Habari kamili
Serikali imeweka mikakati madhubuti
kupambana na magonjwa yasiyoambukiza hapa nchini,hayo yamesema na Meneja
Masoko na Elimu kwa Umma toka Mfuko wa Taifa wa Bima ya
Afya ( NHIF) Bi Anjela Mziray wakati wa mkuatano na waandishi wa habari
leo jijini Dar es salaam.
Akieleza Bi Anjela amesema kuwa
Serikali kupitia Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya imekuwa ikichukua juhudi
za maksudi katika mapambano dhidi ya magonjwa yasiyoambukiza kama vile
kisukari, shinikizo la damu na Saratani za aina mbalimbali.
Akifafanua zaidi Bi Anjela amesema
programu hiyo imekuja kutokana na ukweli kwamba magonjwa haya yamekuwa
yakiongezeka na yamekuwa tishio na kusababisha vifo vya watu wengi nchini na
duniani ambapo takwimu za shirika la afya Duniani za mwaka 2012/2013 watu zaidi
ya milioni 35 hufa kwa sababu ya magonjwa yasiyoambukiza.
Bi Anjela aliongeza kuwa kati ya
waathirika wa magonjwa yasiyoambukiza milioni 28.1 wanatoka katika nchi
zinazoendelea ambapo kwa Tanzania magonjwa hayo husababisha vifo mara 4 zaidi
mijini ambavyo ni sawa na asilimia 12.8 wakati asilimia 3.1 wapo
vijijini.
Akitolea Mfano Bi Anjela
alisema katika zoezi la upimaji lililofanyika Dodoma Septemba, 2013 jumla ya
watu 591 walipimwa kati yao 14 sawa na asilimia 2.3 waligundulika kuwa na
kisukari, na 28 sawa na asilimia 5 walikuwa na shinikizo la damu, wakati
watu 128 sawa na asilimia 22 walikuwa na uzito uliokithiri.
Bi Anjela aliongeza kuwa katika
zoezi lililofanyika Mlimani City Jijini Dar es salaam ocktoba, 2013 watu 450
walipimwa, nusu yao waligundulika kuwa na uzito uliokithiri na katika zoezi
lililofanyika Zanzibar watu 273 walipimwa ambapo kati yao watu 10 sawa na
asilimia 3.6 waligundulika kuwa na kisukari, watu 83 sawa na
asilimia 30.4 walikuwa na uzito uliokithiri.
Naye Meneja Uhakiki na Madai
wa mfuko huo Dk.Clement Masanja alitoa wito kwa wananchi kuhusu umuhimu
wa kufanya mazoezi na kuzingatia lishe bora ili kujikinga na magojwa
yasiyoambukiza kama kisukari, msongo wa mawazo na shinikizo la damu.
Katika jitihada za Kutoa huduma bora
kwa wananchi Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya (NHIF) umebuni mkakati maalum
ambao unajulikana kama Afya Bonanza ambayo ni Kampeni ya kupima afya na kutoa
elimu juu ya magonjwa yasiyoambukiza na inakusudiwa kufanyika mikoa yote
hapa nchini ambapo Zoezi hilo lilizunduliwa rasmi Wilaya ya Temeke Jijini
Dar es salaam mwezi machi 2014.
No comments:
Post a Comment