Bismillah Rahmani Rahimu
Ndugu
zangu Amani ya Mwenyezi Mungu iwe kweny nyote
Siku ya Israa na Miiraj ni siku ya
kuwafunza Watanzania Elimu,Maadili Mema, Umoja wa Dini zote na kuenzi
Amani.
“SUBHANA, Ametakasika aliye mchukua mja wake usiku mmoja
kutoka Msikiti Mtukufu mpaka Msikiti wa Mbali, ambao tumevibariki vilivyo
uzunguka, ili tumuonyeshe baadhi ya Ishara zetu. Hakika Yeye ni Mwenye kusikia
na Mwenye kuona” 17. SURA AL ISRAAI,aya ya 1.
Siku hii ya leo tunasheherekea kwa shangwe na furaha kubwa
matukio mawili makubwa, tukio la kwanza ni tukio la Israa na Miiraj, tukio la
Mtume Muhammad (s.a.w.w) kupelekwa usiku kutoka Makka mpaka Masjid al Aqswa
ulioko Jurusalem nchini Palestina, na baada ya hapo msafara wa kutoka Masjid al
Aqswa kwenda Mbungu za juu.
Na tukio la pili ni tukio la Mtume Muhammad (s.a.w.w)
kukabidhiwa Utume na kupelekwa kama Mtume kwa walimwengu wote, matukio haya
mawili, kwanza kwa matukio haya mawili na kwa sherehe hizi mbili, napenda kutoa
Salamu zangu za dhati kwa Viongozi wa Dini wote, na kwa Marajii wetu wote
wakubwa akiwemo Ayatullah Sayyid Sistan.
Lakini vilevile natoa salamu katika siku hii ya leo ya Israa,
Miiraj na Siku ya Biidha kwa Kiongozi wa Umma wa Kiislamu Duniani Imam
Khamenei,Mwenyezi Mungu amuhafidhi na ambakishe, lakini vile vile natoa salamu
zangu za dhati na hongra na pongezi zangu kwa Imam wa Zama hizi Imam wa 12 Imam
al Mahd (a.j.t.s).Tukio la Israa, Miiraj na Biidhaa lina tafsi nyingi na lina
ishara nyingi, lakini nitapenda kusema tukio hili linaweza kutupa ishara 5
Muhimu.
Ishara ya Kwanza: ni ishara ya Umuhimu wa Elimu, tukio
la Mtume Muhammad (s.a.w.w) la kutoka Makka na kupelekwa Jerusalem nchini
Palestina kwenye msikiti mtakatifu wa al
Aqswa ni tukio la kielimu, ni tukio la kisayansi, ni tukio la kiteknolojia.
Mtume Muhammad (s.a.w.w) kuondoka Masjid al Aqswa kwenda kwenye sayari za juu,
ni ishara ya Elimu, ni ishara ya Sayansi,ni ishara ya Teknolojia.
Na mwenyezi Mungu amelizungumza katika Qur’an “Kama mnaweza
kwenda katika sayari za juu, basi mnaweza kwenda lakini huko kunahitajia
Elimu”. Tukio la Mtume Muhammad (s.a.w.w) kukabidhiwa Utume kwa neon “Soma” ni
dalili ya elimu, kwa hivyo tukio la Israa na Miiraj moja ya funzo yake muhimu
ni funzo ya elimu. Kwa kuwa Israa na Miiraj na kwa kuwa Bi’idha, kupelekwa ni
funzo la elimu ni nafasi yetu na ni muda wetu kutilia umuhimu jambo la Elimu.
Sisi kama Watanzania, sisi kama Waislamu lazima kuhakikisha
watoto wetu wanasoma, watoto wetu wanakwenda Shuleni, watoto wetu wanakwenda
Vyuo, watoto wetu wanakwenda Madrasa, wanakwenda kujisomea kuhakikisha wanakuwa
na elimu. Ilakuwa ni kuwadhulumu haki zao kufikia kwamba kutakuwa na watoto wa
kitanzania ambao hawapelekwi Shuleni.
Hawaendi kusoma au
wako majumbani kwasababu yoyote itakayopatikana, imefikia muda kwa sisi kama
waislamu na kama watanzania kuhakikisha watoto wetu wote wanakwenda masomoni
pasina kuwabagua wawe watoto wa kiume
wawe watoto wa kike kwasababu wote wanahaki ya elimu.
