WAZIRI MKUU
Kassim Majaliwa amesema Serikali haitavumilia kuona mamia ya vijana
waliofaulu mitihani ya darasa la saba na kuchaguliwa kuingia kidato cha
kwanza wanabaki nyumbani eti kwa kuwa hakuna madarasa ya kutosha.
“Serikali
haitaridhika kuona vijana waliofaulu vizuri wanashindwa kwenda kidato
cha kwanza. Halmashauri zilijua tangu mapema ni wanafunzi wanaenda shule
za msingi kwa hiyo inataka kuona wote waliofaulu wanakwenda sekondari
kwa asilimia 100,” amesema.
Ametoa kauli
hiyo leo mchana wakati akizungumza na viongozi na watendaji wa mkoa wa
Lndi mara baada ya kupokea taarifa ya mkoa huo kwenye Ikulu ndogo
wilayani Nachingwea. Waziri Mkuu amewasili wilayani Nachingwea akiwa
njiani kuelekea Ruangwa kwa mapunziko ya mwisho wa mwaka.
Amesema
Serikali ya awamu ya tano imedhamiria kutoa elimu ya bure kwa kila mtoto
sasa iweje watoto wengine wanafaulu na wanashindwa kujiunga na elimu ya
sekondari. “Tumesema elimu ni bure hakuna sababu ya kufanya wengine
wasiende shule wakati azma ya Serikali ni kutoa elimu ya bure.
Hakikisheni wote wanaingia katika chaguo la kwanza,” amesema.
Amewataka Wakuu
wa Wilaya na Wakurugenzi wa Halmashauri ambazo zimefaulisha wanafunzi
lakini hazina madarasa na madawati ya kutosha warudi mezani na kujipanga
upya ili kuhakikisha wanafunzi wote waliofaulu wanapangwa na kuanza na
wenzao katika chaguo la kwanza kwani wakisubiri chaguo la pili wanakuwa
wamechelewa.
“Kama
tumepokea vijana wengi kwenye udahili wa kidato cha kwanza, ni dhahiri
kuwa ,tutapata Vijana wengi watakaomaliza kidato cha nne. Sote tunajua
kuna agizo la kila tarafa kuwa na sekondari moja ya kidato cha tano na sita, nataka utekelezaji wa agizo hili usimamiwe kuanzia sasa.”
“Tafuteni moja
kati ya shule kwenye tarafa zenu na ipandishwe hadhi kwa kuwekewa
miundombinu inayotakiwa ya bwalo, jiko, mabweni, mifumo ya maji,
madarasa na vyoo vya kutosha,” amesema.
Katika hatua
nyingine, Waziri Mkuu amesema atafuatilia ili abaini ni kwa nini taasisi
ya maghala ya Serikali inadai tozo kwa wakulima wanaohifadhi mazao
kwenye maghala hayo.
Waziri Mkuu
amesema atapitia sheria ya kuanzishwa kwa taasisi hiyo ili kuona kama
inaruhusu tozo hizo na kuangalia sheria gani inawaruhusu kutoza kodi.
Alihoji inakuwaje taasisi ya Serikali inatoza tozo kwenye maghala ambayo
yamejengwa na wananchi.
Akitoa mfano
kuhusu ghala la Liwale, Waziri Mkuu amesema: “Kuna viagency vimeanzishwa
kazi yao ni kutoza mapato tu. Inakuwaje kunakuwa na taasisi imekaa tu
na kuanza kutoza tozo kwa wananchi wanaotumia facility za Serikali.
Sheria ya kutoza tozo imetokana na nini na hizo zinakwenda kwa nani, je
srikali imeanza kufanya biashara?,” alihoji.
“Nimepata
taarifa kuwa walikuja kuzuia mazao yasitoke hadi wao walipwe, hapana huu
siyo utaratibu. Ni kwa nini tuwanyang’anye fedha wale waliojenga ghala?
Wao walijenga ghala kutokana na ubunifu halafu unasema unawapa sh. 7/-
kwa kilo wakati wewe umetoza sh.25/- kwa kilo moja. Hapana hilo
halikubaliki,” amesisitiza.
Waziri Mkuu
amesema kama Serikali inaruhusu kuwepo kwa tozo hizo kwa jambo ambalo
wananchi wamelibuni wenyewe, basi ilipaswa kudai kodi na hiyo kodi
ilitakiwa kukusanywa na Mamlaka ya mapato Tanzania (TRA) na siyo
vinginevyo.
Waziri Mkuu
amesema atafuatilia wakala mbalimbali walioanzishwa kwenye wizara kwani
kuna nyingine zinafanya kazi ambazo zilistathili kufanywa na idara
kwenye wizara mama.
IMETOLEWA NA:
OFISI YA WAZIRI MKUU,
JUMANNE, DESEMBA 27, 2016.