Monday, January 13, 2014

Rais wa Marekani kuzuia vikwazo vipya dhidi ya Iran

Rais Barack Obama wa Marekani ametishia kupiga kura ya veto muswada wowote wa vikwazo vipya dhidi ya Iran wa Baraza la Seneti la nchi hiyo wakati huu ambapo Jamhuri ya Kiislamu na nchi za kundi la 5+1 zinapojitayarisha kuanza kutekeleza makubaliano ya nyuklia ya Geneva.

Obama amesema katika taarifa yake ya maandishi kwamba kuweka vikwazo vipya dhidi ya Iran kutahatarisha juhudi za utekelezaji wa makubaliano ya mwezi Novemba mjini Geneva.

'Nitapiga veto muswada wowote wa vikwazo vipya dhidi ya Iran katika kipindi hiki cha mazungumzo ya kundi la 5+1 na Iran', amesisitiza Obama na kuongeza kuwa hatua kama hiyo inaweza kukwamisha juhudi za kutatua kadhia hii kwa amani.

Muswada wa vikwazo vipya vya Marekani dhidi ya Iran umetayarishwa na Seneta wa chama cha Republican Bob Menendez.

Jamhuri ya Kiislamu ya Iran imesisitiza kuwa haiwezi kufanya mazungumzo chini ya vitisho na mashinikizo na kwamba iwapo Marekani itapasisha vikwazo vipya hatua hiyo itakuwa na maana kuwa makubaliano ya nyuklia ya Geneva yamekufa.
Chanzo.irib.ar

TAARIFA YA TAHADHARI YA MVUA KUBWA NA UPEPO

                  JAMHURI YA MUUNGANO WA TANZANIA


WIZARA YA UCHUKUZI MAMLAKA YA HALI YA HEWA TANZANIA
Simu: 255 22 2460735/2460706
FAKSI: 255 22 2460735/2460700 S.L.P. 3056
Barua pepe: met@meteo.go.tz DAR ES SALAAM
Tovuti: www.meteo.go.tz
……………………………………………………..
Taarifa kwa umma: Kunatarajiwa kuwepo na upepo mkali, mawimbi makubwa na mvua kubwa.
Taarifa Na.
201401-03
Muda wa Kutolewa
Saa za Afrika Mashariki
Saa 4 Asubuhi
Daraja la Taarifa:
Tahadhari
Kuanzia:
Tarehe
14 Januari, 2014
Mpaka:
Tarehe
16 Januari, 2014
Aina ya Tukio Linalotarajiwa
1. Hali ya Upepo mkali unaozidi kilomita 40 kwa saa pamoja na mawimbi makubwa zaidi ya mita 2.0
2. Vipindi vya mvua kubwa (zaidi ya mm 50 ndani ya saa 24)
Kiwango cha uhakika:
Wastani (60%)
Maeneo yanayotarajiwa kuathirika
1. Upepo mkali: Pwani ya mikoa ya Tanga, Dar es Salaam, Pwani, Lindi, Mtwara pamoja na visiwa vya Unguja na Pemba
2. Mvua kubwa: Mikoa ya Rukwa, Mbeya , Njombe, Ruvuma, Mtwara pamoja na kusini mwa mkoa wa Morogoro
Maelezo:
Hali hii inatokana na kuimarika kwa mfumo wa mgandamizo mdogo wa hewa kusini magharibi mwa Bahari ya Hindi, maeneo ya mkondo wa Msumbiji. Mfumo huu unatarajiwa kuvuta upepo kutoka Pwani ya Somalia na misitu ya Congo.
Angalizo:
Watumiaji wa bahari na wakazi wa maeneo hatarishi wanashauriwa kuchukua tahadhari.
Maelezo ya Ziada
Mamlaka ya Hali ya Hewa inaendelea kufuatilia hali hii na itatoa mrejeo pale itakapobidi.
Imetolewa na
Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania

Malinzi atembelea kituo cha Alliance

Rais wa Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF), Jamal Malinzi atafanya ziara ya siku moja kutembelea kituo cha mpira wa miguu wa vijana cha Alliance cha jijini Mwanza.


