Bislamillah Rahmani Rahim
Ndugu zangu Waandishi na Watanzania Wenzangu
Amani ya Mwenyezi Mungu iwe kwenu Nyote.
Siku ya Baba Duniani kwa Kuzaliwa Imam Ali Ibn Abutwalib (a.s).
Siku hii ya leo ambayo kwa tarehe ya Kiislamu ni sawa na
Tarehe 13 mwezi wa Rajab mwaka wa 1440, ambao ni sa /\wasawa na terehe 20, mwezi
wa 3 mwaka 600 AD.Mwaka huo unakumbana na siku hii ya leo ambayo waislamu
duniani, hususan Shia Ithnasheriya tunakumbuka siku ya kuzaliwa Imam au
Kiongozi Ali (a.s) ambae ni Imam wa Kwanza na Kiongozi wa Kwanza baada ya Mtume
Muhammad (s.a.w.w) kuondoka duniani.
Mazazi ya
Imam Ali (a.s) au Kiuongozi Ali (a.s) baada ya Mtume (s.a.w.w) ni muhimu
kukumbukwa kwa mambo yafuatayo:
Jambo la kwanza, napenda tutambue huyu
tunaemzungumza mahali alipozaliwa , alizaliwa ndani ya al kaaba, yaani kwa
ibara nyingine nzuri ndani ya ile nyumba ambayo waislam wote duniani
wanapofanya ibada zao iwe ni dua iwe ni swala, iwe ni ibada nyingine yoyote
wanaelekea pale mahala panapoitwa al kaaba, pale ndipo alipozaliwa muheshimiwa huyu anaeitwa Imam Ali (a.s).
Kitendo cha kuzaliwa mahala pale kinatupa sisi tutafakari
baadhi ya mambo, kwanini amezaliwa pale?, nitazungumza nukta tano za yeye
kuzaliwa pale.Nukta ya kwanza alizaliwa pale ambapo ni mahala pa Ibada ili iwe
ni darasa kwetu sisi walimwengu, kwetu sisi wanadamu, kitu kinachoitwa Umuhimu
wa Ibada, mahala pale alipozaliwa Imam Ali (a.s) ni mahala ambapo aliejenga
mahala pale ni Nabii Ibrahimu (a.s).
Nabii Ibrahimu tunavyomuita sisi waislamu, tunamwita ni baba
wa dini zote kwasababu Nabii Ibrahimu (a.s) ndio alimzaa Nabii Ismail (a.s) na
Nabii Islamail ndicho kizazi cha Mtume Muhammad (s.aw.w), Nabii Ibrahimu ndio
aliemzaa Nabii Isshaq/Isaka (a.s),Isaka ndio aliemzaa Nabii Yakub (a.s), Nabii
Yakub (a.s) ndie alieitwa Israel kwahiyo ndio aliezaa Mitume wote wa Israel
yaani Nabii Mussa (a.s), Nabii Issa / Yesu Kristo (a.s) na wengineo wote.
Kwahivyo alieijenga al kaaba ni Baba wa dini zote mahali hapo
ndipo alizaliwa Imam Ali (a.s), Imam wa Kwanza baada ya Mtume Muhammad
(s.a.w.w) ikiwa ni ishara ya umuhimu wa wanadamu wote kumuabudu mungu, binadamu
wote kumtii Mungu, binadamu wote kumsikiliza Mungu, mara kwa mara nilikuwa
nikisema Ibada sio kuswali tu, bali mwenyewe Mtume Muhammad (s.a.w.w)
anatuambia ya kwamba ibada kubwa zaidi ni kumtumikia mwanadamu.
kwa hivyo yoyote
anaemtumikia mjane amefanya ibada kubwa sana, yeyote anaemjali yatima amefanya
ibada kubwa sana, yeyote anaewajali watu wanaoishi katika mzingira magumu
amefanya ibada kubwa sana, hayo yote hayafungamani na dini yoyote bali ni mbali
yanayohusiana na dini zote za mbinguni.Siku hii ya kuzaliwa Imam Ali (a.s) Imam
wa kwanza ni siku ya kuenzi Ibada, na bora ya Ibadan i kumtumikia mwanadamu.
Jambo la pili: ya kuzaliwa Imam Ali (a.s) ndani ya
al kaaba linatupa darasa moja muhimu sana, linatupa darasa la umhimu wa kazi,
Sayyidina Ali (a.s) Imam Ali (a.s) katika historia yake ikimsoma ni mtu alikuwa
halali, ni mtu alikuwa mchapa kazi, ni mtu aliekuwa masaa 24 akifanya kazi,
kwasababu alikuwa akiamini, mungu anatutaka tufanye kazi.
