Saturday, October 31, 2015

UKAWA Watoa Tamko Zito Lenye Masharti Manne Tanzania Bara na Zanzibar

Viongozi wa vyama vinavyounda Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa), wamesema baada ya kufuatilia mwenendo wa Uchaguzi Mkuu wa Zanzibar wana taarifa za uhakika kwamba Maalim Seif Sharif Hamad, Mgombea Urais wa Chama cha Wananchi (Cuf) anayeungwa mkono na Umoja huo, ameshinda urais wa Zanzibar.

Taarifa iliyotolewa na viongozi hao jana kwa vyombo vya habari imetoa masharti  manne kufuatia kufutwa kwa uchaguzi wa Zanzibar.

Sharti la kwanza ni kuzitaka mamlaka zinazosimamia Uchaguzi Mkuu huo kuondoa mara moja tangazo la kuufuta Uchaguzi Mkuu wa Zanzibar.
 
Sharti la pili ni kumtangaza Seif kuwa ni mshindi halali wa nafasi ya urais na hivyo aapishwe kuwa Rais wa nchi ya Zanzibar ambayo ni sehemu ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

Sharti la tatu, wametoa  wito kwa Jumuiya ya Kimataifa kuingilia kati na kulaani kwa nguvu zote kinachofanyika Zanzibar ambako kwa mara nyingine tena demokrasia inataka kuminywa wazi wazi  ili tu kuinusuru CCM isiondoke madarakani kama ambavyo wapiga kura wamekuwa wakiamua. 
 
Aidha sharti la nne ni kwa wananchi wa Zanzibar, “tunapenda kuwahakikishia  kuwa tuko nao pamoja katika kipindi hiki kigumu cha kupigania mabadiliko .

Kura  za  Urais
Aidha  wamedai ushindi wa urais umetengenezwa, kwenye taarifa rasmi ya NEC ambayo imetangaza hadharani na kunukuliwa kwenye vyombo vya habari kwamba; wapiga kura walikuwa 15,589,639.
 
Katika uchaguzi huo kura zilizopigwa 15,193,862 na kati ya hizo zilizoharibika ni 402,248:”Kupitia hesabu hizo hapo juu unaweza kushuhudia upikwaji na utengenezwaji wa matokeo uliofanywa ili kuhujumu matokeo ya Lowassa kwa ajili ya kumbeba na kumpatia ushindi Dk. Magufuli ili kuinusuru CCM.”

Viongozi hao walisema Ili kuthibitisha kauli yao kwamba wameongoza uchaguzi katika nafasi hiyo kwa Lowassa ndiye Rais aliyechaguliwa na Watanzania walio wengi walioshiriki uchaguzi Mkuu Oktoba 25.
 
“Tunazitaka mamlaka zinazohusika, kwa mujibu wa katiba, sheria na taratibu za uchaguzi, zitengue matokeo batili waliyoyatangaza na zimtangaze mara moja Lowassa kuwa ni mshindi wa nafasi ya urais na Duni Juma Haji kuwa Makamu wa Rais,” walisema viongozi hao

Profesa Kitila "Mgombea wa urais wa Chadema, Edward Lowassa, hana budi kukubali matokeo licha ya kupoteza nafasi hiyo"

Dar es Salaam. Mhadhiri Mwandamizi wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), Profesa Kitila Mkumbo amesema aliyekuwa mgombea wa urais wa Chadema, Edward Lowassa, hana budi kukubali matokeo licha ya kupoteza nafasi hiyo.
Pia Profesa Mkumbo alisema mgombea huyo kisheria, hakuwa na haki ya kujitangaza mshindi wa nafasi ya urais katika uchaguzi wa mwaka huu.

Juzi, Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) ilitangaza matokeo ya kura za urais zilipopingwa Jumapili, Oktoba 25 mwaka huu na kumtangaza mgombea wa urais kwa tiketi ya CCM, Dk John Magufuli mshindi, lakini Lowassa siku hiyo pia alisema ameshinda katika uchaguzi kwa kura 10,268,795 sawa na asilimia 62 na kuitaka tume hiyo kumtangaza mshindi.

