Wednesday, June 8, 2016

“Ninatoa mkono wa Kheri na Fanaka kwa Watanzania wote kwa Mwezi wa Ramadhani na kuwataka Watanzania kuoneana huruma” Sheikh Jalala.

Kiongozi Mkuu wa Waislam, Dhehe Shia Ithnasheriya Tanzania Sheikh Hemed Jalala amewataka Waislamu na wasiokuwa waislamu kuitumia fursa ya mwezi Mtukufu wa Ramadhani kuachana na matendo yasiyompendeza Mungu na badala yake wajikite katika kuoneana huruma na kupendana miongoni mwao kwani kufanya hvyo ndiyo Mafundisho ya Mtume(s.a.w.w).

Akizungumza na Waandishi wa habari Masjid Ghadir, Kigogo Jijini Dar es salaam wakati wa tukio la kuukaribuisha Mwezi Mtukufu wa Ramadhani, Sheikh Hemed Jalala amesema Mwezi wa Ramadhani unamafundisho mengi lakini kubwa watu wanapaswa kuoneana huruma na kupendana.

Amesema Jamii haina budi kuhakikisha wanaitumia Ramadhani kwa kuwaonea huruma wazee, mayatima, vikongwe na majirani zao kwani kufanya hivyo kutaongeza ustawi wa Amani miongoni mwa jamii.

“Ninawapa Hongera Waislam wote wa Tanzania, Salama zinazo ambatana na Mkono wa Kheri na Baraka na fanaka na mafanikio kwa kuingia katika mwezi Mtukufu wa Ramadhani, Pia napenda kuwapa hongera Watanzania wote kwa Ujumla, Waislam  na Wasiokuwa Waislam, Waislam wakristo pamoja na dini zote zilizopo hapa Tanzania niwape mkono wa heri na baraka kwa kuingia mwezi huu Mtukufu wa Ramadhani” amesema Sheikh Jalala

Sheikh Jalala amelaani vikali  mauaji ambayo ameyaita ya kiigaidi yaliyotokea katika mikoa mbalimbali nchini huku akisema kuwa vitendo hivyo vinakwenda kinyume na Imani ya dini ya Kiislam na dini yoyote nchini na vinastahili kupingwa na kila mtanzania.

 
“Dini zote zilizoletwa duniani hazina mahusiano hata kidogo na hayo yanayotokea, sisi kama viongozi wa dini, kama Waislamu kama Mashia Inthna-Sheriya tunalaani kitendo hiki na kukipiga vita

“Bali ninatoa wito kwa wakazi wa maeneo yaliyokumbwa na ukatili huo endapo wataona au kubaini sura ngeni iwe mtaani au kwenye nyumba zao za ibada watoe taarifa mapema kwenye vyombo vya usalama” amesema Sheikh Jalala.


 Aidha amewataka watanzania kuchukua jukumu la kuwa walinzi wa maeneo wanayoishi na kuhakikisha kuwa wanatoa taarifa haraka pale ambapo wanaona watu au kikundi cha watu ambao hawaeleweki wakiwa katika maeneo yao huku akivitaka vyombo vya usalama kuhakikisha kuwa wanachukua taarifa za wananchi na kuzifanyia kazi mara moja ili kuepuka kutokea kwa matukio ya kigaidi na mauaji kama yaliyotokea mwezi huu.

“Tukumbuke kuwa siku za hivi karibuni kumekuwa na mfululizo wa matukio ya mauaji ya kutisha huku wengine wakichinjwa ambayo yaiyokea mkoani mwanza na mengine mkoani tanga matukio ambayo yameacha simanzi kwa watanzania walio wengi.”amesema Sheikh Jalala.