Na nabii Ibrahimu (a.s) baba wa dini zote alifanya kazi yeye
na Nabii ismail,wakaijenga al kaaba wakaitengeneza ibada ya hijja, ambayo ibada
yenyewe ni kazi, kwahivyo tendo la kuzaliwa Sayyidina Ali (a.s) au Imam Ali
(a.s) tunakumbuka kuzaliwa kwake ndani ya al kaaba, moja ya darasa muhimu kwa
sisi watanzania wote pasina kubagua dini zetu ni funzo la kufanya kazi, na
kwamba kufanya kazi ndio kutatufanya tufikie mahala panapoitwa mahala muhimu na
mahala pakubwa.
Jambo la tatu:Kitendo cha kuzaliwa Sayyidina Ali
(a.s) kuzaliwa katika nyumba kubwa na nyumba muhimu, nyumba ya kwanza kuwekwa
duniani, nyumba inayofunza uadilifu ni nyumba inayoitwa nyumba ya Mungu
tunasoma darasa la Umuhimu wa Uadilifu, na ndio maana yeye mwenyewe Sayyidina
Ali (a.s) ameitwa nani?, yeye mwenyewe ameitwa kwamba ni sauti ya uadilifu.
katika vitu alivyopigana navyo alipigana navyo
Uadilifu,alipigana kuhakikisha watu wote wanapata haki zao, watu wote ni sawa,
hakuna tabaka fulani hilo ni bora kuliko tabaka linguine, hakuna akina fulani
wao wanahaki zaidi kuliko wengine, Kitendo cha Kuzaliwa Ali (a.s) ndani ya al
kaaba nyumba ya Uadilifu ni dalili ya kwamba Sayyidina Ali (a.s) ni mwalimu wa
waadilifu na kwamba sisi katika siku hii ya leo siku ya mazazi ya Imam Ali
(a.s) tuuwenzi uadilifu na kuukumbuka uadilifu, na kwamba kubakia kwetu,
kustawi kwetu ni kwasababu ya Uadilifu tutakao ufanya hapa duniani.
Jambo la nne: la muhimu la kuzungumzwa la kuzaliwa
Sayyidina Ali (a.s) ndani ya al kaaba tunapata darasa gani? Tunapata darasa la
Umoja, al kaaba nyumba ya kwanza iliyojengwa kumuabudu maungu, baada yake ndio
ikajengwa nyumba ya Jerusalem, al kaaba iliyojengwa na Nabii Ibrahimu (a.s)
baba wa dini zote, baba wa waislamu, baba wa wakristo, baba wa mayahudi ndie
mjenzi wa nyumba ile.
Kitendo cha kuzaliwa
Sayyidina Ali (a.s) pale ndani ni darasa moja muhimu, darasa kwamba Imam Ali
(a.s) ni bingwa wa kutengeneza Umoja, ni bingwa wa kuzifanya dini zote hizi
zikae mahala pamoja, nakwamba tukae tukifikiria na tukae tukitambua ya kwamba
waislamu, mayahudi, wakristo hawa wote baba yao ni mmoja.
Nae ni Yule mjenzi wa al kaaba na Yule mjenzi wa mahala pale
patakatifu mahala pale ndipo alipozaliwa Imam wa kwanza wa waislamu Sayyidina
Ali (a.s) au Khalifa wanne anavyojulikana kwa waislamu wengine. kwahivyo ni
somo muhimu, ni somo kubwa la kuenzi umoja wetu wa wawatanzania, umoja wetu wa
wanadini,waislam, wakristo na mayahudi, ndani ya ardhi yetu ya Tanzania.
Jambo la tano: Al kaaba mwenyezi mungu anasema
ndani ya Quran “yoyote mwenyekufika al kaaba, amefika mahala pa amani” kwahivyo
mungu ameweka nyumba maalumu akaiita ni nyumba ya kuenziwa amani, Sayyidina Ali
(a.s) alizaliwa katika nyumba hiyo, amezaliwa katika nyumba ya kuienzi amani.
Hii ni ishara na ni dalili ya kwamba moja katika mambo muhimu
ya kufanywa kukumbuka mazazi ya Imam Ali (a.s) Kiongozi huyu baada ya Mtume
Muhammad (s.a.w.w) ni kuenzi amani, ni kuenzi utulivu, ni kuenzi mshikamano, ni
kuenzi upendo kati ya watanzania kama watanzania, kati ya waafrika kama
waafrika,lakini vilevile kati ya wanadunia na kati ya wanaulimwengu wote.
Na kwamba nyumba ya kwanza iliyojengwa na nabii Ibrahimu
(a.s) baba wa dini zote, baba wa wakristo, baba wa waislamu,baba wa mayahudi na
akaziliwa Imam Ali (a.s) Kiongozi wa Waislamu ni dalili ya kwamba jambo la
amani ndio jambo ambalo limeasisiwa mahala pako mpaka leo tunapaona watu wa
dini zote, na kwa tukio hili napenda nigusie ya kwamba hii inaonyesha ya kwamba
waislamu, si katika nadharia ya Uislamu, wala si katika nadharia ya kiyahudi,
wala si katika nadharia ya wakristo kitu kinachoitwa kuvunja amani, kitu kinachoitwa
Ugaidi, kitu kinachoitwa kutumia nguvu.
Kulaani: Kwa tukio hili la kuzaliwa Imam Ali
(a.s) tunatoa msimamo wetu na tunatoa kauli yetu ya dhati kabisa ya kulaani
kitendo cha kigaidi kilichofanyika katika nchi ya Newsland kilichopelekea
mauaji ya waislamu wasiopungua takriban watu 50 ndani ya Msikitini, tumesema ni
kitendo cha kigaidi, na hii ni dalili ya kwamba
ugaidi hauna dini, hauna Ukristo, hauna Uyahudi wala hauna Uislamu, na
sisi tupo pamoja na yeyote ambae anaenzi watu wakae vizuri, anaenzi watu wake
kwa upendo na watu wakae kwa usalama.
Wito: wito wetu katika siku hii ya
kuzaliwa Imam Ali (a.s) au Kiongozi au Imam wa kwanza wa waislamu baada ya
Mtume Muhammad (s.a.w.w), wito wetu kwanza kwa viongozi wa dini waislamu na
wakristo nchini, tunatoa wito wa kuwa wawe Viongozi wa dini na nia ya dhati ya
kujenga umoja,mshikamano, ushirikiano na upendo kati yao kama alivyokuwa
Sayyidina Ali (a.s), Imam Ali (a.s) katika Utawala wake moja ya mambo muhimu
ukimsoma aliyoyajenga ilikuwa ni maelewano, upendo na mshikamano kati yao wao
wenyewe kama viongozi wa dini.
Na hayo yatafikiwa na Viongozi wa dini kuwa na mambo
yafuatayo, kwa ibara nyingine nzuri Viongozi wa dini watafikia mahala mahala
wanamshikamano, wanaupendo, ushirikiano na umoja watakapokuwa na mambo matatu
muhimu yakuyafanya, jambo la kwanza, wawe na tabia ya kutembeleana, jambo la
pili wawe ya kukaa pamoja,jambo la tatu wawe na tabia kupeana zawadi, kwenye
Krismasi, kwenye Eid, kwenye Maulid na matukio mengine.
Wito wetu wa pili, ili watanzania waishi kwa amani,kwa
utulivu, kwa Upendo na kwa umoja lazima tuishi kama mitume wa mungu
walivyoelekeza na kama Maimam , Viongozi akiwemo Sayyidina Ali (a.s)
walivyoelekeza, lakini vilevile kama vitabu vya mbinguni Taurati, Injili,
Zaburi na Qur’an vilivyoelekeza, vitabu vyote hivyo vimeelekeza
Upendo,Mshikamano, Umoja na watu kukaa Vizuri.
Mwisho: Mwenyezi Mungu nakuomba katika siku
hii ya kuzaliwa Imam Ali (a.s) Imam wa Kwanza baada ya Mtume Muhammad
(s.a.w.w), au Khalifa wan ne waislamu wengine, Mwenyezi Mungu nakuomba Tanzania
uipe amani, Tanzania uipe Utulivu, Viongozi wetu Mwenyezi Mungu uendelee kuwapa
Hekima,uwape busara, uwape muono wao wa kuwatumikia watanzania mpaka mwisho wa
masiku yao.
Na sisi kama watanzania tuwe na tabia ya kuombea Mungu
Viongozi wetu ili waweze kutuongoza katika njia iliyokuwa ya kisawasawa. Mungu
aibariki Tanzania, Mungu awabariki Viongozi wetu wote tuliokuwanao
wanaotuongoza, Asanteni sana Amani ya Mwenyezi Mungu iwe kwenu nyote.
Imetolewa na:
Maulana Sheikh Hemed Jalala
Kiongozi Mkuu wa Waislam Shia Ithnasheriya Tanzania
Tare:20.03.2019/13 Mwezi wa Rajab, 1440.
Masjid Ghadir, Kigogo Post Dar es salaam.
Masjid Ghadir, Kigogo Post Dar es salaam.