Tuesday, October 13, 2015

Ujerumani yataka kuzipatanisha Iran na Saudia

Waziri wa Mashauri ya Kigeni wa Ujerumani Frank-Walter Steinmeier anatazamiwa kutumia ziara yake katika nchi za Saudi Arabia na Jamhuri ya Kiislamu ya Iran mwishoni mwa juma hili, kujaribu kuzipatanisha Riyadh na Tehran.
Steinmeier amesema nchi mbili hizo zina umuhimu mkubwa katika eneo la Mashariki ya Kati, na huenda kupatana kwao kukaupatia ufumbuzi wa kudumu mgogoro wa kisiasa unaoshuhudiwa nchini Syria.
Waziri wa Mashauri ya Kigeni wa Ujerumani anatazamiwa kuzuru Iran na Saudia mwishoni mwa juma hili.
Mgogoro wa Syria uliibuka tangu mwaka 2011, wakati makundi ya kigaidi yanayopata uungaji mkono wa silaha na fedha kutoka nchi za Magharibi, utawala wa Kizayuni wa Israel na baadhi ya nchi za Kiarabu, yalipoanzisha mashambulizi na hujuma za kila aina kwa lengo la kuiondoa madarakani serikali halali ya nchi hiyo, ya Rais Bashar al-Assad, njama ambazo hadi leo zimeambulia patupu.chanzo irib

Rais Kikwete azindua mradi wa Umeme Gesi Asilia Kinyerezi

Rais Dkt.Jakaya Mrisho Kikwete akikata utepe na kufunua kitambaa katika jiwe la msingi kuzindua rasmi mtambo wa kufua umeme kutokana na Gesi Asilia huko Kinyerezi jijini Dar es Salaam.Mradi huo umejengwa kwa gharama ya shilingi bilioni 400.Kushoto ni mwakilishi wa benki ya African Development Bank(ADB) Bi Tonia Kandiero na kulia ni Mkurugenzi Mkuu wa TANESCO Bwana Felchesmi Mramba.


Rais Dkt.Jakaya Mrisho Kikwete akitembelea mradi wa kufua umeme kutokana na gesi asilia muda mfupi baada ya kuzindua mradi huo huko Kinyerezi jijini Dar es Salaam Oktoba 13, 2015.


LHRC watoa mafunzo kwa wagombea Ubunge na Udiwani kwa Wanawake Nchini



Mgombea ubunge wa ubungo kwa tiketi ya chama cha TLP Mama GODLIVA MANUMBA na kulia kwake ni  mgombea ubunge wa jimbo la ubungo kwa tiketi ya ACT-wazalendo Mama NYANJURA NYARINDO wakizngumza na wanahabari wakati wa mafunzo hayo ambayo yamefanyika kwa siku mbili Jijini Dar es salaam.
 
 Wagombea wa nafasi za udiwani na ubunge ambao ni wanawake katika uchaguzi mkuu wameomba vyombo vya habari pamoja na wadau wa uchaguzi nchini kuwapa kipaumbele katika nyakati hizi za kampeni kutokana na kile walichodai kusahaulika na kipaumbele kikubwa kupewa wagombea wanaume katika uchaguzi wa mwaka huu.
 Wito huu umetolewa leo jijini Dar es salaam wakati wa mafunzo kwa wagombea wa nafasi hizo wanawake nchini Tanzania mafunzo ambayo yameandaliwa na kituo cha sheria na haki za binadamu nchini LHRC kwa udhamini wa shirika la kimataifa la wanawake la UN-WOMEN,mafunzo ambayo yamefanyika kwa siku mbili Jijini Dra es salaam.
Wakizungumza na wanahabari wakati wakitoa tamko lao juu ya mwenendo wa uchaguzi huo mgombea ubunge wa jimbo la ubungo kwa tiketi ya ACT-wazalendo Mama NYANJURA NYARINDO pamoja na mgombea ubunge wa ubungo kwa tiketi ya chama cha TLP Mama GODLIVA MANUMBA wamesema kuwa katika hatua hii ya kampeni wanawake wamekuwa wakiwekwa nyuma sana na vyombo vya habari pamoja na wadau wa uchaguzi jambo ambalo wamesema linazidi kuwarudisha nyumba katika harakati zao za uchaguzi huo.
 