Profesa Mkumbo ambaye pia alipendekezwa na chama cha ACT- Wazalendo kugombea  nafasi hiyo na kukataa, alisema Lowassa aliingia kwenye kinyang’anyoro hicho akifahamu kuwa tume ndiyo yenye mamlaka ya kumtangaza mshindi.

Alisema licha ya mchuano mkali kati yake na mgombea wa CCM anatakiwa kukubali matokeo.

 “Hivyo Lowassa na  wenzake wa Ukawa hawana msingi wowote wa kisheria au kisiasa kutangaza ushindi wenyewe. Walikubali  kushiriki katika uchaguzi huu wakati wakifahamu kikamilifu kuwa NEC ndiyo yenye  jukumu la  kutangaza mshindi na mshindwa katika uchaguzi.”

Aliongeza: “Zaidi ya hayo, takwimu za uchaguzi zinaeleza pia.”

Hata hivyo alisema katika uchaguzi huu ambao ni wa kihistoria kutokana na upinzania mkali kati ya CCM na upinzani tofauti na miaka ya nyuma, bado upinzani umepoteza nafasi ya ubunge licha ya kujinyakulia viti 76 huku  CCM ikiwa na viti 188.

“Kupoteza viti hivyo ni ishara kwamba ushindi wa Lowassa haukuwa wa uhakika,”alisema Profesa Mkumbo na kuongeza;

“...nawashauri Ukawa kukubali kwamba Dk Magufuli ndiye rais mtaule wa awamu ya tano. Wahakikishe wanashirikiana  na kufanya kazi naye kazi kwa karibu katika kipindi chake cha miaka mitano ya uongozi. Kwa namna hiyo wataweza kuwa chachu ya kupata Katiba Mpya itakayowezesha kubadili mazingira ya kikatiba na kisheria katika uchaguzi ujao.”

Maalim Seif Shariff Hamad, kusema hatakubali kuporwa ushindi wake.

Mgombea urais wa Zanzibar kupitia Chama cha Wananchi (Cuf), Maalim Seif Sharif Hamad akitoa msimamo wa chama chake baada ya Tume ya Uchaguzi Zanzibar (Zec) kufuta matokeo ya uchaguzi.

Sakata la kufutwa kwa uchaguzi visiwani Zanzibar limechukua sura mpya baada ya mgombea urais kwa tiketi ya Chama cha Wananchi (CUF), Maalim Seif Shariff Hamad, kusema hatakubali kuporwa ushindi wake.

Mgombea huyo ambaye pia ni Makamu wa Kwanza wa Rais katika Serikali ya Umoja wa Kitaifa visiwani humo, pia ameitaka Tume ya Uchaguzi Zanzibar (ZEC) kuendelea na mchakato wa kuhesabu kura katika majimbo yaliyobaki ili kumtangaza mshindi.

Kadhalika, Maalim Seif ameonya kuwa kufikia kesho (Novemba Mosi, 2015), endapo Mwenyekiti wa ZEC, Jecha Salim Jecha, ataendelea na msimamo wake wa kuufuta uchaguzi huo na kupuuza maamuzi ya wananchi kupitia sanduku la kura, yeye na viongozi wenzake wa CUF watajiweka kando katika kuwazuia (wananchi) wasiendelee na hatua ya kudai haki yao ya kidemokrasia kwa njia za amani.

Chaguzi nne nimeibiwa matokeo. Kama Dk. Shein ameamua kung’ang’ania madaraka safari hii... sikubali, sikubali sikubali, alisema Maalim Seif ambaye pia ni Makamu wa Kwanza wa Rais katika Serikali ya Umoja wa Kitaifa iliyotarajiwa kumaliza muda wake baada ya rais mpya kupatikana kutokana na Uchaguzi Mkuu uliofanyika Jumapili iliyopita.

Akizungumza na waandishi wa habari kwenye Makao Makuu ya CUF, Mtendeni mjini Zanzibar jana, Maalim Seif alisema ifikapo Novemba Mosi (kesho Jumapili), wananchi wataanza kudai haki yao ya kidemokrasia kupinga uamuzi wa ZEC kufuta matokeo ya Uchaguzi Mkuu uliofanyika Jumapili.