Ishara ya pili: ni ishara ya Umuhimu wa Akida, katika
ishara ya za tukio la Israa na Miiraj pamoja na Bi’idha ni akida, tendo la
Mtume Muhammad (s.a.w.w) kutoka Makka msikitini na kufikizia Masjid al Aqwa hii
ni ishara ya kwamba msikiti mtakatifu wa Masjid al Aqswa ulioko Juerusalem ni
msikiti wa Waislamu, ni mali ya Waislamu na ni haki ya Waislamu, nan i Lazima
(Wajibu) kwa waislamu kuutaka Msikiti wao, kuunadi Msikiti wao,kuhakikisha ya
kwamba msikiti wao upo katika mahali pa amani, kuhakikisha msikiti wao huu
unabakia kumbukumbu yao hii inabakia, Masjid Aqswa msikiti ambao Mtume Muhammad
(s.a.w.w) ndie alievikizia baada ya kutoka msikiti wa Makka.
hii ni ishara kubwa ya kwamba msikiti huu hauna tofauti na
msikiti wa Makka, na kwamba utukufu baada ya Msikiti wa Makka unafuatia msikiti
wa al Aqswa. Kwa hivyo katika fursa hii tunachukua nafasi kuwaeleza maimam wa
Misikiti, kuwaeleza Masheikh kwamba imefikia muda wa kuwaeleza waumuni wao ni
upi msikiti mtakatifu, msikiti mtakatifu ni mali ya nani? Na ni sehemu ya nani
katika ardhi ile ambao upo msikiti mtakatifu.
Ishara ya tatu: ni ishara ya maadili mema, Msafara
wa Israa na Miiraj pamoja na Bi’idha ni msafara unaotupa funzo la Maadili,
msafara unaotupa funzo la maadili mazuri, tendo la mtume Muhammad (s.a.w.w)
tendo la kuingia peponi, tendo la mtume Muhammad (s.a.w.w) kuwaangalia moto na
adhabu zilizopo ndani ya moto na kubainisha Mtume Muhammad (s.a.w.w) ya kwamba
watu walioko mototni ni watu wa aina gani.
Na kwanini walikuwepo ndani ya moto? Na kwanini ipo pepo?,
kwanini Mtume Muhammad (s.a.w.w) alikutana na baadhi ya mambo njiani, alikutana
na Maidhriti na akapewa maneno ya kuyasoma, alikutana na watu wabaya lakini
akapewa kinga ya kujikinga na watu wabaya, alipewa vinywaji akachagua kinywaji
kizuri, kwanini haya yote? Haya yote ni kufunza maadili mema, siku ya Israa na
Miiraj iwe ni siku ya kuwafunza watanzania
ya kuwaelekeza watanzania maadili mema, maadili mazuri, imefikia muda
kuachana na kila jambo ambalo ni maadili mabaya, si mila za watanzania, si mila
za waafrika, si mambo yao, na haya maadili leo ni mengi ambayo ni changamoto
kubwa inayoikabili taifa na inayowakabili watanzania kwa ujumla.
Ishara ya nne: ni ishara ya Umoja wa dini zote, tukio
la Israa na Miiraj pamoja na Bi’idha tunajifunza funzo la Umoja wa dini zote,
Mtume Muhammad (s.a.w.w) baada ya kufika Masjid al Aqswa aliweza kuswali na
Mitume wote (a.s) nay eye akatangulia mbele akawaswalisha , Mitume wote
waliotumwa na Mungu 124,000 walikusanyika pale, wakaswali pamoja na Mtume
Muhammad (s.a.w.w), wakaswali swala moja, wakaomba maombi mamoja,wakakaa kikao
kimoja, wakatanguliwa na mtu mmoja.
Hii ni ishara na ni mafunzo ya kwamba Mitume (a.s) wote
waliotumwa na Mungu, wote ujumbe wao ni mmoja, mafunzo yao ni mamoja, maelekezo
yao ni mamoja. Kwahivyo yeyote hapa Tanzania, yoyote hapa Afrika, yoyote hapa
Duniani atakae kuja na dini yake akafunza kinyume na umoja, akafunza kinyume na
mshikamano, akafunza kinyume na Upendo, huyo amekwenda kinyume mafunzo ya Mitume
(a.s) wote, na maimam wote, Vitabu vyote, na watu waliokusanyika pale katika
msikiti mtakatifu wa al Aqswa na wakamuomba Mwenyezi Mungu na wakaswali swala
moja wakiongozwa ni Mtume Muhammad (s.a.w.w).
