Thursday, March 10, 2016

Serikali kuunda Mamlaka Kuu ya Mapato ya Taifa

KADASerikali ipo kwenye mpango wa kuunda Mamlaka ya Mapato Kuu ya Taifa nje ya Mamlaka ya Mapato ya Tanzania (TRA) iliyopo kwa sasa ili kuondokana na malalamiko ya kero za kodi kwa wananchi wenye kipato cha chini.

Hayo yamesemwa leo Jijini  Dar es Salaam na Kaimu Kamishna wa Mamlaka ya Mapato Tanzania Alphayo Kidata alipokuwa  akifafanua kuhusu juhudi za Serikali katika kuwasaidia wananchi wa kipato cha chini kuweza kumudu kulipa kiwango cha kodi kinachowekwa na na Mamlaka hiyo.

“ Napenda kuwambia umma wa watanzania kwamba Serikali ya Awamu ya tano inawajali watu wake na ndio maana imeona kuwa kuna haja ya kuunda  Mamlaka moja ya utozaji wa kodi itakayojumuisha taasisi zote zinazohusika na kukusanya mapato nje ya kodi na ushuru ili kuondokana na malalamiko mengi ya wananchi juu ya utozaji wa kodi hasa katika Halmashauri zetu”Alisema Kidata.
KADA
Kamishna Kidata amesema kuwa katika dunia hii hakuna Serikali ambayo imechaguliwa na wananchi ikaamua tu kuwakandamiza wananchi wake katika jambo lolote lile hivyo basi kwa sasaserikali ipo  katika mchakato wa kuunda Mamlaka hiyo ambayo itasaidia kuweka viwango vya kodi ambavyo wananchi wa hali ya chini watamudu kulipa kutokana na biashara au kazi wanazozifanya.

Kamishna huyo ameongeza kuwa Mamlaka yake kwa kushirikiana na mamlaka nyingine zinazokusanya kodi katika Halmashauri nchini watahakikisha wanalipatia ufumbuzi suala la kero ya kodi kwa wananchi wa hali ya chini kwa kupata muafaka ambao utasaidia pande zote mbili bila kukandamiza upande wowote iwe Serikali ama mwananchi wa kawaida.

Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) imekuwa na rekodi nzuri ya ukusanyaji wa kodi ila kumekuwa na malalamiko mengi kutoka kwa wananchi kuhusu kodi ambazo zimekuwa kero na hazina tija. Hivyo Serikali imejipanga kuiongezea nguvu Mamlaka hiyo kwa kuipa uwezo wa kukusanya na mapato ambayo  hayatokani na kodi toka katika wizara, mashirika,tasisi za serikalina Halmashauri zote nchini.

WAZIRI MKUU: TANZANIA YAPIGA ​HATUA KIUCHUMI

TIH4WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amesema mabadiliko ya kiuchumi yaliyofanyika nchini yameifanya Tanzania ipige hatua kubwa katika kipindi cha miaka 10 iliyopita.

“Kumekuwa na mabadiliko chanya kwenye ukuaji halisi wa Pato la Taifa, kushuka kwa mfumuko wa bei, na akiba ya kutosha ya fedha za kigeni. Pato la Taifa limekua kwa wastani wa asilimia 7 na mfumuko wa bei umeshuka hadi kufikia asilimia 5.3 mnamo Juni 2015 ikilinganishwa na asilimia 16 na asilimia 8 ilivyokuwa mwishoni mwa mwaka 2012 na mwanzoni wa mwaka 2013,” alisema.

Ametoa kauli hiyo leo jioni (Jumatano, Machi 9, 2016) wakati akihutubia kongamano la biashara baina ya Tanzania na Vietnam lililofanyika kwenye ukumbi wa Mikutano wa Mwalimu Nyerere jijini Dar es Salaam na kuhudhuriwa na Rais wa Jamhuri ya Kisoshalisti ya Vietnam, Bw. Troung Tan Sang.

