Thursday, September 12, 2019

Dini na Madhehebu Mengine waigeni Shia Ithnasheriya” Mhe. Kumbilamoto


Meya wa Manispaa ya Ilala Mhe. Omari Kumbilamoto (watatu kushoto) akishiriki Matembezi ya Amani ya kukumbuka Kifo cha Imam Hussein (a.s) Mtoto na Mjukuu wa Mtume Muhammad (s.a.w.w) katika maadhimisho ya siku ya Ashura juzi Dar es salaam.

Meya wa Manispaa ya Ilala Mkoa wa Dar es salaam Mhe. Omari Kumbilamoto amezitaka Dini na Madhehebu Mengine nchini kuwaiga Waislamu Shia Ithnasheriya katika namna yao ya kuadhimisha matukio ya Kiimani kwa kufanya mambo ya Kijamii katika jamii inayowazunguka bila kujali dini wala dhehebu.

Kumbilamto alisema hayo juzi katika Matembezi ya amani ya kukumbuka Kifo cha Imam Hussein (a.s) Mtoto na Mjukuu wa Mtume Muhammad (s.a.w.w) yaliyoandaliwa na Jumuiya ya Waislamu Khoja Shia Ithnasheriya Jamati Posta jijini Dar es salaam.

Meya wa Manispaa ya Ilala Mkoa wa Dar es salaam Mhe. Omari Kumbilamoto akiongea na Waandishi wa Habari punde tu baada ya kuanza kwa mataembezi ya Aamani.
“Kwasisi kwa Manispaa ya Ilala tumelipokea kwa faraja kwa kukumbuka kwao Kifo cha Imam Hussein (a.s) imekuwa na manufaa katika taifa letu, kwa hiyo niwaombe dini zingine na madhehebu mwengine  waige mfano wa Shia Khoja namna wanavyoweza kuadhimisha mambo yao ya kidini na vilevile wanavyotoa mchango katika jamii mfano damu na vilevile Matibabu ya Bure yanasaidia jamii , kwa hiyo mchango unasaidia katika serikali yetu ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania” alisema Mh.Kumbilamoto

“Tunawashukuru sana na Mwenyezi Mungu aweze kuwabariki, funzo kubwa ni la Amani kama ambavyo anasisitiza Mhe. Raisi Magufuli kama vile vile waumini wa shia Khoja wanaamini kuwa Imam Hussein (a.s) ni muumini wa Amani na utulivu, kwa hiyo ni tukio zuri”alisema Mh.Kumbilamoto

Kwa upande wake Kiongozi wa Waislamu Shia Ithnasheriya Maulana Sheikh Hemed Jalala alisema kuwa malengo ya kukumbuka Kifo cha Imam Hussein (a.s) ni kuienzi Amani ,Utulivu, Mshikano, Upendo na Uvumilivu uliopo kwa Watanzania

“Matembezi haya ya Amani mnayoyaona yaliyojaa huzuni ni kuenzi Umoja wa Mwanadamu,umoja wa Utu ambao alitoka kwa ajili yake Imam Hussein (a.s), Msafara wa Imam Hussein (a.s) historia inaeleza kwamba kuna kitu kilikuwa kimekosekana amani, utulivu mshikamano, busara na kuvumiliana haya ni mambo  yaliyokuwa yamekosekana na kusambaratika, Imam Hussein  (a.s) akakubali kuuwawa yeye na Kizazi chake kwanini? Kwasababu ya kurudisha Amani utulivu na mshikamano ndani ya jamii aliyokuwa nayo”alisema Sheikh Jalala



No comments: