Friday, January 8, 2016

KULAANI TUKIO LA SERIKALI YA SAUDIA ARABIA KUMNYONGA SHEIKH NIMR BAQIR NA WENZAKE



Jinai za ukoo wa Aal Saud za kumnyonga Sheikh Nimr Baqir al-Nimr, kiongozi wa Waislamu wa Kishia nchini Saudia zimekabiliwa na radiamali kali katika eneo hili na ulimwengu mzima kwa ujumla.

Mmoja wa Viongozi wakuu wa Kiroho wa Waislam, Dhehebu la Shia Ithnasheriya Tanzania ambae pia ni Kiongozi Mkuu wa Chuo cha Kiislam (Hawzat) Imam Swadiq, kilichopo Kigogo Post, Dar es salaam, Sheikh Hemed Jalala amelaani kitendo cha kunyongwa kwa kiongozi wa Waislamu wa Kishia nchini Saudia,Sheikh Nimr Baqir na kukiona kitendo hicho hakiendani na haki za Binadamu ambapo kila mmoja ana hakai ya kuishi.

Sheikh Nimr Baqir Al-Nimr aliyekuwa na umri wa miaka 56, alikuwa mkosoaji mkubwa wa utawala wa ukoo wa Aal Saud na shakhsia mkuu wa harakati ya vuguvugu la upinzani la mwaka 2011 katika eneo la mashariki mwa Saudia ambalo wakaazi wake ni wa jamii ya wachache ya Waislamu wa Kishia wa nchi hiyo.

 Jamii ya Waislamu hao ambao wanaishi katika mkoa wa Ash-Sharqiyyah wenye utajiri mkubwa wa mafuta wanalalamikia kutengwa na kunyongeshwa; na katika muda wote huu Sheikh Nimr amekuwa ndiye sauti kuu ya kupigania haki za wananchi wa eneo hilo dhidi ya utawala wa kidikteta wa Aal Saud

Juzi asubuhi Januari 2,2016, Wizara ya Mambo ya Ndani ya Saudia ilitoa taarifa rasmi na 
kutangaza kuwa Sheikh Nimr Baqir Al-Nimr, ulama na mwanaharakati mashuhuri wa kisiasa nchini humo pamoja na watu wengine 46 wamenyongwa kwa sababu ya kuhusika na vitendo vya kuhatarisha 

usalama wa nchi.Baada ya kupita masaa machache tu tangu kutangazwa habari ya kunyongwa Sheikh Nimr, asasi, shakhsia na makundi mbalimbali katika pembe tofauti za dunia walilaani hatua hiyo ya jinai na kusisitiza kwamba kuendelea siasa za ukandamizaji nchini Saudia kutashadidisha malalamiko na upinzani dhidi ya utawala wa Aal Saud na kuudhoofisha utawala huo.

Philip Luther, Mkurugenzi wa Shirika la kutetea haki za binadamu la Amnesty International katika Mashariki ya Kati na Afrika ya Kaskazini, yeye amesema viongozi wa Saudia wanasema wametekeleza hukumu hizo za kifo kwa ajili ya kulinda usalama, lakini kunyongwa kwa Sheikh Nimr kunajenga hisia kwamba utawala wa Aal Saud unalitumia suala hilo kutekeleza visasi vya kisiasa kwa kisingizio cha kupambana na ugaidi.

Mbali na kueleza kwamba kesi ya Shekih Nimr haikuendeshwa kwa uadilifu, Luther ameongeza kuwa lengo la unyongaji mkubwa wa wanaharakati wa kisiasa na kidini nchini Saudia ni kutaka kuzima sauti za ukosoaji dhidi ya utawala wa Aal Saud hususan unaofanywa na Waislamu wa Kishia.
 
Wizara za Mambo ya Nje za Ujerumani, Uingereza na Marekani nazo pia zimetoa taarifa tofauti, ambapo mbali na kueleza wasiwasi zilionao kutokana na kunyongwa Sheikh Nimr zimeitaka serikali ya Saudia iheshimu haki za binadamu na kuruhusu utoaji maoni wa wapinzani unaofanywa kwa njia za amani.

Pia amekosoa vikali kimya cha wale wanaodai kuwa eti ni wapigania uhuru, demokrasia na haki za binaadamu amelaani pia uungaji mkono wao kwa utawala wa ukoo wa Aal Saud ambao umemwaga damu ya mtu asiye na hatia kwa sababu tu ya kukosoa na kulalamikia ukiukaji wa sheria unaofanywa na utawala huo, na kusisitiza kuwa ulimwengu wa Kiislamu na dunia kwa ujumla lazima uhisi wajibu wa kutekeleza ipasavyo majukumu yake. 

mwanachuoni huyo madhlumu, hakuwaita watu kwenye harakati yakubeba silaha wala kuwaita watu kwenye harakati ya siri na kufanya njama, bali alisimama na kujishughulisha na ukosoaji kwa namna ya wazi na kuamrisha mema na kukataza maovu kutokana na ghera ya kidini.

