Sheikh Ikrima Sabri, Khatibu na Imam wa msikiti wa
Al-Aqsa amesema sheria ya kupiga marufuku sauti ya adhana katika
misikiti ya ardhi za Palestina zinazokaliwa kwa mabavu ni ya kidhalimu
na kusisitiza kwa kusema: Sitatekeleza uamuzi huo.
Mufti wa Quds na Khatibu wa msikiti wa Al-Aqsa ameongeza kuwa
hatua za aina hiyo za maghasibu wa Kizayuni si za kisheria na ni
uingiliaji unaofanywa na Wazayuni katika masuala ya kidini ya Waislamu.
Huku akisisitiza kwamba hatua ya utawala wa Kizayuni kuhusiana na
suala hilo ni uingiliaji mipaka ya Waislamu, Sheikh Sabri ameongeza kuwa
adhana ni katika alama za Kiislamu na hakuna mtu mwenye haki ya
kuingilia suala hilo kwa sababu au kisingizio chochote kile.
Mufti wa Quds na Imam wa Msikiti wa Al-Aqsa ameonya kuwa serikali ya
mrengo wa kulia ya utawala wa Kizayuni wa Israel ndiyo itakayobeba dhima
ya mivutano na mtafaruku wowote utakaosababishwa na uamuzi huo.
Kamati ya mawaziri ya utungaji sheria ya utawala wa Kizayuni siku ya
Jumapili ilipitisha rasimu iliyofanyiwa marekebisho ya sheria ya
"marufuku ya kutangaza adhana" katika mji wa Baitul Muqaddas na
kuiwasilisha kwenye bunge la utawala huo Knesset.
Kwa mujibu wa
duru za habari, bunge la utawala wa Kizayuni wa Israel, linatazamiwa
kuupigia kura muswada huo kesho Jumatano ili uwe sheria.
Kwa mujibu wa
sheria hiyo, utumiaji vipaza sauti katika maeneo ya ibada na usomaji
adhana utakuwa marufuku kuanzia saa tano usiku hadi saa moja asubuhi.
Katika miongo ya
karibuni utawala wa Kizayuni umekuwa ukifanya kila njama za kubadilisha
utambulisho wa Kiislamu wa mji wa Baitul Muqaddas; ambapo hatua ya
karibuni kabisa ni hiyo ya kupiga marufuku kusomwa adhana kwenye
misikiti ya mji huo