Waislamu wa Marekani jana walikusanyika mbele ya ofisi za Nigeria
katika Umoja wa Mataifa mjini New York wakitaka kuachiwa huru kiongozi
wa Waislamu wa madhehebu ya Shia nchini Nigeria, Sheikh Ibrahim Zakzaky
anayeshikiliwa na vyombo vya usalama.
Walioshiriki katika mjumuiko huo wametoa nara na kaulimbiu za kulaani
mauaji yaliyofanywa na jeshi la Nigeria dhidi ya Waislamu nchini humo.
Sayyid Iliya mwanachama wa Congresi ya Waislamu wa Marekani ambaye
amehutubia mjumuiko huo amesema kuwa, Sheikh Ibrahim Zakzaky ni miongoni
mwa viongozi wakubwa wa kidini barani Afrika na kwamba shughuli zake
haziwahusu Waislamu wa madhehebu ya Shia pekee bali hata Waislamu wa
Suni na jamii za Wakristo.
Mwanaharakati wa Kiislamu wa Marekani, Ali Naqavi ambaye pia
amehutubia mjumuiko huo mjini New York amesema kuwa, Sheikh Ibrahim
Zakzaky na wenzake wanaoshikiliwa na jeshi la Nigeria wanapaswa kuachiwa
huru bila ya masharti yoyote.
Mamia ya Waislamu wa madhehebu ya Shia wameuawa shahidi katika
mashambulizi yaliyofanywa siku kadhaa zilizopita dhidi ya kituo cha
kidini cha Baqiyatullah katika mji wa Zaria nchini Nigeria. Kiongozi wa
Waislamu hao, Sheikh Ibrahim Zakzaky pia ametiwa nguvuni na jeshi baada
ya kujeruhiwa kwa risasi na kupelekwa kusikojulikana.