Wednesday, April 15, 2015

Butiku amewataka wananchi kuipigia kura ya hapana katiba inayopendekezwa

Mkurugenzi mtendaji wa taasisi ya mwalimu Nyerere akifungua madahalo katika ukumbi wa Chuo Kikuu (TEKU). Kulia kwake ni Ally Saleh na kushoto kwake ni Pof. Mwesigwa Balegu na Hance Polepole
Baadhi ya watu waliojitokeza kusikiliza mdahalo katika ukumbi wa Chuo Kikuu (TEKU)
Wakati harakati za mashirika yasiyo ya Serikali zikiendelea kutoa elimu juu ya katiba inayopendekezwa kabla ya kupigiwa kura na kuwa katiba kamili, Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya Mwalimu Nyerere bwana Joseph Butiku amewataka wananchi kuipigia kura ya hapana katiba hiyo inayopendekezwa.

Amenukuliwa kuyasema hayo katika mdahalo uliofanyika katika ukumbi wa Chuo Kikuu (TEKU) wakati wakitoa maoni yaliyotolewa katika "Tume ya Jaji Warioba" kwamba katiba hiyo haijazingatia kile kilichomo katika rasimu.

“Isomeni katiba vizuri na kuipigia kura ya hapana kwani mkifanya hivyo italazimu kuipitia upya kutokana na kwamba katiba inayopendekezwa imeondolewa maono yenu mengi ikiwepo mamlaka ya Rais, Mbunge kuwajibishwa na wapiga kura wake, Mawaziri wasitokane na wabunge na kadhalika... wamefanya hivyo kutaka kutetea maslahi yao na kuwakandamiza wananchi,” amesema Butiku

Naye mtoa mada, Hance Polepole amesema katiba ni mkataba kati ya wananchi na viongozi wanao waongoza na hivyo wanatakiwa kuwa makini katika kutengeza mkataba ili wasije kulaumiwa na vizazi vijavyo kwa kushindwa kutengeneza katiba yenye kulinda maslahi yao na kuwafanya wengine watumwa katika nchi yao, kwani kila mtu ana haki ya kufaidi kwa usawa. 
Chanzo 

Mashine za BVR na aundikishaji wapiga Kura

Tume ya Taifa ya Uchaguzi Nchini Tanzania itaanza kusambaza mashine za BVR 248 katika mikoa saba nchni Tanzania kuanzia katikati mwa wiki ijayo.

Mikoa iliyoanza kupokea mashine hizi ni Lindi, Mtwara, Ruvuma, Iringa. Mkuu wa kitengo cha Ufundi wa idara ya Daftrari/ICT wa NEC Dk Sisit Cariah, amesema kwamba mpaka sasa wanachi wa mikoa ya Lindi, Mtwara, Ruvuma na Iringa wakae tayari kwani muda wowote watatangaziwa vituo vya kujiandikisha.

Mikoa zitakakopelekwa katika awamu ya pili ni Katavi, Mbeya, Dodoma, Singida Tabora Geita na Kigoma.

Pamoja na mshine hizo 248 Tume ya taifa ya uchaguzi imewaandaa wataalamu 248 ambao watakuwa na jukumu la kutoa elimu kwa wataalamu wengine 50 kwa kila mmoja nchi nzima kwa ajili ya kuharakisha uandikishaji kwa mfumo wa BVR.

Dk Sisit ameeleza kwamba wamefanikiwa kufanya maboresho makubwa katika mashine hizi ikiwa ni pamoja na kubadilisha upangaji wa vifaa (settings), mfumo endeshi (software) na upande wa vichapishio (printers) ambazo sasa zimetengenezewa nchini Ufaransa umeboreshwa na ni rahisi kusafishwa.

Mafunzo yaliyoendeshwa hapa Jijini Dar es Salaam yamechukua siku moja na yamezingatia sana upande wa vichapishio (printers), visoma alama za vidole (Finger Print Scanner) na kamera kutambua macho. Ameongoza kwamba printer za sasa ni rahisi kusafishwa na hata kuweka kifaa kipya baada ya cha zamani kuharibika vimerahisishwa.

Kuhusu uchukuaji wa alama za vidole, amesema kwa sasa tatitzo la mashine ya kuchukua alama za vidole wamelitatua kwa asilimia mia, kwani kwa wale ambao hawana alama za vidole mashine zimewekewa mfumo wa algorithm mpya ambao uatatambua kila aina ya kidole.

Pia, kamera zimewekewa mfumo mpya wa kutambua macho mekundu na kurekebisha rangi ya macho mekundu (Red eyes) bila kukwamisha zoezi la uandikishaji.

Mtarajio ni kwamba zoezi la uandikishaji liwe limekamilika ndani ya kila siku 28 tokea kila mkoa unapopokea mashine hizi. Vile vile Dk Sisit ameishukuru serikali kwa kufanikisha upatikanaji wa vifaa, “serekali imejitahidi kuandaa upatikanaji wa mashine hizo, na usafirishaji kwa njia ya ndege kwenda nchi nzima. Kila halmashauri na mkoa utachukua angalau siku 28 kukamilisha mkoa utakapo pokea vifaa,” Dr Sisit amesema.

Mwisho amesema kwamba mashine nyingine 1,600 zitawasili wakati wowote. Serikali imetoa Dola za Kimarekani milioni 72 (Sh. bilioni 133). Kuwasili kwa mashine hizo, kunaifanya NEC kupokea mashine 2,098, huku ikisubiri mashine 5,902, ili kukamilisha 8,000 zinazotakiwa. 