Aidha wamesema kuwa changamoto nyingine ambayo inawarudisha nyuma wagombea wanawake katika uchaguzi wa mwaka huu ni changamoto ya rasilimali ambayo imekuwa ikiwafanya kushindwa kuendesha shughuli zao za kampeni huku wakiwaomba wadau kuhakikisha wanawasaidia ili waweze kufanikisha ndoto zao katika uchaguzi huu.

Nao waandaaji wa Mafunzo hayo ambayo ni LHRC kupitia Afisa Program wa dawati la jinsia na watoto NAEMY SILAYO amesema kuwa lengo kuu la kuandaa mafunzo hayo ni kuwajengea uwezo wagombea wanawake wa udiwani na ubunge katika maeneo mbalimbali nchini Tanzania ili waweze kupambana na kasi ya uchaguzi iliyopo sasa nchini.
 Afisa Program wa dawati la jinsia na watoto kutoka kituo cha sheria na haki za Binadamu LHRC ,NAEMY SILAYO akizngumza na wanahabari juu ya mafunzo hayo na malengo yao kwa wagombea hao. Amesema moja kati ya malengo ya mafunzo hayo.
 
Pia ni kuhakikisha kuwa wanawatoa wanawake hao katika fikra za kuamini kuwa wanaweke hawawezi na kuwarudisha katika fikra za kuamini kuwa wanawake wanaweza kama wakiwa na nia na kujituma pamoja na kuwapa mbinu mbalimbali ambazo wanaweza kuzitumia katika uchaguzi huo ili waweze kushinda nafasi ambazo wanawania.
Aidha NAEMY amevitaka vyama vya siasa kuhakikisha kuwa vinatoa nafasi sawa kwa wanawake na wanaume katika kuwania nafasi mbalimbali za uongozi ambapo kwa sasa amekiri kuwa nafasi ya wanawake ndani ya vyama vya siasa bado ni finyu.

Watanzania wametakiwa kufuatilia Historia ya Nchi yao

Akizungumza kwenye maonesho ya kumbukumbu ya miaka 16 ya kifo cha Baba wa Taifa yanayoendelea mjini Dodoma.  Afisa mipango wa Taasisi ya Mwalimu Nyerere Edgar Tubwanikisye, amesema bado Watanzania wengi hawana utamaduni wa kujisomea kwa nia ya kujipatia maarifa.

Amesema jambo hilo linawafanya wengi wao kutumia hoja zinazotolewa na watu wengine wakiwemo wanasiasa ambao baadhi yao hupotosha.

Amesema kuwa kwa kujisomea na kufuatilia mambo kutoka vyanzo halisi, mtu anaweza kutofautisha ukweli na upotoshaji na hivyo kuelewa hoja mbalimbali na maslahi yake kwa taifa.

Taasisi ya Mwalimu Nyerere ni moja ya taasisi zinazotunza mamabo mbalimbali yanayomhusu Mwalimu katika harakati zake za kulikomboa Taifa.

Kufichuliwa uhusiano wa Israel na Saudi Arabia

Mjumbe wa Baraza Kuu la Mapinduzi ya Yemen Bwana Abdur Rahman Mukhtar amesema kuwa Israel inashirikiana na Saudi Arabia kufanya ujasusi nchini Yemen na kwamba ndege za kivita za pande hizo mbili zinashambulia kwa pamoja maeneo mbalimbali ya nchi hiyo. 
Amesema kuwa Saudi Arabia imeshambulia maeneo mawili ya Yemen kwa kutumia silaha ambazo Mashariki ya Kati hazipatikani katika nchi yoyote isipokuwa katika utawala ghasibu wa Israel. Ameongeza kuwa mmoja wa maafisa wa zamani wa ngazi za juu wa Saudia aliyefanya safari huko Tel Aviv amemshukuru Waziri Mkuu wa Israel, Benjamin Netanyahu kwa kuupa utawala wa Riyadh silaha za aina hiyo.
Saudi Arabia na waitifaki wake tarehe 26 Machi mwaka huu walianzisha mashambulizi makali dhidi ya taifa la Yemen kwa kisingizio cha kumrejesha madarakani rais aliyetoroka nchi. Miongoni mwa jinai kubwa za Saudi Arabia huko Yemen ni kuushirikisha moja kwa moja utawala wa Kizayuni wa Israel katika mashambulizi ya anga, nchi kavu na majini dhidi ya Waislamu wa Yemen.
Siku chache zilizopita uongozi wa Jeshi na Kamati za Wananchi wa Yemen ulitangaza kuwa una habari za kushiriki moja kwa moja utawala wa Kizayuni wa Israel katika mashambulizi ya anga, nchi kavu na baharini katika muungano wa Saudia dhidi ya eneo la Bab al Mandab.
Wakati huo huo Mkuu wa majeshi ya Israel alisema siku chache zilizopita katika Taasisi ya Siasa za Mashariki ya Kati mjini Washington huko Marekani kwamba jeshi la utawala huo linatilia maanani eneo la Babul Mandab.
Lango la Babul Mandab ni njia kuu ya baharini kutoka Asia kuelekea Ulaya na Marekani na lina umuhimu mkubwa sana kwa uchumi wa dunia hususan kwa nchi na madola makubwa. 
Katika upande wa pili vita vinavyopiganwa na Saudia kwa niaba ya nchi nyingine vinapaswa kutazamwa katika fremu ya mipango na njama kabambe za Marekani na Wazayuni katika eneo la Mashariki ya Kati. Kwa msingi huo vita vya Yemen ni mwanzo wa mpango wa Marekani na waitifaki wake wa kuigawa nchi hiyo na baadaye nchi za Iraq, Syria, Misri na huenda hata Saudi Arabia yenyewe.

Njama na mipango hiyo ya Marekani inaonesha kuwa nchi hiyo ingali inafuatilia siasa zake za kikoloni na kujuba zinazofanyika chini ya majina ya Mashariki ya Kati Kubwa au Mashariki ya Kati Mpya ambayo miongoni mwa vielelezo vyake vikuu ni kuzigawa nchi nyingi za eneo hilo na kutimiza ndoto ya Israel ya kuunda dola la Kiyahudi ambalo mipaka yake ni kuanzia mto Nile hadi Furati (Euphrates).
Kwa mijibu wa ramani zilizotolewa hadi sasa kuhusu mpango wa Mashariki ya Kati Kubwa, Yemen ni miongoni mwa nchi zinazolengwa katika mpango huo. Kwa msingi huo ili kuweza kufikia malengo yao huko Yemen, Wamarekani wanatumia fursa zote na wanawaona watawala wa kifalme wa kizazi cha Aal Saud kuwa ndio wenzo na chombo bora zaidi cha kutumia katika vita vinavyopiganwa huko Yemen kwa niaba ya Marekani na Israel.

Jambo la kusikitisha zaidi ni kuwa nchi za Kiarabu nazo badala ya kuisadia nchi ya Yemen kwa ajili ya kutatua mgogoro wa sasa, zimejiunga Aal Saud katika kutekeleza mipango ya Kimarekani na Kizayuni ya kutaka kuzidhoofisha nchi za Kiislamu za Mashariki ya Kati.
Mashambulizi ya kigaidi na harakati za kiadui za kizazi cha Aal Saud katika kanda hii vinaonesha kuwa nchi zinazohitilafiana au kupinga siasa za Marekani na Israel ndizo zinazolengwa na kukumbwa zaidi na mashambulizi ya kigaidi ya makundi ya kitakfiri na Kiwahabi. Kwa msingi huo kuna ulazima wa Waislamu kuwa macho na makini zaidi mbele ya njama hizo chafu.chanzo irib

Putin asema jeshi linaendelea kupiga hatua Syria

Rais Vladimir Putin wa Russia amesema mashambulizi ya anga ya jeshi la nchi yake dhidi ya magaidi nchini Syria yamekuwa na matokeo mazuri tangu yalipoanza na kwamba serikali na jeshi la nchi yake litaendelea kuiunga mkono serikali halali ya Damascus. 

Akizungumza kwenye mahojiano na kanali moja ya televisheni nchini Russia, Rais Putin amesema kuwa hakuwezi kufanyika mazungumzo ya amani kwa ajili ya kutatua mgogoro wa Syria ilihali bado makundi ya kigaidi yanaendelea kushambulia raia. Hii ni katika hali ambayo ripoti zinaonyesha kuwa, jeshi la Syria likisaidiwa na ndege za kivita za Russia limeweza kuwarudisha nyuma magaidi na kudhibiti maeneo kadhaa katika mkoa wa Hama, magharibi mwa nchi.
Huku hayo yakijiri, Mawaziri wa Mambo ya Nje wa nchi za Umoja wa Ulaya mapema leo wametoa taarifa ya kukosoa hatua ya Russia ya kushambulia ngome za magaidi nchini Syria. Taarifa hiyo iliyotolewa baada ya mkutano wa mawazi hao huko Luxemburg imesema Russia inalenga kudhoofisha wapinzani wa Syria badala ya kupambana na magaidi. Tuhuma hizo za EU zimekanushwa vikali na serikali ya Moscow.chanzo irib

Wanasheria: Liundwe jopo kufuatilia maafa ya Mina

Wataalamu na wanasheria wamesema kuna udharura wa kuundwa "jopo la waamuzi" la kufuatilia maafa ya Mina. Abbas Ali Kadkhodai, mhadhiri wa Taaluma ya Sheria wa Chuo Kikuu cha Tehran amesema maafa ya Mina yameweka wazi suala la mas-ulia ya viongozi wa Saudi Arabia kwa sababu ima kuna uzembe au kosa la makusudi lililofanywa katika maafa hayo. 

Akizungumza katika majadiliano maalumu ya kuzungumzia kadhia ya Mina, mhadhiri huyo wa Sheria katika Chuo Kikuu cha Tehran ameongeza kuwa katika sheria za kimataifa serikali zina jukumu la kulinda raia wa kigeni na mas-ulia ya kudhamini usalama wa maisha yao. 
Mehdi Davatgari, mtaalamu wa sheria na mjumbe wa Kamati ya Bunge ya Usalama wa Taifa na Sera za Nje amesema kuhusiana na maafa ya Mina kuwa mbali na suala la kuundwa kamati ya kutafuta ukweli itakayoweza kuchunguza nukta mbalimbali kuhusiana na maafa hayo, kufidia hasara ndiko kunakoufanya utawala wa Aal Saud uwe na mas-ulia juu ya kadhia hiyo. 

Fadhlullah Musavi, mkuu wa zamani wa kitengo cha Sheria na Sayansi ya Siasa cha Chuo Kikuu cha Tehran amesema kamati ya kutafuta ukweli kwa ajili ya kufuatilia maafa ya Mina inapasa iundwe na Umoja wa Mataifa. 

Amefafanua kuwa utendaji dhaifu wa serikali ya Saudia katika maafa ya Mina unalifanya liwe na udharura na ulazima suala la uundaji kamati ya kimataifa ya kutafuta ukweli kwa ajili ya kufuatilia maafa hayo.chanzo irib

Dc Paul Makonda Aongoza Matembezi ya Vyama vya Siasa Kuombea Nchi Amani Kuelekea Uchaguzi Mkuu

Mkuu wa Wilaya ya Kinondoni, Paul Makonda (kulia), akihutubia wananchi baada ya kupokea matembezi ya amani ya vyama vya siasa yaliyofanyika kuanzia eneo la Magomeni hadi viwanja vya Kinondoni Biafra Dar es Salaam leo asubuhi.