Lengo la ziara hiyo ni kuangalia jinsi Alliance inayoendesha shughuli zake ili Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) liweze kushirikiana na kituo hicho kwa karibu.

Rais Malinzi katika ziara hiyo atakayoifanya keshokutwa (Januari 15 mwaka huu) atafuatana na Mwenyekiti wa Kamati ya Mpira wa Miguu kwa Vijana, Ayoub Nyenzi na mjumbe wa Kamati ya Utendaji ya TFF, Ramadhan Nassib.

Alliance inatarajia kufanya mashindano yatakayoshirikisha vituo vyote vya kuendeleza mpira wa miguu kwa vijana (academy) wiki ya tatu ya Februari mwaka huu jijini Mwanza.

Mashindano hayo yatashirikisha timu za umri wa miaka 13, 15 na 17 ambapo Alliance itagharamia malazi, chakula na usafiri wakati timu hizo zikiwa jijini Mwanza.

RAMBIRAMBI MSIBA WA MCHEZAJI BONIFACE NJOHOLE
Shrikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) limepokea kwa masikitiko kifo cha mchezaji wa zamani wa timu ya Reli Morogoro, Boniface Njohole kilichotokea jana (Januari 12 mwaka huu) mkoani Morogoro.

Njohole ambaye alikuwa mjumbe wa Kamati ya Ufundi na Mashindano ya Chama cha Mpira wa Miguu Mkoa wa Morogoro (MRFA) hadi umauti unamkuta anatarajia kuzikwa kesho (Januari 14 mwaka huu) kijijini kwao Mngeta wilayani Ifakara.

Msiba huu ni mkubwa kwa jamii ya mpira wa miguu kwani alitoa mchango akiwa mchezaji, kocha na kiongozi kwa nyakati tofauti, hivyo mchango wake tutaukumbuka daima.

TFF tunatoa pole kwa familia ya marehemu Njohole, klabu ya Reli na MRFA na kuwataka kuwa na subira na uvumilivu katika kipindi hiki kigumu cha msiba huo mzito. Pia TFF itatoa ubani wa sh. 200,000 kwa familia ya marehemu kama rambirambi zake.

Bwana alitoa, Bwana ametwaa jina lake lihimidiwe. Amina

YAHYA KUFUNGA SEMINA YA WAAMUZI, MAKAMISHNA
Mwenyekiti wa Bodi ya Ligi Kuu ya Tanzania (TPLB) ya Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF), Hamad Yahya atakuwa mgeni rasmi katika ufungaji wa semina ya waamuzi na makamisha.

Semina hiyo ya siku mbili itafungwa kesho (Januari 14 mwaka huu) saa 4 asubuhi kwenye ukumbi wa mikutano Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.

Waamuzi zaidi ya 100 na makamishna 50 wanashiriki katika semina hiyo. Makamishna hao ni baadhi ya wale wanaosimamia mechi za Ligi Kuu ya Vodacom (VPL) na Ligi Daraja la Kwanza (FDL).

Kwa upande wa waamuzi ni wale wa daraja la kwanza (class one) ambao ndiyo wanaochezesha mechi za VPL na FDL.

Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) linatarajia kuandaa semina nyingine baadaye mwaka huu kwa makamishna wapya wanaotaka kusimamia mechi za VPL na zile za FDL.

VITAMBUSHO KWA WAANDISHI WA MPIRA WA MIGUU
Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) linatoa vitambulisho vipya kwa waandishi wa habari za mpira wa miguu kwa ajili ya kuripoti mechi mbalimbali inayoziandaa na kuzisimamia.

Kila chombo cha habari kupitia Mhariri wake au Mhariri wa Michezo kinatakiwa kuwasilisha majina ya waandishi wake kwa barua maalumu ya ofisi pamoja na picha (soft copy) kwa ajili ya vitambulisho hivyo.

Orodha ya majina ya waandishi wakiwemo wapiga picha wanaoombewa vitambulisho hivyo iwekwe kwa umuhimu.

Kocha Mkuu wa Taifa Stars ameunda kikosi cha wachezaji 32.


