Sala ya Idul Fitri imefutwa katika mji mwa
Southampton Uingereza kufuatia ripoti kuwa makundi ya watu wenye
misimamo mikali wenye chuki dhidi ya Waislamu wanapanga kuvuruga sala
hiyo.
Kwa mujibu wa gazeti la Independent, Jumuiya ya Utamaduni ya
Bangladesh na Uingereza ambayo huandaa Sala na sherehe za Idul Fitr
imelazimika kufuta maandalizi yake baada ya tishio kutoka kundi la South
Coast Resistance ambalo wafuasi wake wana misimamo ya kufurutu ada na
wana chuki dhidi ya Waislamu na watu wenye asili ya mataifa ya kigeni.
Maelfu ya Waislamu walikuwa wamepanga kujumuika katika Bustani ya
Southampton kushiriki katika Sala ya Idul Fitr na sherehe ambazo
hufanyika siku hiyo baada ya kumalizika Mwezi Mtukufu wa Ramadhani.
Waislamu wa mji huo wa Southampton ulio kusini mwa England sasa
watasimamisha sala za Idi ndani ya misikiti mbali mbali mjini humo.
Sara Thornton afisa wa shirika moja la kutetea haki za binadmau
Uingereza liitwalo Tell Mama amebainisha masikitiko yake kuwa Waislamu
wamelazimika kufuta sherehe ambazo ni muhimu katika dini yao kutokana na
kuhofia usalama wao.
Hayo yanajiri wakati ambao, Idara ya Polisi ya Uingereza imesema
kumeshuhudiwa ongezeko kubwa la chuki na jinai dhidi ya watu wenye asili
ya kigeni na wasio wazungu Uingereza baada ya nchi hiyo kupiga kura ya
maoni ya kujiondoa Umoja wa Ulaya.Chanzo:Parstoday