Aliyasema hayo akiwa na mwenyekiti wake wa kampeni, Nassor Ahmed Mazrui, na pia msaidizi wake, waziri wa zamani wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar (SMZ), Mansoor Yussuf Himid.
Kwa mujibu wa Katiba ya Zanzibar ya mwaka 1984, kifungu cha 28(2), baada ya tarehe 2 Novemba 2015, Zanzibar haitakuwa na rais wala baraza la wawakilishi na haitakuwa na serikali wala mawaziri, makamu wa kwanza wala makamu wa pili wa rais wa Zanzibar, alisema.

Alisema kimsingi, Zanzibar itakuwa imeingia katika mgogoro mkubwa wa kikatiba na kisheria kutokana na uamuzi wa Mwenyekiti wa Zec, Salim Jecha, wa kufuta matokeo ya uchaguzi bila ya kuwashirikisha viongozi wenzake wa ZEC kinyume cha Katiba.

Alisema kwa mujibu wa katiba, ukomo wa uongozi wa Rais Dk. Ali Mohamed Shein na serikali yake ni Novemba 2, mwaka huu, na anatakiwa kuapishwa rais mpya pamoja na wajumbe wapya wa Baraza la Wawakilishi visiwani humo.

ASHANGAA VIFARU KUJAZWA ZANZIBAR

Alisema tangu kufutwa kwa matokeo, yeye amekuwa akichukua juhudi za kutafuta ufumbuzi kwa kukaribisha mazungumzo na viongozi wenzake wa kitaifa akiwamo Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Jakaya Kikwete na pia Rais wa Zanzibar, Dk. Shein, lakini wamekuwa wakimpiga chenga.
Alisema baada ya uchaguzi kufutwa, alianza kuwatafuta kwa kutumia mawasiliano ya simu na ujumbe kupitia wasaidizi wao, akitaka wakutane lakini hadi sasa ameshindwa kuwapata.
Tumeshatoa nafasi ya kutosha ya kutafuta ufumbuzi wa suala hili kwa njia za mazungumzo lakini viongozi wa CCM wanaonekana hawataki ufumbuzi,î alisema.

“Badala yake tunashuhudia Rais Kikwete akituletea majeshi na vifaru Zanzibar wakati wananchi wa Zanzibar wametulia wakitekeleza wito wetu wa kuwataka watunze amani ili kutupa nafasi viongozi wao kutafuta ufumbuzi, alisema Maalim Seif.
Maalim Seif alisema pamoja na yote, CUF inaendelea na juhudi za kufanya mazungumzo kwa kushirikiana na Jumuiya za Kimataifa ili kuhakikisha viongozi wa Zec wanarudi kazini kumalizia kazi ya kufanya uhakiki na majumuisho katika majimbo 14 yaliyobakia kati ya 54 na kumtangaza mshindi badala ya kuitisha uchaguzi mpya Zanzibar.

Iwapo hadi tarehe Mosi, Novemba 2015, hatutaona hatua zozote za maana zikichukuliwa kukamilisha uchaguzi huu na kuheshimu maamuzi ya Wazanzibari waliyoyafanya Oktoba 25, 2015, mimi na viongozi wenzangu wa CUF tutaondoa mikono yetu na kuwaachia wananchi wenyewe wa Zanzibar watafute haki yao kwa njia ya amani, alisema Maalim Seif aliyekuwa amefuatana pia na Waziri wa Katiba na Sheria wa Zanzibar, Abubakar Khamis Bakari.
Aidha, alisema CUF inaamini kuwa Watanzania wote na wapenda haki na amani na Jumuiya za Kimataifa, watawaunga mkono Wazanzibari katika kutafuta haki yao ya Kidemokrasia.

