ni moja ya mambo yatakayosababisha maadili makubwa ndani ya familia zetu, ndani ya jamii zetu na ndani ya taifa letu, kwahivyo kuilea nafsi kuitakasa nafsi ni kauli mbiu muhimu ya kuifanyia kazi ndani ya mwezi mtukufu wa Ramadhani.

Walhamdulillah Rabbil aalamini, Asanteni sana,na Mungu awabariki na Inshaalla atujalie tufunge swaumu,  iliyokuwa yenye kheri na Baraka na malengo makubwa ya kuitaka nafsi na kuwatumikia wanadamu, Asanteni sana Mungu awe Nanyi.

Imetolewa na
Kiongozi Mkuu wa Waislamu Shia Ithnasheriya Tanzania
Maulana Sheikh Hemed Jalala