Waislamu nchini Nigeria wamepongeza uamuzi wa
Mahakama ya Rufaa mjini Lagos kufutulia mbali marufuku ya kuvaa hijabu
katika shule za umma mjini hapo.
Shirika moja la kutetea haki za Waislamu nchini humo linaloitwa
Muslim Rights Concern (MRC) limeipongeza Mahakama ya Rufaa kwa kufuta
marufuku hiyo na kusisitiza kuwa, uamuzi huo ni ushindi kwa jamii ya
Waislamu nchini.
Jaji wa mahakama hiyo alisema kuwazuia mabinti wa
Kiislamu kuvaa vazi hilo la stara kwa mujibu wa mafundisho ya dini yao
eti kwa kigezo kuwa hakuendani na kanuni za shule, ni kukiuka katiba ya
nchi inayosisitiza kuwa, kila mmoja ana haki ya kuabudu na kufuata
maelekezo ya imani yake madhali maelekezo yale hayakiuki haki za
wengine.
Haijabanika iwapo serikali ya nchi hiyo ya magharibi mwa Afrika
itaelekea katika Mahakama ya Juu kupinga uamuzi huo wa Mahakama ya
Rufaa.
Mapema mwaka huu, jumuiya za Kaislamu nchini Nigeria zilitoa taarifa
ya kulaani vikali azma ya Rais Muhammadu Buhari wa nchi hiyo ya kutaka
kupiga marufuku vazi la hijabu na kusema kuwa, sera kama hiyo ni njia ya
kukwepa utatuzi wa matatizo ya kimsingi ya nchi hiyo. Aidha Jumuiya ya
Mawakili Nigeria (NBA) ilisema kupigwa marufuku vazi la kujisitiri
wanawake Waislamu yaani hijabu ni kinyume cha katiba ya nchi hiyo.
Kauli hizo zilitolewa baada ya Buhari kusema kuwa baadhi ya
wanaotekeleza hujuma za kigaidi nchini ni wanawake wanaovaa hijabu na
kwamba iwapo italazimu, serikali yake haitakuawa na njia nyingine ghairi
ya kuchagua moja kati ya mambo mawili ima vazi la hilo la staha au
usalama wa taifa.Chanzo:parstoday