Kocha Mkuu wa Taifa Stars, Kim Poulsen ameunda kikosi cha wachezaji 32 kwa ajili ya mechi ya kirafiki ya kimataifa dhidi ya Kenya (Harambee Stars) itakayochezwa Jumanne, Novemba 19 mwaka huu Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.

Hayo yamesemwa na Boniface Wambura Mgoyo, Kaimu Katibu Mkuu, Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) wakati akiongea na Wanahabari kuwa Kikosi hicho kinajumuisha wachezaji 16 walioitwa Taifa Stars inayodhaminiwa na Kilimanjaro Premium Lager, na wengine 16 kutoka Future Taifa Stars.

Aidha kasema kuwa Wachezaji walioitwa ni makipa wanne; Aishi Manula (Azam), Ally Mustafa (Yanga), Deogratias Munishi (Yanga) na Ivo Mapunda (Gor Mahia, Kenya). Mabeki ni Aggrey Morris (Azam), Ismail Gambo (Azam), Kelvin Yondani (Yanga), Michael Pius (Ruvu Shooting), Nadir Haroub (Yanga) na Said Moradi (Azam).

Viungo wakabaji ni Erasto Nyoni (Azam), Himid Mao (Azam), Shomari Kapombe (AC Cannes, Ufaransa) na Vincent Barnabas anayechezea Mtibwa Sugar ya Morogoro, Amri Kiemba (Simba), Athuman Idd (Yanga), Frank Domayo (Yanga), Haruna Chanongo, Hassan Dilunga (Ruvu Shooting), Jonas Mkude (Simba), Ramadhan Singano (Simba), Salum Abubakar (Azam) na William Lucian (Simba).

Hatahivyo amesema kuwa Viungo washambuliaji ni Faridi Musa (Azam), Joseph Kimwaga (Azam), Mrisho Ngasa (Yanga), Mwingi Kazimoto (Markhiya, Qatar) na Simon Msuva (Yanga), Elias Maguli (Ruvu Shooting), Juma Liuzio (Mtibwa SugarMbwana Samata (TP Mazembe, DRC) na Thomas Ulimwengu (TP Mazembe, DRC).

Vitendo vya ukatili wa kijinsia wazidi kuongezeka.

Vitendo  vya makosa  ya  ukatili  wa kijinsia  na watoto  vimezidi kuongezeka    katika wilaya ya Ilala  hadi kufikia  208  tofauti na  mwaka  jana ambapo   takwimu zilikuwa chini  kwa makosa 168.

Unyanyasaji huo unajitokeza katika sura mbalimbali kama vile vipigo,ukeketaji,ubakaji,mauaji ya wanawake na watoto wa kike,kurithi wajane pamoja na ukatili wa nyumbani.

Kauli  hiyo  ilitolewa  jana jijini Dar es Salaam na Kaimu  Kamanda wa  Mkoa wa Ilala  ambaye  pia ni mkuu wa upelelezi  mkoa wa kipolisi  Ilala, Juma Bwire,  wakati  alipokuwa  akizungumza  na waandishi  wa habari  kuhusiana na  vitendo vya  kikatili   wa  kijinsia  wanavyofanyiwa wanawake na watoto.

Kamanda Bwire amesema  kutokana  na vitendo vya kikatili  kuzidi kuongezeka, Jeshi  la Polisi  limekuja na mkakati endelevu kwa ajili ya kuwasaidia  waathirika wa vitendo hivyo ambapo leo watanzidua  kituo  cha kulelela  watoto waishio katika mazingira hatarishi.

Amesema kuwa huduma katika  kituo hicho zitatolewa na wataalamu waliopata mafunzo  ya kutosha ili kuweza  kutatua  kero  zinazohusiana na   masuala  ya kijinsia na suluhisho la  muathirika  litatatuliwa na kupatiwa  ufumbuzi wa pamoja  kwani  huduma zote za kipolisi  zitapatikana  hapo katika kituo hicho.


Hatahivyo amesema  katika kuadhimisha siku 16 za ukatili wa kijinsia leo kutakuwa na maandamano ambayo yataanzia  katika Ofisi  ya  Kipolisi  Mkoa wa Ilala na  kumalizikia Viwanja  ya mnazi  mmoja.