Ishara ya tano: ni ishara ya Umuhumu wa kuenzi Amani
na maelewano,Nukta ya tano nay a Mwisho kitendo cha msafara wa Mtume Muhammad
(s.a.w.w) kuondoka mahala panapoitwa Masjid Harraam yaani Msikiti mtakatifu,
nini maana ya msikiti mtakatifu? Msikiti mtakatifu maana yeke ni msikiti ambao
huruhusiwi kumwaga damu, hauruhusiwi vita, hauruhusiwi mapambano, msafara
ukaanzia katika msikiti huo moja kwa moja ukaja msikiti wa pili Masjid al Aqswa, hii ni ishara ya nini? Ni
ishara ya kwamba kilichopo Masjid Haraam ndio kilichopo Masjid al Aqswa,kama
ulivyokuwa Masjid al Haraam Hairuhusiwi Vita,
hauruhusiwi kumwaga damu, hairuhusiwi mapambano.
Hivyo hivyo Masjid Aqswa hairuhusiwi vita vyoyote,
hairuhusiwi kumwaga damu, hairuhusiwi mapambano yoyote, kama ilivyokuwa Al
kaaba ni mahala pa kuenziwa amani, hivyohivyo masjid al Aqswa ni mahala pa
kuenziwa amani,kama ilivyokuwa msafara uliondoka uliondoka kwenye msikiti na
ukafikizia kwenye msikiti, msikiti ni mahala pa amani, msikiti ni mahala pa
upendo, msikiti ni mahala pa kutokumwaga damu.
Tuko dhidi ya yoyote ambae anamwaga damu katika msikiti iwe
ni masjid Haraam iwe ni Masjid al Aqswa, tuko dhidi ya yoyote ambae anatumia
nguvu zake kumwaga damu, iwe ni msikiti ulioko Makka au ni Msikiti ulioko
Jerusalem, yoyote ambae anavunja amani ya sehemu hizi mbili huyo sisi tuko
dhidi yake na hatuko nae na yuko dhidi ya amani ya dunia,yupo dhidi ya Upendo wa Dunia.
Kwa hivyo msafara wa Israa, Miiraj na Bi’idha ya Mtume Muhammad (s.a.w.w) ni
msafara wa unaofunza amani, ni msafara wa kuenzi amani, ni msafara wa kusomesha
upendo na maelewano.
Mwisho: Ujumbe wetu katika siku hii ya Israa
na Miiraj pamoja na Bi’idha ya Mtume Muhammad (s.a.w.w), ujumbe wetu mkubwa
tunaouelekeza kwa watanzania ni Ujumbe wa umuhimu wa Elimu, kimefika kipindi ya
kwamba itakuwa ni kosa la jinai watoto kubakia majumbani pasina kupelekwa
Shuleni, hususani katika kipindi hiki ambacho
Elimu imekuwa ni Elimu ya Bure, nafasi za Shuleni zimekuwa nafasi pana,
ujumbe mkubwa ni kuhakikisha watoto wetu wanasoma, kama tunataka maendeleo ya
familia zetu lazima watoto wetu wasome, kama tunataka maendeleo ya taifa letu
lazima watoto wetu wasome, kama tunaitaka dunia basi watoto wetu wasome, kama
tunataka akhera watoto wetu wasome.
Mwenyezi Mungu nakuomba kwasababu ya tukio la Israa na Miiraj
pamoja na Bi’idha ya Mtume Muhammad (s.a.w.w) Taifa hili ulipe amani, taifa
hili ulipe utulivu, yoyote mwenyekuitakia matatizo na migogoro Tanzania ,
Mwenyezi Mungu huyo asiweze kufanikiwa.
Mwenyezi Mungu endelea kubakiza Upendo na Mshikamano kwa
watanzania wote, endelea kuifanya Tanzania ni kisiwa na amani ni mahala pa watu
wanakaa vizuri,na Mshikamano watu wasioelewa Vita wala kugombana , Asanteni
sana, Miiraj njema, Israa njema na Bi’idha ya Mtume Muhammad (s.a.w.w) njema. Ndugu
zangu Amani ya Mwenyezi Mungu iwe kweny nyote.
Imetolewa na
Maulana Sheikh Hemed Jalala
Kiongozi Mkuu wa Waislamu Shia Ithnasheriya Tanzania
Tare: Jumanne 02.04.2019 sawa na 26 Rajab 1440
Masjid Ghadir, Kigogo Dar es salaam
No comments:
Post a Comment