Afisa wa ngazi za juu katika polisi ya Kenya
amesema vikosi vyote vya usalama nchini humo vina azma imara ya
kuangamiza kundi la kigaidi la Al Shabab.
Msemaji wa Polisi ya Kenya George Kinoti amenukuliwa akisema
maafisa wa usalama nchini humo watafanya kila wawezalo kung'oa mizizi ya
Al Shabab na kukabiliana na vitisho vyote vya usalama nchini humo.
Kinoti aidha amethibitisha habari ya kuuawa maafisa wawili wa Polisi
Kenya waliotoweka wakati Al Shabab walipovamia kituo cha polisi katika
kaunti ya Garissa. Amesema magaidi wa Al Shabab walichukua miili ya
polisi hao na kuipeleka Somalia.
Katika hujuma hiyo ya Alkhamisi iliyopita magaidi wa Al Shabab mbali
na kuua maafisa hao wa polisi pia walipora idadi kubwa ya risasi, silaha
na vifaa vya mawasiliano katika kituo hicho cha polisi.
Baadhi ya duru zinasema magaidi hao walipora risasi elfu 10 na
bunduki 13 za AK 47. Kundi la Al Shabab linafungamana na mtandao wa Al
Qaeda na hutekeleza hujuma za mara kwa mara dhidi ya raia na maafisa wa
usalama Kenya ambapo mamia wamepoteza maisha katika kipindi cha miaka
miwili iliyopita.
No comments:
Post a Comment