Friday, September 18, 2015

Jengo refu zaidi Afrika Mashariki na Kati lazinduliwa nchini Tanzania

Jengo refu zaidi lililokamilika Afrika Mashariki na Kati lazinduliwa nchini Tanzania.
PSPF Towers ni moja ya majengo machache marefu barani Afrika na ndiyo jengo refu zaidi LILILOKAMILIKA Afrika Mashariki na Kati, likiwa na urefu wa mita 147.
Majengo mengine marefu Afrika ni Carlton Centre (mita 223) lililopo Afrika Kusini, Hassan II Mosque (mita 210) lililopo Moroko, Ponte City (mita 173) lililopo Afrika Kusini, Necon House (Mita 160) lililopo Nigeria, Marble Tower (mita 152), Pear dawn (mita 152), Pear dawn (mita 152), Met Life Centre (mita 150) na 88 on field (mita 147) yote ya Afrika ya kusini.
Jengo hilo lililozinduliwa na Rais wa Tanzania Jakaya Kikwete, ujenzi wake ulitumia miaka minne tangu mwaka 2011 hadi 2015 limegharimu shilingi bilioni 139.20 za Tanzania lina maeneo ya ofisi na nyumba za makazi 88. Pia katika jengo hili kuna sehemu ya Mgahawa, Mabenki, Bwawa la kuogelea, Sehemu za kufanyia mazoezi, Maegesho ya Magari na sehemu nyingine muhimu.

NCCR-MAGEUZI"Hatuwezi kuitoa CCM kwa mbinu za ulaghai na ujanja-ujanja"

Makamu Mwenyekiti wa Chama cha NCCR-MAGEUZI,Reticia Ghati Mosore akizungumza na vyombo mbalimbali vya habari katika Hoteli ya Land Mark jijini Dar es Salaam  muda huu kuhusiana na ukiukwaji wa taratibu katika umoja wa Katiba ya Wananchi (UKAWA) na kutangaza kuendelea na mapambano nje ya umoja huo wa vyama pinzani.
 
UTANGULIZI
Sisi viongozi wa ngazi ya juu wa Chama cha NCCR-Mageuzi, Makamu Mwenyekiti, Katibu Mkuu tukiwa na Wajumbe wa Halmashauri Kuu ya taifa na viongozi wengine, tumekuja mbele yenu mtusaidie kufikisha ujumbe maalum kwa wanachama wetu na Watanzania wote wanaokiamini chama chetu,
Tumefika kuelezea kutoridhishwa na mwenendo wa ushirikiano wa vyama vinavyounda UKAWA. Tumekuja pia kuwaelezea ni hatua gani tulizoamua kuchukua kukabiliana na changamoto hii. 
Wengi wenu mnafahamu kuwa UKAWA ni Umoja wa Katiba ya Wananchi ulionzishwa wakati wa Bunge Maalum la Katiba kutetea Rasimu ya Katiba iliyotokana na maoni ya wananchi dhidi ya uchakachuaji uliokuwa unafanywa na CCM. 

UKAWA  siyo chama cha siasa bali umoja. NCCR-Mageuzi iliamua kujiunga na harakati hizi kwa nia njema ya kutetea maslahi ya taifa letu. Zaidi ya mwaka sasa tangu tujiunge na umoja huu, matokeo yake yamekuwa ni mabaya kwa uhai na ustawi wa chama chetu. Wakati vyama vingine vimezidi kuimarika ndani ya UKAWA, NCCR-Mageuzi imedhoofika. Hali hii haikubaliki.

MAKUBALIANO YA USHIRIKIANO BAINA YA VYAMA VYA UKAWA
Vyama vinavyounda UKAWA, vilisaini Makubaliano ya Ushirikiano katika Mkutano wa Hadhara kwenye viwanja vya Jangwani. Kitendo hicho kiliwavutia na kuwapa matumaini wananchi na wao wakazidi kutuunga mkono. Iliamuliwa kwamba tusiuwe vyama vyetu bali tuunganishe nguvu za vyama vyetu kama namna ya kujiimarisha kwa pamoja. 
UCHAGUZI WA SERIKALI ZA MITAA DISEMBA 2014.
Kabla ya Uchaguzi wa Serikali za Mitaa wa mwaka 2014, vyama vinavyounda UKAWA vilitiliana saini ya Mwongozo wa Ushirikiano katika Uchaguzi huo.
Licha ya kutiliana saini Makubaliano hayo, bado kulikuwa na ukiukwaji mkubwa na wa makusudi  wa Mwongozo huo.
Licha ya kuzijadili changamoto zilizojitokeza katika Uchaguzi huo, lakini hazikupatiwa ufumbuzi wowote.
Sisi tuliopo hapa tulionya mapema kuhusu mwenendo huu wa kuvunja makubaliano na tukaomba taratibu tulizokubaliana zitumike ili kurudi kwenye misingi ya UKAWA lakini hatukusikilizwa.

