Mkurugenzi Mtendaji wa Kituo cha Sheria na Haki za Binaadamu Bi. Helen Kijobi Simba ameitaka Serikali
kupitisha Sheria maalumu kwa ajili ya Wajane kwa kufuta Mila na Desturi ambazo
ni kandamizi kwa wajane zinazosababisha kukosa haki zao na kupelekea kunyanyaswa
na familia husika.
Aidha Bi Simba ambae pia ni Mjumbe wa Bodi ya Chama cha
Wajane Tanzania ameiomba serikali kuwachukulia hatua kali za Kisheria kwa wale
wote wanaoendekeza Mila na Desturi Kandamizi kwa wajane pia kusaidia kwa kutoa
elimu katika hizo Mila na Desturi zilizopitwa na wakati ili ziweze kuondoka.
Wito huo ulitolewa jana katika Kongamano la Kimataifa
lililoandaliwa na Chama cha Wajane Tanzania, Dar es salaam, taasisi mbalimbali
zinazohusiana na kutetea haki za binadamu na Mambo ya Uchumi zilishiriki.
Kwa Upande wake Mkurugenzi wa Chama cha Wajane Tanzania Madam
Rose Sarwat alisema lengo kuu la Kongamano hili la Kimataifa ni kuweza kukaa
Wajane wan chi nzima kuangalia changamoto za wajane zinaweza kutatuliwa vipi? Na chanzo cha
changamoto ni nini? Na jinsi gani tunaweza kuungana kama wajane wa Tanzania na
nchi jirani kutatua changamoto zetu.
Kongamano hili la Kimataifa
limewakutanisha Wawakilishi wa Chama cha Wajane kutoka Mikoa yote ya
Tanzania, Kutoka nchi za Jirani kama Kenya, Malawi na DRC-Congo, kongamano hili
limeanza Jana, na linatarajiwa linatarajiwa kudumu kwa kipindi cha siku tatu
katika Mwezi huu wa Januari 2018.