Wednesday, February 17, 2016

Waziri wa afya , atembelea MNH , aridhishwa na utendaji kazi.

hi6Waziri wa Afya Maendeleo ya Jamii , Jinsia , Wazee na Watoto  Ummy  Mwalimu leo  ametembelea Hospitali ya Taifa Muhimbili-MNH- kwa lengo la kukagua jengo la watoto pamoja na jengo la wazazi namba mbili ( Maternity Block Two)  ili kuona utendaji kazi na  utekelezaji wa maagizo ya Rais John Magufuli .

Mwishoni mwa wiki iliyopita,  Rais Magufuli aliagiza watumishi wa Wizara  ya Afya , Maendeleo ya Jamii , Jinsia , wazee na Watoto kitengo cha  afya ya mama na mtoto kuhama katika jengo hilo ili kupisha Hospitali ya Taifa Muhimbili kulitumia kama wodi ya wazazi .

Waziri Ummy  ambaye ameambatana na Naibu Waziri Dokta Hamis  Kigwangala ameelezea kuridhishwa na ukarabati unaoendelea katika majengo hayo  .
hi7
“Jengo la watoto tatizo kubwa lilikuwa  ni miundombinu ya maji lakini naona ukarabati unaendelea vizuri na nina imani kuwa ukarabati utakamilika kwa wakati” amesema Waziri .

Akizungumzia kuhusu jengo la wazazi namba mbili , Waziri huyo wa afya amesema kuwepo kwa jengo hilo ni faraja kwa kina mama  na kusisitiza kwamba hakuna mama mjamzito atakayelala chini .
Mpaka sasa kina mama 53 tayari wamehamia  katika jengo hilo na wanapatiwa huduma zote.

Jeshi la Nigeria laharibu kambi za Boko Haram

Jeshi la Nigeria laharibu kambi za Boko HaramJeshi la Nigeria limesema kuwa, limefanikiwa kuharibu kambi za wapiganaji wa kundi la kigaidi la Boko Haram katika vijiji vya Doro na Kuda vya kaskazini mashariki mwa jimbo la Borno. 
 
Msemaji wa jeshi la Nigeria, Kanali Sani Usman, amewaambia waandishi wa habari kwamba wanamgambo wanne wa Boko Haram wameuawa huku wengine wawili wakikamatwa wakati wa operesheni katika misitu ya eneo la Alagarno na Sambisa. 

Wanajeshi watatu na raia wanne wamejeruhiwa katika mapigano kati ya wanamgambo hao na maafisa wa usalama.
Jeshi la Nigeria limesema operesheni kama hizo zitaendelea katika maeneo mengine ya nchi hiyo hadi pale kundi hilo la kitakfiri litakapozidiwa nguvu na kutokomezwa. 

Rais Muhammadu Buhari wa Nigeria amesisitizia umuhimu wa ushirikiano wa mataifa ya Afrika Magharibi na Kati ili kufanikiksha vita dhidi ya ugaidi. 

Kundi la Boko Haram limepoteza eneo kubwa lililokuwa likilidhibiti, lakini bado linafanya hujuma za kushitukiza dhidi ya maeneo ya raia na kusababisha maafa na hasara kubwa.Chanzo irib

Jela ya wenye misimamo mikali kujengwa Kenya

Jela ya wenye misimamo mikali kujengwa KenyaRais Uhuru Kenyatta wa Kenya amesema njia pekee ya kupunguza kuenea athari mbaya za ugaidi na madudu yake ni kupitia kuundwa jela ya aina yake itakayotumiwa kuwafungia watu wenye misimamo mikali.

Rais Kenyatta amesema kuchanganyika wafungwa wa kawaida na wale wenye misimamo mikali na magaidi kumechangia tatizo hilo kuenea na watu wengi kujiunga na makundi ya aina hiyo.

"Tutaunda jela maalumu kwa ajili ya watu wenye misimamo mikali. Hatutokubali fikra za ugaidi na misimamo mikali kuenezwa kupitia jela za nchi hii" amesema kiongozi huyo.

Ingawa hakutaja kundi lolote moja kwa moja, wachambuzi wanasema kundi la kigaidi la al Shabaab ndilo lililolengwa kwenye kauli hiyo ya Rais wa Kenya.

