Bismillah Rahman Rahimu
Ndugu zangu Amani ya Mwenyezi Mungu iwe kwenu nyote.
Tunapokumbuka Mazazi ya Imam Mahdi
(a.s), tunakumbuka Utawala Bora.
Napenda nianze kikao change hiki kwa maneno ya Mwenyezi Mungu
(swt) yaliyopo katika Qur’an takatifu Suratul Raad aya ya 7, Mwenyezi Mungu
anasema mwisho wa hii aya : “na hakika hapana vingine wewe Muhammad (s.a.w.w)
ni mwenye kuhofisha na kila watu wanakiongozi wao”
Katika aya hii inakwenda sambamba na tukio la leo la mwezi 15
shabani siku ambayo waislamu duniani na hususan Waislam Shia Ithnasheriya wanasheherekea
na kukumbuka mazazi ya kuzaliwa Imam wa 12 ambae ndie muokozi atakaekuja
kuwaokoa na kuwaongoza walimwengu.
Katika tukio hili la kuzaliwa Imam wa 12 , kwanza napenda
kutoa mkono wa hongera na Baraka na fanaka kwa waislamu wote duniani kwa mazazi
ya Imam Mahdi (a.j.t.s), lakini pia napenda kutoa mkono wa heri fanaka na
Baraka kwa watanzania wenzangu wote, pia kwa wanazuoni na maulamaa wote duniani
na marajiin wetu hususani Kionngozi wa Vyuo vya Kidini Duniani Sayyid Sistani,
pia natoa mkono wa Hongera na kheri iliyojaa fanaka kwa Kiongozi wetu na Naibu
wa Imam wa 12, Kiongozi wa Waislam Duniani Imam Khamenei.
Katika tukio hili la kukumbuka kuzaliwa Imam wa 12 Imam Mahd
(a.s) napenda kuzungumza yakwamba wamekubaliana waislamu wote yakwamba
atadhihiri zama za mwisho Kiongozi anaeitwa Mahdi (a.s) na kwa hili
wamekubaliana vilevile dini zote, Wakristo, Mayahudi, Mabudha na dini za
Kimisri za zamani, kwamba Dunia haiwezi kumalizika lazima atakuja kudhihiri Mtu
ambae ndie atakaeihakikishia duniani imekuwa mahala pa Amani, mahala pa Upendo
na mahala pa mshikamano.
Kwahiyo itikadi ya kudhihiri muokozi hii ni itikadi ya dini
zote, je muokozi huyo ni nani?, sisi waislamu tunasema muokozi huyo ni Imam
Mahdi (a.s) na sisi Waislamu Shia Ithnasheriya btunasema kwamba ndio huyuhuyu
aliezaliwa siku kama ya leo ya mwezi 15 shabani, ambayo tunaiitwa kwa lugha
nyingine siku ya kugawa riziki ambayo waislamu wote hukesha Misikitini na
kuomba dua maalumu.
Lakini kubwa lakuzungumzwa ni malengo ya Imam huyu,na jambo
analotaka kulifanya ni jambo gani?.
Hadith zinasema bwana huyu atakapodhihiri ataijaza dunia uadilifu,
ataijaza dunia haki, ataijaza dunia amani. Kwahivyo niseme yakwamba Imam Mahdi
(a.s) atakapodhihiri atakachokileta ataleta Utawala Bora, atakacholeta ataleta
Utawala anaostahiki mtawala au watawala wawe.
Utawala huo atakaokuja nao Imam Mahdi (a.s) atakuwa ni
mtawala ambae dunia ameijaza uadilifu, ameitajaza amani, ameijaza haki. Katika
utwala bora wa Imam Mahdi (a.s) ni utawala utakao kuwa vitu vitano vifuatavyo:
Jambo la kwanza:
Ubaguzi, Bwana huyu
atakapodhihiri atapambana na kuondoa Ubaguzi, atapambana kuhakikisha ubaguzi
haupo, nah ii ni moja katika siri ya Utawala Bora.Aina zote za Ubaguzi atazisambaratisha, Ubaguzi wa mweupe na
mweusi kwake kutakuwa hakuna katika utawala wake kwamba mweupe ni bora mweusi
si bora au mweusi ni bora mweupe sio bora hilo litakuwa hakuna.
