Katika kile kinaachoonekana ni kuzidi kuingia
doa uhusiano wa Uganda na Marekani, Waziri wa Teknolojia ya Habari na
Mawasiliano wa nchi hiyo ya Afrika Mashariki amesema serikali ya Kampala
haibabaishwi na matamshi ya vitisho yaliyotolewa hivi karibuni na
Washington.
Frank Tumwebaze, Waziri wa Teknolojia ya Habari na
Mawasiliano wa Uganda amekosoa kauli ya hivi karibuni ya Rais Barack
Obama wa Marekani kwamba Washington yumkini ikakata uhusiano wa
kibiashara na Kampala iwapo serikali ya Rais Yoweri Kaguta Museveni
itaendelea kuwakamata na kuwazuilia wakosoaji wake wakiwemo viongozi wa
upinzani,
wanaharakati na waandishi wa habari. Tumwebaze amesema miamala
ya kibiashara ya Uganda na nchi nyingine yeyote ile ikiwemo Marekani,
imejengeka juu ya misingi ya kuheshimiana na kwa faida ya pande zote na
wala sio kutokana na namna nchi hizo zinavyoitazama Uganda.
Waziri wa Teknolojia ya Habari na Mawasiliano wa Uganda
ameongeza kuwa, Uganda huko nyuma ilikosoa na sasa pia inakosoa tena
matamshi ya aina hiyo ya Marekani ya kujaribu kuisawiri serikali ya
Kampala kuwa ni mkiukaji wa misingi ya demokrasia na mkanyagaji wa haki
za binadamu.
Hivi karibuni, Obama alisema kuwa, Uganda iko katika hatari
ya kutimuliwa kwenye mpango wa msaada wa kiuchumi wa Marekani
unaojulikana kwa jina la African Growth and Opportunity Act (AGOA),
iwapo itaendelea kuwakamata na kuwazuilia wakosoaji wa serikali ya Rais
Museveni.Chanzo:parstoday
No comments:
Post a Comment