Friday, November 30, 2018

"Wahitimu wa Elimu ya Dini Muende Mkalinganie Umoja, Upendo na Mahusiano Mazuri"-Maulana Sheikh Jalala


Kiongozi Mkuu wa Waislamu Shia Ithnasheriya Tanzania Maulana Sheikh Hemed Jalala amewataka Wanafunzi wa Dini ya Kiislamu wahubiri Umoja, Upendo, mahusiano mazuri na utulivu pindi wanapokuwa wamemaliza masomo yao.

Maulana Sheikh Jalala amesema hayo katika Kikao na Waandishi wa Habari ikiwa ni katika kukaribisha kumbukizi ya Mazazi ya Mtume Muhammad (s.a.w.w),iliyofanyika jana masjid Ghadir, Kigogo Post Dar es salaam.

“Tumewaomba wale ambao wamemaliza Masomo yao katika chuo hiki, Seminari hii ya Imam Swadiq (a.s) waende wakalinganie Umoja wa watanzania, waende wakalinganie Upendo wa watanzania, waende wakalinganie mahusiano mazuri ya watanzania, waende wakawalinganie watu wakae vizuri katika nchi hii na kuboresha utulivu tulionao” amesema Sheikh Jalala

Aidha Maulana Sheikh Jalala amesema kuwa kwa kuadhimisha kumbukumbu ya kuzaliwa Mtume Muhmmad (s.a.w.w), Masjid Ghadir umejipanga kuimarisha Mahusiano mema katika ya Kata ya Kigogo na Tanzania kwa Ujumla ili kuleta amani na Utulivu katika maisha yetu ya kila siku.

“Mtume Muhammad (s.a.w.w) alikuwa ni mtu wa Mahusiano Mazuri, Msikiti wa Kigogo wa Masjid Ghadir, katika kuadhimisha mazazi ya Mtume Muhammad (s.a.w.w) umejipanga kuhakikisha  kwamba mahusiano yanakuwa mazuri kwa watu wote wanaoishi kata hii ya Kigogo na Tanzania kwa Ujumla.” amesisitiza Sheikh Jalala

Kwauapnde wake Mkuu wa Kituo cha Al-Mustafa Khairiya Sheikh Ali Mwazoa amewataka Watanzania kuwa wazalendo katika kuipenda nchi yako katika kuhakikisha jamii yako katika eneo unaloishi wanakuwa salama na Amani.

“Mtume Muhammad (s.a.w.w) anasema kuipenda nchi yako ni katika imani” nchi inamaana ya watu, lazima ifikie uwapende watu wan chi yako, watu wa kijiji chako, watu wa mji wako,kuipenda nchi yako ni kuhakikisha mazingira ya nchi yako yanakuwa ni salama na amani kwa maisha ya wanadamu na maisha ya viumbe kwa Ujumla” Amesema Sheikh Mwazoa.