Mwenyekiti wa Kamati ya Amani wa dini zote Mkoa wa Dar es Salaam, Sheikh Alhad Mussa Salum, akiongoza dua za kuombea nchi amani katika mkutano huo.

Vijana wa Joging wakishiriki matembezi hayo
Na Dotto Mwaibale
 
Mkuu wa Wilaya ya Kinondoni Paul Makonda amesema kila mtu ana wajibu wa kuilinda na kudumisha amani iliyodumishwa na waasisi wa nchi hii hasa katika kipindi hiki cha kuelekea uchaguzi mkuu utakaofanyika Oktoba 25 mwaka huu.
Makonda alitoa mwito huo wakati akihutubia wananchi baada ya kupokea matembezi ya kuombea nchi amani yaliyofanyika katika viwanja vya Biafra Dar es Salaam leo.
Maandamano hayo yameratibiwa na Makonda katika wilaya yake kwa niaba ya watanzania wote.
Makonda alisema Tanzania ni miongoni mwa nchi chache zilizodumu kwa amani na amani hiyo ilidumishwa na waasisi wa Taifa hivyo imebaki kuwa kimbilio na tegemeo kwa watanzania.
Alisema ili kuwaenzi waasisi hao ni kutunza tunu hiyo na kwamba yapo mataifa yamepita katika nyakati mbalimbali za uchaguzi lakini hawana amani kama tuliyonayo hivyo tuna wajibu mkubwa kuitunza.
“Vipo viashiria vya uvunjifu wa amani, lakini ikumbukw kuwa amani ni kubwa kuliko ahadi za mgombea yoyote wa chama cha siasa hivyo hakuna kinachoweza kufanywa na mgombea yeyote kama hakuna amani,”alisema.
Hata hivyo Makonda alisema kuwa aliandika barua kwa kila chama cha siasa ambapo vyote vilithibitisha kushiriki lakini cha kushangaza baadhi havijahudhuria kwa kutoa sababu zisizo na msingi wowote kama kutokuwa na nauli na mambo mengine.
“Niliviandikia barua vyama vyote, lakini vingine havijahudhuria kwa makusudi hivyo dalili mnayoona hapa ni dalili tosha kuwa amani wanayohubiri kwenye majukwaa si hii wanayoitaka,”alisema Makonda.
Makonda aliongeza kuwa vyama vilivyoshiriki katika maandamano hayo ya amani ni CCM, CUF, UPDP, UDP,UMD, Jahazi asilia na vilabu vya Jogging .
Akizungumza katika mkutano huo Mwenyekiti  wa Kamati ya Amani Mkoa wa Dar es Salaam, Sheikh Alhad Mussa Salum alisema mtu yeyote asiyependa  amani ni adui wa Mungu.
Sheikh Alhad aliitoa kauli hiyo aliitoa Dar es Salaam leo wakati alipoongoza dua maalum ya kuombea amani wakati wa maandamano ya vyama vya siasa yaliyofanyika kuanzia eneo la Magomeni hadi viwanja vya Kinondoni Biafra.
Alisema kuwa anavipongeza vyama vilivyothibitisha kushiriki maandamano hayo pamoja na Mkuu wa Wilaya ya Konondoni, Paul Makonda na kamati ya ulinzi kwa kuandaa shughuli hiyo.
Alisema kuwa kuna baadhi ya vyama ambavyo vilitakiwa kushiriki lakini havijashiriki ambapo havijaathiri chochote na kuweka wazi kuwa wachache wanaweza kufanya mambo kwa ajili ya wengi.
“Kuna baadhi ya vyama havijashiriki maandamano haya, hivyo vikumbuke kuwa watu wachache wanaweza kufanya mambo kwa ajili ya wengi hivyo ni jambo kubwa na kwamba mungu analisikia,”alisema.
Wakizungumza kwa nyakati tofauti baadhi ya viongozi na wawalikishi wa vyama hivyo walisema kuwa watanzania wanapaswa kupiga kura kwa amani pia walishamaliza wakatulie nyumbani kusubiri matokeo kutoka kwa mawakala wanaowaamini waliowaweka vituoni.