WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa
amesema mabadiliko ya kiuchumi yaliyofanyika nchini yameifanya Tanzania
ipige hatua kubwa katika kipindi cha miaka 10 iliyopita.
“Kumekuwa na mabadiliko chanya
kwenye ukuaji halisi wa Pato la Taifa, kushuka kwa mfumuko wa bei, na
akiba ya kutosha ya fedha za kigeni. Pato la Taifa limekua kwa wastani
wa asilimia 7 na mfumuko wa bei umeshuka hadi kufikia asilimia 5.3 mnamo
Juni 2015 ikilinganishwa na asilimia 16 na asilimia 8 ilivyokuwa
mwishoni mwa mwaka 2012 na mwanzoni wa mwaka 2013,” alisema.
Ametoa kauli hiyo leo jioni
(Jumatano, Machi 9, 2016) wakati akihutubia kongamano la biashara baina
ya Tanzania na Vietnam lililofanyika kwenye ukumbi wa Mikutano wa
Mwalimu Nyerere jijini Dar es Salaam na kuhudhuriwa na Rais wa Jamhuri
ya Kisoshalisti ya Vietnam, Bw. Troung Tan Sang.
Akizungumza kwa niaba ya Rais,
Dk. John Pombe Magufuli, Waziri Mkuu alisema mbali ya mabadiliko ya
kiuchumi, Tanzania pia imefanya mabadiliko kwenye sheria, mifumo ya
kifedha na sekta za kuhudumia jamii za umma.
“Katika kipindi cha muongo mmoja
uliopita tumefanya mabadiliko ya kisera na kwenye sheria zetu ili
kuboresha hali ya uwekezaji, kukuza uchumi na kuboresha maisha ya
wananchi,” alisema.
Alitoa mwaliko kwa
wafanyabiashara walioambatana na Rais wa nchi hiyo kwa kuwaeleza kwamba
faida kubwa ya kuwekeza nchini Tanzania ni uwepo wa soko la uhakika kwa
wakazi zaidi ya milioni 300 waishio Mashariki na Kusini mwa bara la
Afrika.
“Tanzania ni mwanachama wa
Jumuiya za Kikanda katika SADC na EAC. Uwepo wake katika taasisi hizi ni
fursa tosha. Pia Tanzania ni lango kwa nchi sita ambazo hazipakani na
bahari. Inasaidia kufanyika biashara katika nchi za Congo (DRC), Rwanda,
Burundi, Zambia, Malawi na Uganda,” alisema.
Akizungumzia kuhusu fursa
zilizopo kwenye sekta ya kilimo, Waziri Mkuu aliwakaribisha
wafanyabiashara hao wawekeze kwenye kilimo cha biashara na viwanda vya
usindikaji ili waweze kusaidia kuongeza uzalishaji wa chakula nchini.
“Tuwakaribisha kuwekeza kwenye
viwanda vya usindikaji ili kuongeza thamani za mazao yanayozalishwa
nchini, kujenga viwanda vidogo vya kutengeneza vifungashio kwa ajili ya
masoko ya ndani na nje ya nchi. Pia mnaweza kuwekeza kwenye utengenezaji
wa zana za kilimo ambazo ni za bei nafuu kwa wananchi wetu,” alisema.
No comments:
Post a Comment