Kiongozi wa Waislam Shia Ithnasheriya Maulana Sheikh Hemed Jalala akiongea katika Sherehe ya Maulid ya Mtume Muhammad (s.a.w.w) katika Viwanja vya Pipo Kigogo Dar es salaam. |
Ndugu zangu Amani ya Mwenyezi Mungu iwe kwenu Watanzania
wote, Waislamu na Wasiokuwa Waislamu.
Siku hii ya leo ni mtiririko wa masiku ya kumkumbuka Kiongozi
wa Waislamu, Kiongozi wa Utu, Kiongozi wa Wanadamu, Mtume alietumwa kwa ajili
ya watu wote ambae ni bwana Mtume Muhammad (s.a.w.w) kutoka mwezi 12 wa mfungo
sita mpaka leo hii mwezi 17 tunakuwa tukisheherekea mazazi ya bwana mkubwa na muheshimiwa
huyu ambae ni Mtume Muhammad (s.a.w.w).
Mtume Muhammad (s.a.w.w) mazazi yake ni muhimu kukumbukwa kwa
sababu ni mtu ambae leo wanadamu wanamuhitajia , Mtume Muhammad (s.a.w.w)
aliyoyafunza, Mtume aliyoyaelekeza , Mtume Mwenendo wake, leo hii duniani
wanamuhitajia , Dunia ya leo inahitajia huruma ya Mtume Muhammad (s.a.w.w),
“Hatukukutuma isipokuwa ni Rahma” ni ili uju ufunze huruma, uje ufunze upendo,
uje ufunze mshikamano, uje ufunze umoja, hayo ni mafunzo aliyoyafunza Mtume
Muhammad (s.a.w.w).
Naamini leo dunia na Tanzania vilevile wanahitajia huruma ya
Mtume Muhammad (s.a.w.w) iwepo, huruma imesambaratika , Mtume Yule aliyekuwa
akiwajali mayatima, Mtume Yule aliyekuwa akiwajali wajane, Mtume Yule aliyekuwa
akiwajali watu wanaoishi katika mazingira magumu, huruma hii ulimwenguni
inahitajika, huruma hii Tanzania inahitajika.
Mtume Muhammad (s.a.w.w) ana haki ya kukumbukwa kwa nini ?
kwa sababu leo dunia inahitajia Umoja, Waislamu wanahitajia Umoja, Mtume
Muhammad (s.a.w.w) katika Mafunzo yake yote aliyoyafunza ilikuwa ni mshikamano,
Umoja Mtume aliufunza Kimaneno na Kivitendo, leo dunia inahitajia Umoja katika
Waislamu.
Mtume Muhammad (s.a.w.w) ameufunza Umoja wa Dini zote, amekaa
na watu wa dini tofauti akakaa nao vizuri, naamini Umoja huu vile vile wa Dini
ya Uislamu na Dini zingine wanadamu hususan watanzania wanauhitajia, hayo ni
mafunzo machache ambayo walimwengu wanayahitajia.
Siku hii ya kukumbuka Mazazi ya Mtume Muhammad (s.a.w.w) ni
siku ya kukumbuka mafunzo haya mazuri ambayo Mtume ameyafunza, Mtume Muhammad
(s.a.w.w) yeye mafunzo makubwa aliyokuwa akiyafunza moja wapo ilikuwa ni funzo
la Amani, ilikuwa ni funzo la Utulivu, ilikuwa ni funzo la kukaa Vizuri na
akatufundisha baada ya swala tuwe tunamuambia Mungu “Mungu wewe ni Amani, kwako
wewe siku zote inatoka Amani Mungu tufanye Tukae kwa Amani”.
Kwahivyo Moja ya Mafunzo yanayotakikana kuenziwa kipindi hiki
hususan hapa Tanzania na Duniani kote ni jambo kubwa la Amani, la watu kukaa
Vizuri, la watu kuishi kama Ndugu, la watu kuishi kama Wanadamu.
Hongereni Sana kwa Mazazi haya ya Mtume Muhammad (s.a.w.w),
Hongereni Sana kwa Mazazi ya Kuzaliwa Kiumbe hiki ambacho leo Walimwengu wote
wanakihitajia, Hongereni sana kwa Mazazi mema ya Mtume Muhammad (s.a.w.w),
Asanteni Sana.
Imetolewa na: Maulana Sheikh Hemed Jalala Kiongozi wa Waislam Shia Ithnasheriya Tare:15.11.2019-Viwanja vya Pipo Kigogo Post Dar es salaam.