USHIRIKIANO KATIKA UCHAGUZI MKUU, OKTOBA 2015.
Licha ya changamoto zilizokuwepo, tuliamua kwa pamoja kwamba vyama vya UKAWA tuingie katika Uchaguzi Mkuu tukiwa na makubaliano ya ushirikiano, ikiwemo kuwa na mgombea mmoja wa Urais na kuachiana majimbo ya uchaguzi. 
Pia, katika kuendesha umoja huu, tuliunda vyombo vya kutusaidia ambavyo ni:-
Kamati ya Wenyeviti.
Kamati ya Makatibu Wakuu.
Kamati ya Ufundi.
Kamati ya Wataalam.
Pamoja na kuunda vyombo vya kuendesha UKAWA, tangu Januari 2015, bado tumeshindwa kujenga UKAWA imara na tuliyotarajia kwa manufaa ya wanaukawa  na wananchi kwa ujumla. 
Yafuatayo yamethibitisha hili jambo:
Tumeshindwa kuweka Kanuni za uendeshaji wa UKAWA kama tulivyokubaliana. Kwa maana hiyo, tunafanya mambo kiholela
Tumeshindwa kuunda Kamati zitakazoshughulikia migogoro baina ya vyama.
Tumeshindwa kuunda na kuzisimamia Kamati za Majimbo
Tumeshindwa kupata muafaka wa kuachiana majimbo. 
Mfano, NCCR – Mageuzi tuliachiwa majimbo 12 ya Kasulu Vijijini, Kigoma Kusini, Muhambwe, Kasulu Mjini, Vunjo, Ileje, Mbinga Mjini, Manyovu, Buyungu, Ngara, Nkenge na Korogwe mjini. Ikumbukwe kwamba, mwaka 2010, NCCR-Mageuzi ilisimamisha wagombea katika majimbo 67.
Kwa maana hiyo, UKAWA umeturidisha nyuma katika kupata wabunge na kuimarisha chama zaidi ya miaka 20 baada ya kuundwa kwake.

Licha ya kukubaliana kwamba NCCR-Mageuzi iachiwe majimbo 12, wenzetu wa vyama vingine katika UKAWA wamesimamisha wagombea katika majimbo 6 kati ya hayo. Wametuvunja moyo na kutuonyesha kwamba hawatujali. Na hata kule ambapo katika majimbo sita ambapo wametuachia bado wenzetu wanatufanyia fujo kuliko hata wanazotufanyia wanachama wa CCM. Tunamifano mingi ya kuonyesha ni jinsi gani wagombea wetu wanavyofanyiwa vurugu. 
Tumeshindwa kupata muafaka wa namna ya kuachiana wagombea udiwani katika kata nyingi.
Tumeshindwa kuonesha na kukubaliana kila chama kitapata nafasi gani na ngapi katika Serikali ya UKAWA.
Tumeshindwa kufuata utaratibu wa kumpata mgombea Urais wa UKAWA
Tumeshuhudia vurugu kubwa iliyoletwa ndani ya UKAWA na wanachama waliotoka CCM na wao kupewa umuhimu kuliko viongozi wa UKAWA. Zaidi ya Mbatia hakuna kiongozi wa NCCR-Mageuzi anayeshirikishwa, anayezungumza au aliyepo kwenye kampeni za mgombea Urais wa UKAWA.
Tumeshindwa kuwa na timu ya kampeni timu ya UKAWA, ambayo inagharamiwa na UKAWA na inatafuta fedha pamoja, kama ilivyokubaliwa.
Tunashuhudia UKAWA ambayo Chadema ndiyo UKAWA-Bara na CUF ndio UKAWA-Zanzibar. Chadema haijali Zanzibar na CUF haijali Bara. Na NCCR-Mageuzi haipo huku wala kule ikiendelea kudhoofika siku hadi siku.  
Tumeshindwa kuona uwazi katika matumizi ya fedha na maamuzi muhimu ya uendeshaji wa UKAWA.
Tumefadhaishwa na kuvunjwa kwa misingi ya kuanzisha kwa UKAWA.
Wakati NCCR imetii mgawanyo wa majimbo kwa vyama vinavyounda UKAWA, vyama vingine na hasa CHADEMA vimesimamisha wagombea kinyume cha makubaliano.

NINI KIFANYIKE NA UKAWA
Hatukuwaita hapa kuwaambia kwamba tunajiuzulu siasa kutokana na changamoto hizi. Tumeamua kupambana na kurudisha hadhi na heshima ya Chama chetu. Hatuwezi kubwaga manyanga. Tunataka kuitoa CCM madarakani kutokana na ulaghai na ujanja-ujanja wa miaka 50. Lakini hatuwezi kuitoa CCM kwa mbinu za ulaghai na ujanja-ujanja. Tunakwenda kukabidhiwa dhamana ya kuongoza nchi na Watanzania. Tunao wajibu wa kujiongoza vizuri ili tuwaonyeshe Watanzania kwamba tuna uwezo wa kuwaongoza vizuri. 



