Rais wa Zimbabwe Robert Mugabe amewatahadharisha
mashujaa wa vita vya uhuru ambao wameonya kuwa huenda wakakataa kuunga
mkono serikali yake kufuatia mporomoko mkubwa zaidi wa uchumi kuwahi
kushuhudiwa nchini humo.
Rais Mugabe amewaonya maveterani
wa vita wanaomkosoa akieleza kwamba, watakabiliwa na adhabu kali endapo
hawataachana na msimamo wao huo.
Mashujaa hao wanaonya kuwa watakataa
kumuunga mkono Mugabe endapo hataweka mikakati ya kukomesha ubadhirifu
wa mali ya umma na ufisadi uliokithiri nchini humo na kusababisha
maandamano makubwa zaidi.
Rais Mugabe amewaonya mashujaa hao alipokuwa akihutubia umati wa wafuasi wa chama tawala cha Zanu-PF.
Aidha rais huyo amewataka viongozi wa chama cha mashujaa kuwachagua viongozi wapya.
Mugabe amesema kuwa, viongozi wa
mashujaa hao wa vita vya ukombozi kutoka mikononi mwa wakoloni kuwa
walikuwa wameshawishiwa na mataifa ya Magharibi.
Mugabe ameonya kuwa wale ambao wanaendeleza maandamano
yaliyoshuhudiwa katika siku za hivi karibuni huenda wakafungwa jela
kwani taifa hilo halina haja ya mapigano ya wenyewe kwa wenyewe.
Hivi karibuni maveterani wenza wa Rais
Robert Mugabe wa Zimbabwe ambao wamekuwa waungaji mkono wake wakubwa,
kwa mara ya kwanza kabisa walimtuhumu kiongozi huyo kuwa ni dekteta,
matamshi ambayo yalitathminiwa na weledi wa mambo kama yataimarisha
harakazi za upinzani dhidi ya Mugabe mwenye umri wa miaka 92.