|
Katibu Mkuu Wa
Chama cha Wananchi CUF, Mhe. Maalim Seif Sharif Hamad |
Katibu Mkuu Wa
Chama cha Wananchi CUF, Mhe. Maalim Seif Sharif Hamad amesema umoja wa
katiba yawananchi Ukawa wakati utakapofika utahakikisha unaweka mgombea
mmoja wa Urais aliye madhubuti mwenye uwezo wa kusimamia mabadiliko na
kutatua shida zinazowakabili Watanzania.
Maalim Seif amesema hayo
katika mkutano wa hadhara uliofanyika katika uwanja wa Manzese kwa
Bakhresa mara baada ya kumaliza ziara ya kukagua uhai wa chama, kuzindua ofisi mpya za mitaa na Kata katika Wilaya za Temeke, Kinondoni na Ilala Dar es Salaam.
Maalim Seif amesema lengo la ushirikiano wa vyama hivyo ni kuwaongoza
wananchi kukikataa CCM kwa vile kwa muda wa miaka 53 kimeshindwa kuweka
sera nzuri zitakazowaletea maisha bora Watanzania.
Ameeleza kuwa
chini ya Serikali itakayoongozwa na Ukawa kila mtu atakuwa na haki ya
kujiamulia ni namna gani anataka kuishi kwa sababu kipaumbe kitakuwa ni
kuwapatia wananchi uwezo ukiwemo wa kitaaluma kumuwezesha kila mtu
kutumia kipaji chake kuishi maisha bora.
Maalim Seif alisema hayo
yanawezekana na zipo nchi kama Korea ya Kusini ambazo zilipata uhuru
wake sawa na Tanganyika, lakini nchi hizo zimeweza kupiga hatua kubwa
kimaendeleo na kuzikaribia nchi zinazoitwa zimeendelea.
Amesema
chini ya utawala wa CCM hali ni tafauti kwa sababu elimu inapatikana kwa
matabaka kwa kuzingatia wenye uwezo ambao wanamudu elimu bora na
wasiokuwa na uwezo ambao wamekuwa wakiishia katika shule za Kata zenye
mazingira duni .
“Huu wetu ni umasikini wa kujitakia, nchi yetu
ina utajiri mkubwa kuna kila aina ya madini, lakini wanaonufaika ni
wageni na viongozi mafisadi, tushirikiane kuiondoa CCM tujenga Tanzaia
mpya yenye matumaini”, alihimzia Maalim Seif.
Naibu Katibu Mkuu
wa CUF Tanzania Bara, Magdalena Sakaya akizungumza katika mkutano huo
alisema kutokana na sera mbaya za CCM nchi imekosa viwanda ambavyo vina
nafasi kubwa ya kuleta ajira na kupunguza umasikini miongozi mwa
wananchi.
Alisema wakati Tanzania ni nchi inayotegemea zaidi
shughuli za kilimo na ufugaji, hakuna viwanda vya kusindika nyama,
maziwa wala mazao ya kilimo na kila kitu kinaagizwa kutoka nje ya nchi.
“Hii ni aibu CCM haina sera zenye mwelekeo wa kuwaletea maisha mazuri
wananchi, leo hii ni miaka minane wafanyabiashara wadogo wameahidiwa
kupatiwa eneo la Machinga Complex lakini hakuna kilichoendelea ni ahadi
zisizotekelezwa”, alisema Sakaya.
Mbunge wa Viti Maalum Kulthum
Mchuchuri alisema uchaguzi wa Serikali za mitaa unaotarajiwa kufanyika
Disemba 14 mwaka huu utumiwe na wananchi kukikataa CCM ili iwe salamu
tosha kwamba wananchi wameamua kukiweka pembeni.