Ubaguzi wa
Ukabila, kabila fulani ndio kabila bora kabila fulani sio kabila bora kwenye
utawala wake bora, ubaguzi huo hautakuwepo.kuwabagua watu kwa dini zao huyu ni
mwislam, huyu ni mkristo, huyu ni Yahudi, ubaguzi huo utakuwa haupo.ataondoa
ubaguzi hata ndani ya madhehebu hakutokuwepo huyu ni bohora, huyu ni
Mwiithnasheriya, huyu ni Mwiismailia, huyu ni sunni, huyu ni Shia, huyu ni
Ibaadhi, huyu ni shafii, huyu ni kadiria, aina hizo za ubaguzi kwenye utawala
wake bora zitakuwa hazipo.
Kwahivyo leo tunapokumbuka mazazi ya Imam Mahdi (a.s) tunakumbuka
Utawala Bora atakaouleta bwana huyo. Sihivyo tu Utawala wake hautakuwa na
Ubaguzi wa Mitaa, wilaya na Mikoa kwamba kuna mkoa fulani ni bora zaidi, mkoa
wa tanga ni bora, mkoa wa Dar es salaam ni Bora, mkoa wa Arusha ni bora mikoa
mingine si bora, Taifa fulani ni bora, nchi fulani ni bora.kwake yeye la, ubaguzi wa hata wa aina hiyo wa kimaeneo kwake
yeye haupo. Hii ni moja na siri ya Utawala bora, Utawala bora ni Utawala ambao
unalenga maeneo yote katika kupeleka huduma na kuwaangalia watu.
Jambo la pili:Kuwatumikia
watu, bwana huyu
atakapodhihiri atahakikisha anawatumikia wanadamu,Mtume Muhammad (s.a.w.w)
anasema bora ya Jambo ni kuwatumikia watu, Utawala wake utawatumikia watu kwa
kila mambo muhimu, huduma za kijamii, kama vile huduma ya elimu itakuwa kwa
watu wote, haitobagua watu.
Utawala wake ni utawala hautokuwa na wajinga,ni Utawala wa
kuhakikisha unafuta ujinga,ni Utawala ambao watu wake watakuwa na masomo yao ya
mwanzo mpaka masomo ya juu, kupatikana Profesa, Injinia, watu wenye PHD katika
jamii yake ni kitu cha kawaida nah ii ndio siri ya Utawala bora. Babu yake Imam
Mahdi (a.s) ambae ni Mtume Muhammad (s.a.w.w) anasema anaetaka dunia lazima awe
na elimu, na anaetaka akhera lazima awe na elimu.
Katika utawala wake Tiba
itaboreshwa kwa hali ya juu, maji salama na safi ndio watakao kunywa wanadamu,
maisha yatakuwa mazuri kwa watu, nah ii ndio siri ya Utawala bora.Mtawala bora
ni Yule anaejali watu wake, ni Yule anaetaka huduma ziwafikie wanadamu wote na
watu wake wote, hivyo ndivyo atakavyokuwa Imam Mahdi (a.s).
Jambo la tatu:Mivutano, bwana huyu atakapodhihiri atahakikisha
kwamba anaondoa mivutano iliyopo kwa walimwengu wote na hiyo ndio sifa ya
Utawala bora, Utawala bota ni ule utawala ambao unahakikisha hauna mivutano, ni
utawala wenye maelewano.ataondoa mivutano ndani ya Jamii, ndani ya Taasisi,
ndani ya nyumba za ibada,zitakuwa hazina mivutano, ataelekeza watu wapendane,
watu washikamane na wamtumukie mungu mmoja, wasitumikie waungu wengi ambao ndio
sababu ya mivutano tulionayo katika jamii yetu.
Jambo la nne:Ufisadi, bwana huyu atakapodhihiri
atahakikisha anaondoa ufisadi, Ufisadi katika Nyanja zote na ufisadi wa waina
yoyote,.Yeye atapambana na Ufisadi, atahakikisha Rushwa hailiwi katika jamii
yake, na kataika utawala wake, na ndio maana tukauita utawala wa Imam Mahd
(a.s) ni Utawala bora, Rushwa itakuwa ni Marufuku, Mikataba feti kwake itakuwa
hakuna.
Wafanyakazi hewa katika Utawala wake kutakuwa hakuna,
hakutokuwa na matengenezo ya ujanja ujanja kitu kimetengenezwa kwa kitu kidogo
lakini mahesabu ni mengi, hapana, Ubabaishaji huo katika Utawala wake kutakuwa
hakuna kwa sababu, watu wanamtambua Mungu, watu wanamuelewa Mungu, Utawala wake
ni Utawala unaolinda mali za Umma, unaolinda mali za Watu.
Jambo la tano : Amani, na la mwisho atahakikisha amani
inatawala kuanzia ngazi ya mtaa, kijiji, tarafa , Kata, wilaya, Mkoa, Taifa na
dunia yote itakuwa ni mahala pa utulivu na amani. Katika Utawala wa Imam Mahdi
(a.s) Amani itakuwa inachukua nafasi ya kwanza,riwaya zinatuambia yakwamba
katika Utawala wa Imam Mahdi (a.s) katika Utawala wake Bora utakuwa Mtu
unatembea masaa 24 hakuna mtu atakaekunyanganya kidani chako cha dhahabu, mama
hawezi kunyanganywa herein yake alievaa hata usiku wa manane.
Kwahiyo atahakikisha amani imeboreka kwa ngazi zote na kwa
dunia, Amani kwa mtu mmoja mmoja, amani kwa upande wa Familia, amani kwa upande
wa jamii, amani kwa mji mzima, amani kwa mabara yetu na amani kwa dunia nzima,
itakuwa ni wakati ambao Amani imetanda , upendo umetawala, watu wanamtambua
mungu mmoja, wanamuabudu mungu mmoja, hivi ndivyo utakavyokuwa utawala wa Imam
Mahdi (a.s).
Hayo ni mambo matano Imam Mahdi (a.s) atakapodhihiri
atapambana nayo na kuhakikisha yanatawala, na ndio maana tukasema Utawala wale
ni Utawala bora, Kwahivyo katika siku hii tunayokumbuka mazazi ya Imam Mahdi
(a.s) ni siku ya kukumbuka na kujifunza utawala bora,Utawala wa Imam Mahdi
(a.s) ambapo utawala huo utakapokuwepo mahali popote, basi mahali hapo itakuwa
ni pepo na mahali hapo.
Asanteni sana, namuomba Mwenyezi Mungu (swt) kwa Baraka ya
Kuzaliwa Imam Mahdi (a.s), Mwenyezi Mungu atupe nguvu za kuweza kuienzi amani,
maelewano mazuri, Tanzania iendelee kubakia kisiwa cha amani, mahala pa watu
wanaopendana, mahala panapokimbiliwa na watu, kwasababu ya hali yake nzuri ya
hewa lakini kwasababu ya watu wake wanavyowapenda watu,na kwasababu ya watu
wake wanavyopenda amani, asanteni sana na Mungu awabariki.
Imetolewa na:
Maulana Sheikh Hemed Jalala
Kiongozi Mkuu wa Waislamu Shia Ithnasheriya Tanzania
Tare:Jumamosi, 20.04.2019 Sawa na 14 Shaban 1440.
No comments:
Post a Comment