Alisema waangalizi wa ndani na wa kimataifa, wakiwamo Umoja wa Ulaya (EU), Jumuiya ya Madola Umoja wa Afrika (AU), Jumuiya ya Maendeleo ya Nchi za Kusini mwa Afrika (SADC), Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC), waangalizi wa Marekani na Uingereza, katika ripoti zao wamesema uchaguzi wa Zanzibar mwaka huu ulikuwa huru na wa haki.
Alisema Mwenyekiti wa ZEC (Jecha) amefanya kitendo cha ubabe kwa kufuta uchaguzi baada ya kuona mwelekeo mbaya wa matokeo ya uchaguzi huo kwa mgombea wa chama tawala -- Chama Cha Mapinduzi (CCM), Dk. Shein.

MSAIDIZI WA MWANASHERIA MKUU

Alipoulizwa kuhusiana na madai ya Maalim Seif kuwa baada ya Novemba 2 Zanzibar haitakuwa na rais, kwa mujibu wa Katiba ya Zanzibar ya mwaka 1984, kifungu cha 28(2) inayoeleza ukomo wa muda wa kuwa madarakani kwa rais na serikali yake, Msaidizi wa Mwanasheria Mkuu wa Zanzibar , Amisa Mmanga hakuwa tayari kutoa ufafanuzi kwa madai kuwa msemaji wa jambo hilo ni Mwanasheria Mkuu ambaye hivi sasa yuko safarini nje ya nchi.

Alisema kwa kuwa mkuu wake (Mwanasheria Mkuu) amesafiri nje ya nchi, hawezi kutoa ufafanuzi kwa jambo lolote kwani ni lazima kwanza apate baraka zake.

Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais, Mohamed Aboud, alipoulizwa kuhusiana na suala hilo, alisema bado ni mapema kwa serikali kutoa msimamo wake kuhusu kauli ya Maalim Seif , hasa ya kuamua kurejesha ajenda ya kufutwa matokeo kwa wananchi wa Zanzibar.

Sina cha kuzungumza serikali itatoa taarifa maalum wakati ukifika kwa kila jambo linalojitokeza sasa baada ya kufutwa kwa matokeo ya uchaguzi, alisema Waziri Aboud ambaye pia ndiye Msemaji Mkuu wa Serikali ya Umoja wa Kitaifa Zanzibar.
Matokeo ya Uchaguzi Mkuu wa Zanzibar yalifutwa na Mwenyekiti wa ZEC, Jecha, baada ya kutangazwa majimbo 31 kati ya 54 kwa madai kulikuwa na kasoro nyingi zinazoufanya usiwe huru na wa haki, ikiwamo kura kuongezeka katika baadhi ya majimbo kisiwani Pemba na pia baadhi ya makamishna wa ZEC kutanguliza itikadi za vyama hadi kuvua mashati ili kupigana.

Kadhalika, Mwenyekiti wa ZEC, alisema katika baadhi ya vituo, masanduku ya kupigia kura yaliporwa na kwenda kuhesabiwa nje ya vituo, kitendo ambacho ni kinyume cha sheria ya uchaguzi na pia, kuna taarifa ya kufukuzwa kwa baadhi ya mawakala wa wagombea na hivyo kushindwa kutekeleza wajibu wao.

Hata hivyo, kwa mujibu wa waangalizi wa kimataifa wakiwamo kutoka SADC, Jumuiya ya Afrika Mashariki, Jumuiya ya Madola, Umoja wa Afrika (AU) na Umoja wa Ulaya (EU), uchaguzi mkuu nchini kote ulifanyika kwa uhuru na haki na hivyo wakaitaka ZEC iendelee na mchakato wa kuhesabu kura na kumtangaza mshindi atokanaye na uamuzi wa Wazanzibari.

Kadhalika, Mwakilishi wa Umoja wa Mataifa (UN) nchini na pia balozi za mataifa mbalimbali zikiwamo za Uingereza, Ireland Kaskazini na Marekani, zimetoa taarifa ya kustushwa na uamuzi wa Mwenyekiti wa ZEC na kutaka tume hiyo iheshimu uamuzi wa Wazanzibar kwa kuendelea na mchakato wa kuhesabu kura, huku wanasiasa wote wakisisitizwa kutanguliza mbele taifa na kuhakikisha kuwa amani na utulivu vinaendelea kustawishwa visiwani humo.

CHANZO: NIPASHE