Sunday, July 24, 2016

Rezaei: Saudia inaendelea kutuma magaidi nchini Iran

Katibu wa Halmashauri ya Kuainisha Maslahi ya Mfumo wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran ameikosoa vikali Saudi Arabia kwa kuendelea kuyaunga mkono makundi ya kigaidi na kuyatuma hapa nchini kutekeleza mashambulizi.

Mohsen Rezaei, Katibu wa Halmashauri ya Kuainisha Maslahi ya Mfumo wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran amesema kuwa, ubalozi mdogo wa Saudia kaskazini mwa Iraq umekuwa ukitoa misaada na uungaji mkono kwa makundi ya kigaidi kama vile Komala Party ili yatekeleze mashambulizi ya kigaidi hapa Iran na Iraq.

 Amesema utawala wa Riyadh umekuwa ukiliunga mkono kundi la kigaidi la Komala ambalo limekuwa likitekeleza mashambulizi ya kigaidi magharibi mwa Iran na kuongeza kuwa, kama vyombo vya usalama vya Jamhuri ya Kiislamu havingekuwa macho, kundi hilo lingekuwa limetekeleza mashambulizi makubwa ya mabomu katika kila kona ya nchi.

Ban Ki-moon, Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa

Mapema mwezi huu akitoa radiamali yake kwa matamshi ya Ban Ki-moon, Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa kuhusiana na majaribio ya makombora ya Iran, Rezaei alisema makombora na mabomu ya utawala haramu wa Israel na Saudi Arabia ndiyo yanayohatarisha usalama na amani ya Mashariki ya Kati. 

Ban Ki-moon alidai katika ripoti yake iliyodaiwa kuwa ni ya siri kwamba, majaribio ya makombora ya balastiki ya Iran yanakinzana na moyo wa makubaliano ya nyuklia yaliyofikiwa kati ya taifa hili na madola sita makubwa duniani.Chanzo:parstoday

Uganda: Hatubabaishwi na matamshi ya vitisho ya Marekani

Katika kile kinaachoonekana ni kuzidi kuingia doa uhusiano wa Uganda na Marekani, Waziri wa Teknolojia ya Habari na Mawasiliano wa nchi hiyo ya Afrika Mashariki amesema serikali ya Kampala haibabaishwi na matamshi ya vitisho yaliyotolewa hivi karibuni na Washington.

Frank Tumwebaze, Waziri wa Teknolojia ya Habari na Mawasiliano wa Uganda amekosoa kauli ya hivi karibuni ya Rais Barack Obama wa Marekani kwamba Washington yumkini ikakata uhusiano wa kibiashara na Kampala iwapo serikali ya Rais Yoweri Kaguta Museveni itaendelea kuwakamata na kuwazuilia wakosoaji wake wakiwemo viongozi wa upinzani, 

wanaharakati na waandishi wa habari. Tumwebaze amesema miamala ya kibiashara ya Uganda na nchi nyingine yeyote ile ikiwemo Marekani, imejengeka juu ya misingi ya kuheshimiana na kwa faida ya pande zote na wala sio kutokana na namna nchi hizo zinavyoitazama Uganda.
Rais Yoweri Museveni wa Uganda akihutubia hadhara

Waziri wa Teknolojia ya Habari na Mawasiliano wa Uganda ameongeza kuwa, Uganda huko nyuma ilikosoa na sasa pia inakosoa tena matamshi ya aina hiyo ya Marekani ya kujaribu kuisawiri serikali ya Kampala kuwa ni mkiukaji wa misingi ya demokrasia na mkanyagaji wa haki za binadamu.
Rais Barack Obama wa Marekani

Hivi karibuni, Obama alisema kuwa, Uganda iko katika hatari ya kutimuliwa kwenye mpango wa msaada wa kiuchumi wa Marekani unaojulikana kwa jina la African Growth and Opportunity Act (AGOA), iwapo itaendelea kuwakamata na kuwazuilia wakosoaji wa serikali ya Rais Museveni.Chanzo:parstoday