Wednesday, December 26, 2018

“Amani iwe juu yangu siku niliyozaliwa, siku nitakayokufa na siku nitakayofufuliwa” Quran 19 aya 33.Maneno ya Nabii Issa (a.s) au Yesu Kristo

Kiongozi Mkuu wa Waislamu Dhehebu la Shia Ithnasheriya Tanzania Maulana Sheikh Hemed Jalala (kushoto) akimkabidhi Kadi ya Krismas Askofu Banza Suleimani kwa Niabaa ya Wakristo wote Tanzania na Duniani, jana katika Kikao na Waandishi wa Habari cha Kutoa Salamu za Krismas na Mwaka Mpya, Kigogo Post Jijini Dar es salaam.

Bismillah Rahmani Rahimu
“Amani iwe juu yangu siku niliyozaliwa, siku nitakayokufa na siku nitakayofufuliwa” Quran 19 aya 33.Maneno ya Nabii Issa (a.s) au Yesu Kristo

Watanzania wenzangu Waislamu na Wakristo, Amani ya Mwenyezi Mungu iwe kwenu nyote.

Katika siku hii ya leo sisi kama Waislamu wa Madhehebu ya Shia Ithnasheriya Tanzania tunapenda kutoa Mkono wa Kheri , Mkono wa Baraka, Mkono wa Fanaka kwa watanzania wote wakristo na wale wasiokuwa wakristo kwa mnasaba huu na kwa eid hii kubwa ya kuzaliwa Yesu Kristo au Issa       Ibn Mariam.

Tunatoa Mkono huu wa Kheri, Mkono huu wa Baraka uliojaa Mahaba, uliojaa Upendo, uliojaa Ushirikiano, uliojaa uzawa, uliojaa Utanzania, uliojaa kupenda nchi yetu kama watanzania sote tunaokusanywa na jina la Tanzania nan chi ya Tanzania, Namuomba Mungu wakristo wote wa Tanzania, Waafrika na Duniani Waisheherekee Eid hii kubwa ya Mazazi ya Yesu Kristo kwa kuzidi Upendo , kwa kuzidi Maelewano na kuzidi Mshikamano.

Napenda katika tukio hili wa Eid hii ya Krismas, Furaha hii ya Krismas kwa ndugu zetu wakristo wa Tanzania na wengine, napenda ninakili Quran takatifu katika sura ya 19 aya ya 33, Quran 19 aya 33 Mwenyezi Mungu anazungumzia Mazazi ya Nabii Issa (a.s) au Mazazi ya Yesu Kristo anasema Maneno yafuatayo “Maneno haya anayatamka  Yesu Kristo au Issa ibn Mariam (a.s) ndani ya Quran Surat Mariam aya ya 33 anasema Yesu au Issa.

“Na amani iwe kwangu Mimi siku niliyozaliwa na siku nitakayo Kufa na siku nitakayofufuliwa nikiwa hai” Maneno haya ameyatamka Nabii Issa (a.s) au Yesu Kristo wakati amezaliwa bado ni Mtoto Mdogo, Mayahudi wanamtilia Shaka Mariya Bikira au  Mariamu ,kwamba Vipi umempata Mtoto kabla ya kuolewa? Anadhibitisha Yesu Kristo au Issa (a.s) yakwamba Amani iwe juu yangu siku hii ya leo na siku nitakapo kufa na siku nitakapo fufuliwa.

Maneno haya yanatufunza nini? Na huu ndio ujumbe Muhimu wa Krismas yetu hii ya mwaka 2018 na 2019, kwamba Yesu Kristo na Mitume wengine wote, Yesu Kristo au Issa (a.s) anazaliwa, anachozaliwa nacho anasema nimezaliwa  kuenzi amani ndio kitu cha kwanza ametoka nacho, kwahiyo huu ni Ujumbe Mkubwa unaozungumzwa ndani ya Quran katika siku hii ya mazazi ya Yesu Kristo au Issa (a.s), mafunzo ya kuenzi amani, lakini kuenzi amani katika Nyanja gani?

Ni katika Nyanja tano Muhimu  lazima kuenziwa amani, Nyanja ya kwanza lazima kuenziwa amani kwenye Nyanja na kiwango cha mtu mmoja mmoja, lazima kila Mwanadamu aishi kwa amani kama alivyoitangaza Issa (a.s) au Yesu Kristo siku anayozaliwa , amani iwe kwangu siku nilipozaliwa , siku nitakapo kufa na siku nitakapo fufuliwa , maisha yangu yote ni maisha yanayogubikwa na amani na mitume wote maisha yao yaligubikwa na amani mpaka siku yao ya mwisho.

Kwahiyo ni lazima tuenzi amani kwa kiwango cha mtu mmoja mmoja, mtu anapofanya kazi anapotekeleza wajibu wake huyo amekaa kwa amani, Mtu anapomuabudu Mungu, Jumapili akaenda Kanisani, Ijumaa akaenda Msikitini huyo anaishi kwa amani, mtu anaekaa Vizuri na Jiraani na wenzake huyo anaishi kwa amani.

Pili kuishi kwa amani kwa kiwango cha familia, familia yoyote inayopendana , baba anaependana na watoto wake, anaependana na mkewe, hiyo ni familia inayoishi kwa amani. Familia yoyote inayowafundisha watoto inayowapeleka watoto shule wasome ,wajifunze, ni familiya inayoishi kwa amani. Familiya inayoishi katika kulinda ada,kulinda taratibu za Kiafrika, za Kikabila, ,mambo mazauri tuliyokuwa nayo ya kiafrika kuyaenzi huku ni kuenzi amani.

Jambo la tatu ni amani kwa ustawi wa Kijamii, Jamii amabyo haitumii madawa ya Kulevya, jamii ambayo haina mambo ya Ushoja, jamii iliyosalimika na mambo ya mahusiano machafu na mabaya, hiyo ni jamii inaishi kwa amani.kwa hiyo jamii iliyosalimika na hayo ni jamii inayoishi kwa amani.

Kwahivyo siku hii ya Mzazi ya Issa (a.s) au Yesu Kristo ametangaza kwamba yeye amezaliwa kwa amani, ameishi kwa amani na atakufa kwa amani Tuienzi amani tutakuwa tumemuenzi Issa  (a.s) , tukienzi amani tutakuwa tumemuenzi Yesu Kristo.

Jambo la Nne ni kuilinda amani au ni kuitazama amani kwenye kiwango cha Kitaifa, Taifa linaloenzi amani ni taifa la aina gani? Ni Taifa linalojitahidi kufuta Ujinga kwa wtu wake, taifa linaloishi kwa amani ni taifa linalojitahidi kufuta maradhi katika jamii yake, taifa linalohimiza watu wake wafanye kazi kwa bidii, taifa ambalo linawatumikia watu wake, hilo ni taifa linaloenzi amani na linaloishi kwa amani.

Mwisho ni kuenzi amani kwa mustawa wa Kimataifa, yoyote yale ambayo yameathiri mataifa mengine, yamesababisha uvunjifu wa amani uwepo katika mataifa mengine, kuenzi amani kimataifa nikujitahidi yale yote mabaya yasifike katika ardhi ya Tanzania. “Amani iwe juu yangu siku niliyozaliwa, siku nitakayokufa na siku nitakayofufuliwa” Quran 19 aya 33.
Huu ni Ujumbe wa Yesu Kristo au Yesu (a.s) ndani ya Quran siku aliyozaliwa , ni Mtu wa Amani ni mpenda amani, ni mpenda watu nan i mpenda jamii na hayo ndio maisha ya Mitume wote akiwemo Mtume Muhammad (s.a.w.w).

Nawatakieni Krismas Njema, nawatakieni watanzania wanaoienzi amani, wanaopenda amani, wanaokaa Vizuri, wanaoelewana na wanaoshikamana, asanteni sana na Mungu awabariki katika Krismas yenye Baraka na kheri tele, Mungu ibariki Tanzania.
                                                                                                                                                                          Imetolewa na:                                                                                    Maulana Sheikh Hemed Jalala                                                   Kiongozi Mkuu wa Waislamu Dhehebu la Shia Ithnasheriya Tanzania