Akizungumza kwa niaba ya Rais, Dk. John Pombe Magufuli, Waziri Mkuu alisema mbali ya mabadiliko ya kiuchumi, Tanzania pia imefanya mabadiliko kwenye sheria, mifumo ya kifedha na sekta za kuhudumia jamii za umma.

“Katika kipindi cha muongo mmoja uliopita tumefanya mabadiliko ya kisera na kwenye sheria zetu ili kuboresha hali ya uwekezaji, kukuza uchumi na kuboresha maisha ya wananchi,” alisema.
TIH4
Alitoa mwaliko kwa wafanyabiashara walioambatana na Rais wa nchi hiyo kwa kuwaeleza kwamba faida kubwa ya kuwekeza nchini Tanzania ni uwepo wa soko la uhakika kwa wakazi zaidi ya milioni 300 waishio Mashariki na Kusini mwa bara la Afrika.

“Tanzania ni mwanachama wa Jumuiya za Kikanda katika SADC na EAC. Uwepo wake katika taasisi hizi ni fursa tosha. Pia Tanzania ni lango kwa nchi sita ambazo hazipakani na bahari. Inasaidia kufanyika biashara katika nchi za Congo (DRC), Rwanda, Burundi, Zambia, Malawi na Uganda,” alisema.

Akizungumzia kuhusu fursa zilizopo kwenye sekta ya kilimo, Waziri Mkuu aliwakaribisha wafanyabiashara hao wawekeze kwenye kilimo cha biashara na viwanda vya usindikaji ili waweze kusaidia kuongeza uzalishaji wa chakula nchini.

“Tuwakaribisha kuwekeza kwenye viwanda vya usindikaji ili kuongeza thamani za mazao yanayozalishwa nchini, kujenga viwanda vidogo vya kutengeneza vifungashio kwa ajili ya masoko ya ndani na nje ya nchi. Pia mnaweza kuwekeza kwenye utengenezaji wa zana za kilimo ambazo ni za bei nafuu kwa wananchi wetu,” alisema.

Ayatullah Makarem Shirazi: Viongozi wa Kiarabu hawawezi kuficha mafanikio ya kujivunia ya Hizbullah

Ayatullah Makarem Shirazi: Viongozi wa Kiarabu hawawezi kuficha mafanikio ya kujivunia ya HizbullahAyatullah Naser Makarem Shirazi mmoja wa Marajii Taqlidi wa nchini Iran amesema kuwa, viongozi wa Kiarabu katu hawawezi kuficha mafanikio ya kujivunia ya Harakati ya Muqawama wa Kiislamu ya Hizbullah ya Lebanon.

Kiongozi huyo wa kidini mwenye makao yake mjini Qum hapa Iran amebainisha kwamba, hatua ya viongozi wa Kiarabu ya kupasisha maazimio ya aibu dhidi ya Hizbullah katu haiwezi kuficha mafanikio ya kujivunia ya harakati hiyo ya mapambano, kwani Hizbullah itaendelea kubakia kuwa ni shujaa na bingwa.

Ayatullah Makarim Shirazi ameongeza kwamba, historia ya Waarabu imeshuhudia mara chache sana ushujaa na ujasiri kama wa Hizbullah ya Lebanon kwani harakati hiyo imeweza kuushinda utawala ghasibu wa Israel uliokuwa haushindwi.

Ikumbukwe kuwa, Jumatano iliyopita Baraza la Ushirikiano la Ghuba ya Uajemi liliiweka harakati ya Hizbullah ya Lebanon katika orodha ya makundi ya kigaidi na kutangaza kuwa, limechukua hatua kadhaa katika uwanja huo. Hatua ya baraza hilo linaloundwa na nchi za Saudi Arabia, Qatar, Kuwait, Oman, Umoja wa Falme za Kiarabu na Bahrain imekabiliwa na upinzani mkubwa ndani na nje ya Lebanon. 

Asasi na harakati mbalimbali za kieneo na kimataifa zimelaani vikali hatua hiyo ya Baraza la Ushirikiano la Ghuba ya Uajemi.Chanzo irib