Kundi hilo limekuwa likifanya mashambulizi ya kushtukiza dhidi ya raia na maafisa wa usalama wa Kenya ndani na nje ya nchi hiyo. Shambulizi la hivi karibuni la kundi hilo dhidi ya Kenya ni lile lililotokea katika kambi ya el-Adde ambako wanajeshi zaidi ya 50 kutoka Kenya waliuawa.Chanzo irib

Israel yaomba kusaidiwa kuzungumza na HAMAS

Israel yaomba kusaidiwa kuzungumza na HAMAS Waziri Mkuu wa utawala wa Kizayuni ameiomba Ujerumani iinasihi Harakati ya Mapambano ya Kiislamu ya Palestina HAMAS ikubali kubadilishana mateka wa Kipalestina kwa viwiliwili vya wanajeshi wawili wa utawala wa Kizayuni vilivyoko mikononi mwa Hamas.

Mtandao wa habari wa Palestine Today umemnukuu Benjamin Netanyahu, Waziri Mkuu wa utawala ghasibu wa Kizayuni akiliambia gaeti moja la Israel kuwa, viongozi wa Ujerumaini wamekubali kuwa wapatanishi katika suala zima la kubadilishana na Hamas, mateka wa Kipalestina kwa viwiliwili vya wanajeshi wawili wa Israel.

Amesema, katika miaka ya huko nyuma pia Ujerumaini iliwahi kuisaidia Israel katika suala kama hilo, hivyo hivi sasa anaiomba tena iusaidie utawala wa Kizayuni.

Wanamapambano wa Palestina waliwateka nyara wanajeshi hao vamizi wa Israel wakati walipouvamia Ukanda wa Ghaza katika mashambulizi ya siku 50 yaliyoanzishwa na Israel dhidi ya ukanda huo uliozingirwa kila mahali.Chanzo irib

Kiongozi ataka wananchi washiriki vilivyo ktk uchaguzi

Kiongozi ataka wananchi washiriki vilivyo ktk uchaguziKiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu amesema kuwa, kujitokeza kwa wingi na kwa mwamko wananchi wa Iran katika chaguzi mbili zijazo za Majlisi ya Ushauri ya Kiislamu (Bunge la Iran) na ule wa Baraza la Wanavyuoni Wataalamu la kumchagua na kusimamia kazi za Kiongozi Muadhamu kutabatilisha njama za maadui.

Ayatullah Ali Khamenei amesema hayo leo wakati huu wa kukaribia maadhimisho ya tukio la Februari 18, 1978 la wananchi wa Tabriz, mbele ya maelfu ya wananchi wa matabaka mbalimbali wa mkoa wa Azerbaijan Mashariki na kusisitiza kuwa, chaguzi mbili za tarehe 26 mwezi huu wa Februari ni dhihirisho la mwamko wa wananchi wa Iran katika kuulinda mfumo wa Jamhuri ya Kiislamu, uhuru na heshima ya taifa lao. 

Amesisitiza kuwa, kushiriki kwa wingi na kwa mwamko wananchi katika chaguzi hizo kutafelisha tamaa ya maadui wanaotaka wananchi wa Iran wasusie chaguzi hizo.

Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu ameongeza kuwa, adui anafanya njama za kila aina ili afikie malengo yake kupitia uchaguzi, hivyo wananchi wa Iran ambao ndio wamiliki hasa wa nchi hii, wanapaswa kuelewa uhakika wa mambo na kutoruhusu kufanikiwa njama hizo za adui.

Amesema siasa za Marekani na nchi nyingi za Ulaya ziko chini ya ushawishi na ubeberu wa kanali za Kizayuni na kusisitiza kuwa, hata hatua zilizochukuliwa na Wamarekani katika kadhia ya nyuklia, navyo vinapaswa kuangaliwa kwa jicho hilo hilo.

Aidha Ayatulah Khamenei amewashukuru wananchi kwa kujenga hamasa ya kipekee kwenye maandamano ya kuadhimisha ushindi wa Mapinduzi ya Kiislamu tarehe 11 mwezi huu wa Februari na kuongeza kuwa, jambo hilo linaonesha namna wananchi wa Iran walivyo macho, wasivyotetereka na walivyo na azma ya kweli ya kufanikisha malengo yao matukufu.Chanzo irin