WITO WETU
Tunamshauri Mwenyekiti wetu, ndg. James Mbatia, aitishe vikao vya kikatiba ili tuweze kujadiliana kuhusu hatima ya chama chetu.
Tunashauri ndg. Mbatia asiwemsemaji wa CHADEMA wakati anakiacha chama chake (NCCR-Mageuzi)kinadhoofika. Kwa mfano, Dr. Slaa alipoishambulia Chadema hakuna kiongozi wa Chadema aliyemjibu isipokuwa Mbatia ndiye aliyeamua kujiingiza kwenye ugomvi ndani ya Chadema. 
Tutachangishana ili tusafiri kwenye majimbo na kata za wagombea wetu na kuwasaidia kwenye kampeni ili wasibaki wapweke kama yatima.

Tunasisitiza kwamba upinzani wa kweli nchini hauwezi kujengwa kwa njia za hila, kwa kukiuka taratibu za kidemokrasia tulizojiwekea wenyewe, kwa kukiuka misingi muhimu kama uadilifu, kwa kuweka mbele tamaa na maslahi binafsi kuliko taifa, kwa kutegemea propaganda. Tukifanya hivi, wananchi watashindwa kututoufautisha na CCM na wataamua kuchagua zimwi walijualo. Hatari hii tunaiona wazi kabisa.
……………………………
Leticia Ghati Mossore                        
                        Makamu Mwenyekiti (Bara)
NCCR-Mageuzi
17.09.2015

Mosena Nyambabe
Katibu Mkuu, NCCR Mageuzi

Kiongozi Ali Khamenei "Maadui Wanania ya Nchini Iran"

Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu Ayatullahil Udhma Ali Khamenei amesema kuwa maadui wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran wanafanya mikakati ya kubadili itikadi za jamii na kupenya katika vituo vya kutayarisha na kuchukua maamuzi hapa nchini.
Ayatullah Ali Khamenei ameyasema haya leo katika hadhara ya maelfu ya makamanda wa Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu (SEPAH) na kuongeza kuwa, kwa matarajio yasiyo na msingi ya kumalizika Mapinduzi ya Kiislamu, adui anafanya mikakati kupenya hapa nchini hususan katika masuala ya kisiasa na kiutamaduni, lakini kutambua vyema njama za adui, kuimarishwa moyo wa kimapinduzi na harakati ya kudumu kuelekea upande wa kutimiza thamani na matukufu vitamzuia kutimiza malengo yake.
Amesema kuwa Iran kamwe haijawa wala haitakuwa ya kwanza kuanza vita na kuongeza kuwa: Pamoja na hayo kwa kuwa Mapinduzi ya Kiislamu siku zote yanakabiliwa na hatari ya wapinzani na wakorofi, kuna udharura kwa jeshi la SEPAH kuwa macho na makini daima kwa ajili ya kukabiliana na vitisho hivyo.
Ayatullahil Udhma Ali Khamenei amesema kuwa, kumtambua adui ni miongoni mwa vipengee vya kulinda Mapinduzi. Ameongeza kuwa, maana ya adui ni ubeberu wa kimataifa ambao dhihirisho na kielelezo chake kamili ni Marekani, na vibaraka wake ni tawala zilizobakia nyuma na watu dhaifu kinafsi.

Kiongozi Muadhamu amesema kuwa, maadui wa Mapinduzi ya Kiislamu ni wale ambao miaka mingi iliyopita walikuja Mashariki ya Kati kwa nara na kaulimbiu za 'kuimarisha amani', 

'kupambana na ugaidi', 'kuleta demokrasia' na 'kuleta amani' lakini hii leo matunda ya kuwepo kwao hapa ni ukosefu wa amani, kujitokeza ugaidi na ukatili na kuzusha vita katika eneo hili.
 
Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu amekosoa vikali fikra za kipotofu na kijinga za matakfiri wanaokufurisha Waislamu na kusema: Uislamu unaotegemea akili na mapokezi, unaoegamia kwenye Qur'ani na mafundisho ya Mtume (saw) na Ahlubaiti zake (as) ndiyo msingi wa mapinduzi yetu na unaweza kutetewa kwa nguvu ya mantiki na kulinganiwa katika duru zote za dunia ya sasa.
 
Ayatullah Khamenei ametilia mkazo udharura wa jeshi la SEPAH kutilia maanani vitisho vyote zikiwemo njama za adui za kutaka kupenya nchini Iran kisiasa na kiutamaduni.Chanzo Irib