Monday, October 12, 2015

Msajili wa Vyama vya Siasa Ahimiza Kulinda Amani ya Nchi Kuelekea Uchaguzi Mkuu

Msajili wa vyama vya siasa nchini Tanzania Jaji FRANCIS MUTUNGI akizngumza na wanahabari mapema leo Jijini Dar es salaam,pembeni ni msanii wa mashairi nchini Mrisho Mpoto

Msanii wa nyimbo za injili nchini Tanzania CHRISTINA SHUSHO akizngumza katika mkutano huo jinsi alivyojiandaa kuelimisha watanzania jinsi ya kuilinda amani yetu 
Msajili wa vyama vya siasa nchini Tanzania Jaji FRANCIS MUTUNGI amewataka viongozi wa vyama vya siasa nchini kuhakikisha kuwa wanatoa matamko na maelekezo kwa wanachama wao wasishiriki katika aina yoyote ya vitendo vya uvunjifu wa amani kipindi hiki cha uchaguzi mkuu kwani amani ya Tanzania ni jukumu la kila mtanzania kuhakikisha anailinda.
 
Jaji MUTUNGI ameyasema hay leo jijini Dar es salaam mbele ya wanahabari wakati akitangaza kuanza kwa kampeni ya ofisi yake ya kuhamsisha utulivu na amani miongoni mwa watanzania kampeni ambayo pia itawashirikisha baadhi ya wasanii wa music wa kitanzania akiwemo Mrisho mpoto na mwimbaji wa nyimbo za injili Christina Shusho.
 
Ameeleza kuwa ofisi ya msajili ina imani kuwa viongozi wa kisiasa wanao ushawishi kwa wafuasi na mashabiki wa vyama vyao hivyo ni wakati wa viongozi hao kutumia nafasi hiyo kusisitiza amani na umoja miongoni mwa watanzania na kuepuka kutoa matamko ambayo yanaweza kuwaibua wanachama wao kufanya fujo na kuiharibu amani ya Tanzania iliyodumu zaidi ya miaka 50.
 
Amesema kuwa ni muda wa watanzania kutambua kuwa utofauti w2a itikadi wa vyama ndio ukomavu wa democrasia nchini hivyo ni jambo la busara kuvumiliana na kufanya siasa za kustarabu,huku akisisitiza kuwa hiki ni kipindi cha mpito na tusikiruhusu kikavuruga amani ya Tanzania kwani kuna maisha baada ya uchaguzi na mwisho wa uchaguzi huu ni mwanzo wa chaguzi nyingine.

Wasanii ambao watashiriki katika kampeni hiyo ambao ni Mrisho Mpoto na Cristina Shusho kwa pamoja wamesema kuwa amani ya Tanzania haiwezi kujengwa kwa itikadi ya vyama vya siasa wala dini wala kabila bali utanzania wetu ndio unaoweza kuendelea kuilinda Tanzania hivyo wamewasihi watanzania kuachana na itikadi za kiivyama na kuweka mbele utanzania ambao ndio nguzo kuu ya amani ya Tanzania.

Wadau wa Usafirishaji Waiomba Serikali Kusimamisha Ongezeko la Tozo Bandarini

Rais wa Chama cha Wasafirishaji Tanzania (TAT), Zacharia Hans Pope (kushoto), akizungumza na waandishi wa habari Dar es Salaam leo, kuhusu  changamoto ya sheria ya ongezeko la thamani VAT katika mizigo inayosafirishwa kwenda nje ya nchi. Kulia ni Rais wa Chama cha Mawakala wa Forodha Tanzania (TAFFA), Stephen Ngatunga

Rais wa Chama cha Mawakala wa Forodha Tanzania (TAFFA), Stephen Ngatunga (kushoto), akizungumza katika mkutano huo. Kulia ni Makamu Mwenyekiti wa TAT, Omar Kiponza

Rais wa Chama cha Wasafirishaji Tanzania (TAT), Zacharia Hans Pope (wa pili kushoto), akiwa na viongozi wengine meza kuu.
Na Dotto Mwaibale
 
WADAU wa usafirishaji wa mizigo kwenda nje ya nchi wameiomba serikali kusimamisha kwa muda sheria ya tozo la VAT katika mizigo inayosafirishwa ili kulinusuru taifa kiuchumi.
Ombi hilo limetolewa na Rais wa Chama cha Wasafirishaji Tanzania (TAT), Zacharia Hans Pope wakati akizungumza na waandishi wa habari Dar es Salaam leo asubuhi kuzungumzia changamoto ya sheria hiyo.
“Sheria hii haina manufaa yoyote katika kuinua uchumi wa nchi yetu kwani imesabisha mizigo kupungua katika bandari yetu kutokana na wadau wa usafirishaji kuanza kutumia bandari za nchi jirani kwa kuogopa kulipa kodi hiyo ya mizigo” alisema Hans Pope.
Alisema hivi sasa katika bandari ya Dar es Salaam kumekuwa na upungufu mkubwa wa mizigo jambo lililosababisha magari ya mizigo kushindwa kusafiri hivyo kutishia ajira na maisha ya watu wanaotegemea kuishi kwa kutegemea usafirishaji.
Makamu Mwenyekiti wa TAT, Omar Kiponza alisema tozo hiyo ya mizigo inayosafirishwa nje ya nchi imeleta changamoto kubwa kwa wadau wa usafirishaji kwani kuna magari zaidi ya 450 ya moja ya kampuni yaliyokuwa yakienda nchi ya nchi na mizigo wa mwezi yamefungiwa ndani bila kufanya safari zozote.
Rais wa Chama cha Mawakala wa Forodha (TAFFA), Stephen Ngatunga alisema ni muhimu kwa serikali kuangalia sheria hiyo ili iwe na manufaa kwa nchi badala ya kuwakandamiza wadau wa usafirishaji.
Alisema hivi sasa miziogo mingi imekuwa ikipishwa katika bandari za nchi jirani kwa kukwepa tozo hilo jambo ambali linaweza kuporomosha uchumi wa nchi unaotegemea sekta ya usafirishaji.
Alisema hivi sasa usafirishaji wa mizigo katika bandari ya Dar es Salaam umeanza kudorora kwa kiasi kikubwa na kuiomba serikali kuliangalia jambo hilo kwa makini ikiwa ni pamoja na kukutana na wadau wa usafirishaji ili kunusuru jambo hilo.
“Unajua kupitishwa kwa sheria hiyo kulifanyika haraka bila ya serikali kukutana na wadau wa usafirishaji ili kujua changamoto zao tunaomba tukutane na serikali ili kujadili jambo hili kwa kina kabla mambo hayajaharibika zaidi” alisema Ngatunga.