Aidha, watu ambao kwa dhati wanaguswa na kufuatilia haki za binaadamu na pia wanalingania 
uadilifu duniani, wanapaswa kufuatilia kadhia hiyo, kama ambavyo pia hawatakiwi kufanya mambo yao kiupendeleo.

jinai hiyo kwa mtazamo fulani inaweza kuwa sababu ya mwendelezo wa mradi wa kuimarisha satwa ya Saudia katika eneo na kuwazuia wapinzani na wakosoaji wake wa ndani na kieneo kwa kutumia siasa za ukandamizaji na za mabavu.

Si vibaya kuashiria hapa kwamba, tangu alipoaga duania mfalme Abdullah bin Abdulaziz Aal Saud na kuchukua madaraka hayo Salman bin Abdulaziz Aal Saud, Saudia imekuwa ikishuhudia mabadiliko ya kisiasa na wakati huo huo vita vya kuwania madaraka ndani ya ukoo wa kifalme wa Aal Saud. 

Wasi wasi inayotokana na madai ya kiraia na malalamiko yanayoongezeka kila uchao kuhusiana na ubaguzi na ukanyagaji wa wazi wa haki za raia na kadhalika kukosekana utawala wa kidemokrasia, ni mambo yaliyowafanya watawala wa Saudi Arabia kufuata zaidi siasa za ukandamizaji na za mtutu wa bunduki katika kujaribu kuzima wimbi hilo la malalamiko ya wananchi. 
 
Pamoja na hayo hali ya mambo nchini humo imezidi kuwa mbaya kiasi cha kuufanya utawala wa kifalme wa nchi hiyo kushindwa kuwadhibiti wapinzani na kurejesha hali ya mambo kama ilivyokuwa awali. Hata hivyo badala yake utawala wa Aal-Saud umeamua kufuata mkondo wa kutoa madai yasiyo na mashiko hasa ya kiusalama na kigaidi au kuzituhumu nchi nyingine kwa kuingilia masuala yake ya ndani.

Ukweli ni kwamba, Saudi Arabia imetekeleza siasa hizo nchini Bahrain na Yemen katika hali 
ambayo, hatua hiyo ya Riyadh inaitia hasara kubwa serikali ya nchi hiyo. Kosa la kwanza ni uingiliaji wake wa kijeshi nchini Bahrain na Yemen na kufanya mauaji makubwa, suala ambalo limekabiliwa na ukosoaji mkubwa wa walimwengu, na hakuna shaka kwamba Saudia inapaswa kutoa majibu kwa jinai zake hizo.

Kosa la pili ni kwamba Saudia ni muhusika mkuu wa kueneza fikra za Kiwahabi na Kisalafi 
duniani, sanjari na kuunda kundi la kigaidi na kitakfiri la Daesh, mienendo ambayo Riyadh 
haiwezi kuipinga.Ama kosa lingine la Saudia ni kuwapuuza wapinzani na wakosoaji wake wa ndani, ambapo inadhania kwamba kwa kutumia siasa za ukandamizaji, itaweza kuzima sauti yao. Kwa hakika kitendo cha 

Saudia kuchochea moto wa migogoro ya kikaumu na kimadhehebu, ni jambo hatari ambalo Riyadh imejichimbia kaburi. Kwa ajili hiyo viongozi wa Saudia wanatakiwa kujiandaa kukabiliana na hatima mbaya inayotokana na siasa zao ghalati walizojiandalia wenyewe. Kama ambavyo Kiongozi Muadhamu alivyosema kuwa, 
 
bila shaka kitendo cha kumwaga damu bila ya haki ya shahid madhlumu Sheikh Nimr Baqir al-Nimri, kitakuwa na athari ya radiamali ya haraka kwa watawala wa Aal Saud.Kwa mnasaba huo mijumuiko na maandamano makubwa yamefanyika katika maeneo mbalimbali nchini Iran, Saudia, Iraq, Pakistan, Lebanon, Bahrain, Uingereza na katika miji mingine ya nchi kadhaa 
za Ulaya, ambapo waandamanaji wametoa sha'ar za kuupinga utawala wa Aal Saud na kuzitaka 
jumuiya za kimataifa zifuatilie jinai za utawala huo dhidi ya raia wa nchi hiyo.
  
Imetolewa na Mmoja wa Viongozi Wakuu wa Kiroho wa Waislam, Dhehebu la Shia Ithnasheriya Tanzania ambae pia ni Kiongozi Mkuu wa Chuo cha Kiislam (Hawzat) Imam Swadiq,Sheikh Hemed Jalala  kilichopo Kigogo Post, Dar es Salaam. 

0654-851747 Au 0765-851747.

No comments: