Afsia wa zamani wa Shirika la Usalama wa Taifa la
Marekani (NSA) amesema mifumo ya simu za iPhone na Android inatumiwa na
vyombo vya ujasusi vya Marekani kudukua na kunasa sauti na mazungumzo
ya watu katika maeneo mbalimbali ya dunia.
Edward Snowden amesema maelfu ya nyaraka za siri za shirika la
ujasusi la Marekani CIA zilizofichuliwa na mtandao wa WikiLeaks
zimethibitisha tena kwamba mashirika ya ujasusi ya Marekani yanadukua na
kunasa mazungumzo ya simu za kiganjani hususan zile zinazotumia mfumo
wa iOS wa simu za iPhone na ule wa Android.
Jumanne ya jana mtandao wa WikiLeaks ulichapisha sehemu ya kwanza ya
nyaraka na mafaili ya siri ya shirika la ujasusi la Marekani CIA katika
majmui iliyopea jina la Year Zero. Nyaraka hizo za siri zinafichua kuwa,
CIA imekuwa ikifanya ujasusi wa kunasa na kusikiliza mazungumzo ya watu
wanaotumia simu za iPhone zinazotengenezwa na kampuni ya Apple na zile
zinazotumia mifumo wa Android na Microsoft na vilevile televisheni za
Samsung kwa ajili ya kufanya ujasusi na kudukua sauti na mazungumzo ya
watu katika pembe mbalimbali duniani.
Afisa wa zamani wa Shirika la Usalama wa Taifa la Marekani (NSA)
Edward Snowden anasema kufichuliwa nyaraka hizo kunathibitisha tena
kwamba, mashirika ya ujasusi ya nchi hiyo yanajasisi na kunasa sauti za
watumiaji wa simu za kiganjani.
Afisa huyo wa zamani wa NSA alikimbia Marekani mwaka 2013 akiwa na
rundo kubwa la nyaraka za siri za mashirika ya ujasisi ya nchi hiyo na
kwa sasa amepewa hifadhi nchini Russia.