Viongozi wa Waislamu katika eneo la Pwani
nchini Kenya wamekosoa vikali uhusiano wa nchi yao na utawala wa
Kizayuni wa Israel pamoja na ziara ya hivi karibuni ya Benjamin
Netanyahu, Waziri Mkuu wa utawala huo dhalimu.
Viongozi hao wa Waislamu wameonya kuwa, hatua zozote za
kuimarisha uhusiano wa kiusalama, kidiplomasia na kiteknolojia na
utawala wa Kizayuni una maana ya kuhalalisha jinai zinazofanywa na
Wazayuni dhidi ya Wapalestina katika ardhi na maeneo matakatifu ya
Waislamu.
Gavana Hassan Ali Joho, Seneta Hassan Omar na mwanasiasa mwengine
maarufu Suleiman Shahbal wamesema hayo wakati wa Sala ya Idul Fitr
iliyosaliwa kwenye viwanja vya Shule ya Msingi ya Ronald Ngala huko
Mombasa.
Seneta wa Mombasa, Hassan Omar amesema kuwa, mikataba ya teknolojia
na kilimo iliyotiwa saini baina ya Kenya na Israel haina maana yoyote
maana mataifa mengi yanayo teknolojia hiyo.
Amesema, Kenya haina haja ya kuwa na mikataba kama hiyo na utawala wa
Kizayuni wa Israel wakati inao uwezo wa kutia saini mikataba ya namna
hiyo na pande nyingine nyingi zenye rekodi nzuri za haki za binadamu.
Matamshi hayo yameungwa mkono na viongozi wengine wengi wa kidini
waliolaani ziara ya Benjamin Netanyahu, Waziri Mkuu wa utawala wa
Kizayuni wa Israel nchini Kenya.Chanzo.Parstoday
No comments:
Post a Comment