Sunday, June 10, 2018

Serikali imetakiwa kutoa tamko kuhusu Mauaji yanayoendelea Palestina

Kiongozi Mkuu wa Waislamu Shia Ithnasheriya Tanzania Maulana Sheikh Hemed Jalala (Watano Kushoto) akiongoza Matembezi ya Amani ya Siku ya Kimataifa ya Quds Duniani, Kushoto kwake ni Mwenyekiti wa Chama cha CUF Taifa Pro.Ibrahimu Lipumba, Jijini Dar es salaam.

Mwenyekiti Wa Kamati ya Mshikamano  wa Tanzania na Palestina, Abdallah  Othmani,  ameiomba serikali itoa tamko rasmi la kulaani mauaji yaliyotokea hivi karibuni Ghaza na nayoendelea nchini  Palestina.

Ombi hilo alilitoa jana Dar es Salaam, wakati wa matembezi  ya amani ambayo yalianzia Ilala Boma  hadi Kigogo Post, ambayo yalikuwa ni  kupigania uhuru wa Wapalestina ambao walidhulumiwa haki zao.

‘Tuwakumbuke wenzetu wapalestina kwani wamekuwa mstari wa mbele katika kupigania haki nchi za Afrika, hivyo itakuwa sio jambo jema kwa Watanzania kukaa kimywa bila kutoa tamko la kulaani mauaji,’’alisema.

Othmani alisema jambo hili sio la waislamu peke yao bali ni kwa Watanzania wote kupinga dhuluma na unyanyasaji.


Nae Kiongozi Mkuu wa waislamu  Shia Ithnasheria  Tanzania,  Maulana Sheikh Hemed Jalala, alisema matembezi haya yanaunga mkono waislamu wa palestina ambao wanaishi katika mazingira magumu.

Sheikh Jalala alisema  Watanzania wako mstari wa mbele kupigania amani iliyoko, hivyo ni vyema kuwapigania wapalestina nao waweze kupata amani.

“Amani yetu nchini haitakuwa na maana kama hatutaunga mkono wenzetu wa palestina, hivyo hatuna budi kuwapigania wapalestina,’’alisema.

Kwa upande wa Mweneykiti wa Chama cha Wananchi (CUF), Profesa Ibrahim Lipumba, alisema, suala la kuunga mkono wapalestina ni haki katika kuendeleza sera ya hayati Baba wa Taifa Mwalimu Julius Nyerere.

“Mwalimu Nyerere alikuwa akiunga mkono haki ya kupata uhuru, hivyo ni wajibu wetu kuendeleza yale ambayo alikuwa anayafanya Baba wa taifa,’’alisema.