Alisema vifaa hivyo vinanunuliwa na serikali kupitia kampuni ya Lithotech Export ya Afrika Kusini, ambayo imeingia mkataba na NEC na inaviagiza kutoka China.
 Chanzo

Marufuku wanachama wa ACT - Wazalendo kushabikia Ukawa.



Kiongozi wa Chama cha ACT-Tanzania, Zitto Kabwe akihutubia mkutano wa hadhara katika Uwanja wa Mwembetogwa, Iringa 

Chama cha ACT-Wazalendo kimesema kila mwanachama anapaswa kuwaunga mkono wagombea watakaopitishwa na chama hicho katika nafasi mbalimbali katika Uchaguzi Mkuu ujao, kwani kinyume chake ni kukisaliti na adhabu yake ni kufukuzwa.

Mwenyekiti wa chama hicho, Anna Mghwira alisema mwishoni mwa juma kuwa katika kipindi hiki cha kuelekea kwenye Uchaguzi Mkuu, chama hicho kinahitaji nguvu za pamoja.

“Sisi bado hatujajiunga na Ukawa, hivyo wanachama wetu wanapaswa kulitambua hilo na kuepuka kushiriki kwenye ushawishi wa kufanya kampeni za wagombea wa vyama vingine. 

Hata kwenye katiba yetu tunasema sasa tunalenga zaidi katika kujiimarisha ili kutoa ushindani mzuri wa kisiasa katika uchaguzi huu,” alisema.
 
Kiongozi wa Chama cha ACT-Tanzania, Zitto Kabwe akihutubia mkutano wa hadhara katika Uwanja wa Mwembetogwa, Iringa
Katiba ya ACT, imeeleza wazi kuwa pamoja na sababu nyingine na kwa mujibu wa kanuni zitakazotungwa na Halmashauri Kuu, mwanachama yeyote ambaye atasaidia kushawishi, kujiunga, kutoa tamko la kuunga mkono chama kingine au mgombea wakati chama kimeweka mgombea wake kwa mujibu wa sheria za nchi, atakuwa amepoteza uanachama wake.

ACT- Wazalendo tayari imetoa ilani yake ya uchaguzi ikionyesha kwamba iwapo itaingia madarakani, itawajibika kwa wananchi kwa kuweka kipaumbele katika maeneo manne ambayo ni hifadhi ya jamii, uchumi shirikishi wenye kuzalisha ajira nyingi na bora, afya na elimu.

Kauli hiyo ya ACT linakuja huku kambi ya vyama kadhaa vya upinzani vinavyounda Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa), ikiwa kwenye mchakato wa kuunganisha nguvu ili kusimamisha mgombea mmoja wa urais na kuachiana majimbo katika baadhi ya maeneo.

Mwenyekiti mwenza wa Ukawa, James Mbatia amewahi kunukuliwa akisema kuwa umoja huo unaoundwa na Chadema, CUF, NCCR-Mageuzi na NLD umehamishia nguvu zake kwenye Uchaguzi Mkuu wa 2015.

Mbatia alisema tayari umoja huo umeunda kamati maalumu kutafuta namna ya kumsimamisha mgombea mmoja wa urais na kuachiana majimbo.
 
Kiongozi wa Chama cha ACT-Tanzania, Zitto Kabwe akihutubia mkutano wa hadhara katika Uwanja wa Mwembetogwa, Iringa 
Mbatia ambaye pia ni Mwenyekiti wa NCCR-Mageuzi, alisema tayari kamati zimeundwa na zinaendelea na kazi ya kuratibu mpango huo mahsusi, unaolenga kuiondoa CCM madarakani.

“Lengo letu ni kuhakikisha Ukawa ina nguvu ya kushika dola katika Uchaguzi Mkuu wa 2015 na katika mpango huo, vyama vitaachiana majimbo na viti vya udiwani kulingana na nguvu ya chama katika sehemu husika,” alisema.

Mkakati huo uliopangwa na Ukawa, unaelezwa na wachambuzi wa masuala ya kisiasa kuwa ni kombora kwa CCM, kwani endapo utafanikiwa, utakiweka chama hicho tawala katika wakati mgumu katika Uchaguzi Mkuu uliopangawa kufanyika Oktoba mwaka huu.
 Chanzo;Mwananchi.com

Zarif: Mashambulizi ya Saudia si suluhisho huko Yemen


Waziri wa Mambo ya Nje wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran amesema kuwa mashambulizi ya kijeshi yanayoendelea kufanywa na Saudi Arabia dhidi ya watu wa Yemen si suluhisho la mgogoro wa nchi hiyo.
Waziri wa Mambo ya Nje wa Jamhuri ya Kiislamu ya IranMuhammad Javad Zarif


Muhammad Javad Zarif ambaye alikuwa akihutubia maafisa wa serikali ya Uhispania mjini Madrid amesema kuwa historia imethitisha kuwa hakuna nchi ya kigeni iliyowahi kuidhibiti Yemen na kwamba mashambulizi ya mabumu yanayofanywa na Saudi Arabia dhidi ya nchi hiyo yanaharibu miundombinu tu. 

Zarif ametaka kusitishwa mashambulizi hayo mara moja na kuruhusu misaada ya kibinadamu kupelekwa nchini Yemen.

Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran pia amezungumzia kadhia ya nyuklia ya Iran na kusisitiza kuwa Tehran daima imekuwa ikifanya jitihada za kupata teknolojia ya nyuklia kwa matumizi ya amani. 

Amesisitiza kuwa Iran haijawahi kukengeuka sheria katika jitihada zake za kupata teknolojia ya nishati ya nyuklia.