Wednesday, December 23, 2015

Waislamu wawatea wenzao wa Nigeria mbele ya UN

Waislamu wa Marekani jana walikusanyika mbele ya ofisi za Nigeria katika Umoja wa Mataifa mjini New York wakitaka kuachiwa huru kiongozi wa Waislamu wa madhehebu ya Shia nchini Nigeria, Sheikh Ibrahim Zakzaky anayeshikiliwa na vyombo vya usalama.

Walioshiriki katika mjumuiko huo wametoa nara na kaulimbiu za kulaani mauaji yaliyofanywa na jeshi la Nigeria dhidi ya Waislamu nchini humo. Sayyid Iliya mwanachama wa Congresi ya Waislamu wa Marekani ambaye amehutubia mjumuiko huo amesema kuwa, Sheikh Ibrahim Zakzaky ni miongoni mwa viongozi wakubwa wa kidini barani Afrika na kwamba shughuli zake haziwahusu Waislamu wa madhehebu ya Shia pekee bali hata Waislamu wa Suni na jamii za Wakristo.

Mwanaharakati wa Kiislamu wa Marekani, Ali Naqavi ambaye pia amehutubia mjumuiko huo mjini New York amesema kuwa, Sheikh Ibrahim Zakzaky na wenzake wanaoshikiliwa na jeshi la Nigeria wanapaswa kuachiwa huru bila ya masharti yoyote.

Mamia ya Waislamu wa madhehebu ya Shia wameuawa shahidi katika mashambulizi yaliyofanywa siku kadhaa zilizopita dhidi ya kituo cha kidini cha Baqiyatullah katika mji wa Zaria nchini Nigeria. Kiongozi wa Waislamu hao, Sheikh Ibrahim Zakzaky pia ametiwa nguvuni na jeshi baada ya kujeruhiwa kwa risasi na kupelekwa kusikojulikana.

No comments: