Amani ya
Mwenyezi Mungu iwe Kwenu Nyote.
Siku hii ya leo ambayo ni swa na Tarehe 25.12.2019 sawa na
mwaka Kiislamu wa 1441, siku hii ya leo Ndugu zetu wakristo wa hapa Tanzania na
duniani, wanasheherekea Siku ya Krismasi au mazazi ya Nabii Issa (a.s) kwa sisi
waislam,au Yesu Kristo kwa ndugu zetu Wakristo wa hapa Tanzania na Duniani.
Sisi kama Waislamu wa Madhehebu ya Shia Ithnasheriya, sisi
kama Viongozi wa Taasisi ya Imam Swadiq (a.s) iliyopo Kigogo Post Dar es
salaam, tunapenda Kutoa Mkono wa Kheri, mkono wa Baraka, mkono wa Fanaka kwa
sikukuu hizi mbili za Krismasi na Mwaka Mpya kwa ndugu zetu wakristo wa hapa
Tanzania na nje ya Tanzania na Dunia kwa Ujumla.
Unaweza ukajiuliza kwanini sisi kama Waislamu, sisi kama
Mashia, sisi kama Waumini wa Kigogo tutoe mkono wa Baraka na Kheri kwa ndugu
zetu Wakristo kwa sababu ya Eid yao na sherehe yao ya Krismasi?, ni kwa sababu
tano (5) Muhimu zifuatzo:-
Sababu ya Kwanza: Ndugu zetu Wakristo waliyopo Tanzania na
waliopo Duniani kwa Ujumla tunashirikiana nao katika kuamini kwamba Mwenyezi
Mungu (swt) alituma Vitabu kwa uchache Vinne hapa Duniani, Kitabu cha kwanza ni
Taurat, Kitabu cha pili ni Injil, Kitabu cha tatu ni Zaburi na Kitabu cha nne
ni Qur’an.
Injili ni Kitabu ambacho ndicho kipo mikononi na kukifanyia
kazi na kukiamini Ndugu zetu Wakristo, lakini sisi waislamu katika Imani zetu
ni kuamini Vitabu hivyo vyote, ikiwemo Taurat, Injil, Zaburi na Qur’an,
kwahivyo ni wenzetu kwamba tunashirikiana nao kwa vitabu vilivyoteremshwa
kutoka mbinguni kutoka kwa Mwenyezi Mungu (swt).
Sababu ya Pili: Kwanini Mkono wa Krismasi?, Kwani wa kuwapa
hongera kwa kusheherekea sikukuu yao ya Krismasi?, ni kwa sababu ni Ndugu zetu.
Imam Ali (a.s) anatoa maelekezo wakati akimtuma Malik Ashtar akielekea Misri,
katika maelekezo alimuambia unakwenda Misri huko utakutana na Waislamu ni ndugu
zako katika Dini, lakini utakutana na watu wa Dini Nyingine hao ni ndugu zako
katika Uwanadamu na katika Utu, sisi sote Baba yetu ni Adamu (a.s), tuwe
Waislam, tuwe Wakristo, sisi sote mama yetu ni Hawa au Eva (a.s) tuwe Waislam,
Tuwe Wakristo.
Sababu ya Tatu: Kwanini Mkono wa Kheri na baraka na pongezi
kwa Krismasi kwa ndugu zetu Wakristo wa Watanzania?, ni kwa sababu ni shehemu
ya Watanzania. Kila itakavyokuwa Tanzania ina Waislamu Masuni, ina waislamu
Mashia, ina Mapagani, ina watu wa dini nyingine vile Wakristo nao wapo.
Kwahivyo tutaendelea kubakia kama Watanzania Waislamu,
Watanzania Mashia, Watanzania Masuni, Watanzania Wakristo na Watanzania
wasiokuwa na Dini, kwa hivyo tunapotoa Mkono wa kheri na baraka kwa sababu ya
Krismasi ni moja ya Kuboresha mahusiano mema kwa sababu sisi sote tunakusanywa
na mwamvuli wa Utanzania.
Sababu ya Nne: ni jambo la Kuvumiliana, Qur’an inatueleza
Umma wa kati na kati, yani umma unaovumiliana, moja ya sababu ya sisi kutoa
mkono wa baraka na kheri ya krismasi kwa ndugu zetu Wakristo wa Tanzania, ni
kwa sababu ya kutoa funzo la kuvumiliana kwa watanzania na watu wenye dini
tofauti.
Na kwamba sisi tutaendelea kubakia na dini zetu, wasije
wakadhania Waislam Mashia na Masuni iko siku watawabadilisha Watanzania wote
watakuwa Waislamu, siku hiyo haitotokea, wala Wakristo wa Tanzania wasije
wakadhania watawahubiria Waislamu Mashia na Masuni watakuwa Wakristo. Kwa hiyo
tutabakia Wakristo tupo, Waislamu tupo, Mashia tupo, watu wa Twariqa tupo, kwa
hiyo kubwa ni kuvumiliana tukiwa na dini zetu tofauti na Mitazamo yetu tofauti.
Sababu ya tano: Mwisho jambo la tano muhimu na kubwa, sisi
Tanzania ni watu ambao tunaishi kwa Amani, tunaishi kwa Utulivu, tunaishi kwa
Kheri, Tanzania yetu haijui vita, Tanzania yetu haijui kugombana, Tanzania yetu
haijui Silaha, Utulivu huu na Amani hii kuuboresha ni Wajibu wetu kama Viongozi
wa Dini,ni wajibu wetu kama Wanadini.
Moja ya mambo ambayo tunaamini, yataboresha Amani ya nchi
yetu, yataboresha Umoja wetu wa Wawatanzania, yataboresha kuvumiliana kwetu
tuliokuwa nao Watanzania, ni Vikao kama hivi vya kutoa Mkono wa Kheri ya
Krismasi na Kheri ya Mwaka mpya na baraka ya Mwaka mpya, jambo linaloishiria
Umoja, Mshikamano na Kukaa Vizuri katika nchi Moja na Taifa moja.
Mwisho: Namuomba Mwenyezi Mungu (swt) Krismasi hii ya ndugu
zetu Wakristo, Mwenyezi Mungu aipitishe kwa Kheri, aipitishe kwa baraka, aondoe
majanga na mabalaa yote barabarani na majumbani,na aifanye ni Krismasi ya Kheri
kwa ndugu zetu Wakristo wa Tanzania wote, lakini pia tunamuomba Mwenyezi Mungu
(swt) azidi kuboresha Umoja wetu wa wawatanzania, Amani yetu ya Tanzania,Mungu
aendelee kuifanya Tanzania kisiwa cha Amani,Kisiwa cha Upendo, Kisiwa cha
Kuvumiliana, Asanteni Sana na Mungu awabariki.
Imetolea na:
Maulana Sheikh Hemed Jalala
Kiongozi wa Kiroho wa Waislamu Shia Ithnasheriya
25/12/2019,Masjid Ghadir, Kigogo Post Dar es salaam.