Tarehe kama
ya leo (20, Jamadal Akhirah,1439 sawa na 09-03-2018) leo amezaliwa bint wa
Mtume Muhammad (s.a.w.w) ambae ni Bibi Fatma Zahra (a.s),Mtoto huyu au Bint
huyu au Mama huyu kwasababu ya daraja lake alilokuwanalo ndani ya Uislamu,
Viongozi wa Dini ya Kiislamu, Masheikh wakaitangaza siku ambayo aliozaliwa Mama
huyu ni siku ya Mwanamke wa Kiislamu
Duniani,siku hiyo tumekuwa tukiikumbuka kila mwaka, siku aliyozaliwa mama
huyu ni siku ya Mwanamke wa Kiislamu Duniani kote.
Yanayotufanya
tumkumbuke mama huyu, kwanza ni mwanamke mtakatifu, pili ni mwanamke
aliegubikwa na sifa nyingi nzurinzuri zilizojaa ndani ya kitabu kitakatifu cha
Quran, lakini vilevile mama huyu amegubikwa na sifa nyingi kutoka kwenye kinywa
cha Mtume Muhammad (s.a.w.w), Mama huyu alikuwa kipenzi cha mtume Muhammad
(s.a.w.w).
Tunapozungumza
Wanawake watakatifu kama vile mama Asia, kama vile mama Khadija, kama vile
Mariam aliemzaa Nabii Issa / Yesu (a.s), tunamzungumza vilevile Bi Fatma Zahra
ni katika gurupu la wanawake hao.
Bi Fatma
Zahra alikuwa na Elimu, Maarifa bila shaka tunahitajia Mama zatu na Dada zetu
leo wawe na maarifa na Elimu nzuri,Dunia leo inatafuta maadili mema, dunia leo
inachangamoto kubwa ya kupoteza maadili yao, ambayo Mungu amewaumba nayo, Bi
Fatma Zahra (a.s) alisifika na maadili mema katika Nyanja zote, pia alisifika
na Ukarimu.
Tunaamini
vilevile Nyumba ya watu wenye Imani, Nyumba ya Watu wanaomtambua Mungu, Nyumba
ya watu wenye hofu na Mungu, Nyumba hiyo inakuwa nyumba salama, bila shaka
nyumba inapokuwa salama, jamii inakuwa salama, jamii inapokuwa salama Taifa
nalo linakuwa salama, kwahivyo Nyumba ya Bi Fatma Zahra (a.s) ni Myumba ya
Mwanamke ambae alikuwa akimuabudu Mungu.
Katika siku
hii ya Mwanamke wa Kiislamu Duniani napenda nigusie jambo zima la haki za
Mwanamke ndani ya Uislamu, ziko baadhi ya fikra zinazoona Uislamu haukumpa
Mwanamke haki zake, laa, napenda nisieme katika siku hii ya Mwanamke wa
Kiislamu Duniani kwa kukumbuka kuzaliwa kwa Binti ya Mtume Muhammad (s.a.w.w),
niseme yakwamba Uislamu unamuangalia Mwanamke na Uislamu unampa Mwanamke haki
zake zote.
Mwanamke
anayohaki ya kurithi ndani ya Uislamu, Dini ya Uislamu inampa Mwanamke haki ya
Kumiliki kama vile mwanaume anavyomiliki,Haki ya kufanya Kazi,Haki ya kuendesha
gari,haki ya usawa na haki zingine ambazo ziko kwa mujibu wa dini ya Uislamu.
Katika siku
ya leo siku ya Mwanamke wa Kiislamu Duniani napenda nizungumzie jambo la kuvaa
sitara au hijabu, Hijabu au Sitara katika Uislamu hakiwekwa kama jambo la
kumdhalilisha mwanamke laaa, sitara au hijabu ambayo yakuigwa kutoka kwa Bint
ya Mtume Fatma Zahra (a.s), Sitara au hijabu yake haikumzuia kufanya kazi,
sitara yake haikumzuia kufanya mambo ya Kiislamu,
sitara yake haikumzuia
kuingia darasani kusomesha, sitara yake haikumfanya aache kutoa Hotuba mbele ya
Maswahaba wa Mtume Muhammad (s.a.w.w), kwa hivyo sitara au hijabu ni kitu cha
kumsitiri mwanamke, ni heshima kwa mwanamke,ni adabu kwa mwanamke, bali
mwanamke amekuwa na dhamani kubwa kwa sababu ya sitara yake.
Mwisho
napenda kugusia jambo muhimu sana ambalo ni jambo la kuigwa kutoka kwa binti ya
Mtume Muhammad (s.a.w.w) ambae ni Fatma Zahra (a.s), Jambo la Malezi, Mwanamke
moja ya kazi aliyokuwa nayo ni kulea jamii iliyokuwa njema,Kama tunataka
tutengeneze jamii ya Wachamungu, jamii ya wakweli, jamii ya watu wenye imani,
jamii ya watu wanaopenda kusaidiana, ni lazima hili lianze katika ngazi ya
familia, na hakuna analolitengeneza hilo isipokuwa ni Mama.
Mama ndio
mwenye nafasi ya kutengeneza jamii yenye wakweli, mama ndio mwenye nafasi ya
kutengeneza wabunge ambao kesho watatuwakilisha katika bunge la Jamhuri ya
Muungano wa Tanzania na ahadi zao walizotuahidi na kuzitekeleza, kwasababu
gani, Mwakilishi huyu ameleleka katika nyumba ambayo inapoahidi inatekeleza,
kama tunataka kutengeneza Wachapa kazi ambao hawachoki, kama tunataka kuunda
watu ambao ni hapa kazi hilo linarudi katika ngazi ya familia na unaona Bi
Fatma Zahra (a.s) angalia alivyowalea na
kuwatengeneza Watoto wake kama Imam Hassan (a.s), Imam Hussein (a.s) na Bi
Zainab (a.s).
Bi.Fatma
Zahra ni Mtoto wa Mtume Muhammad (s.a.w.w), Mama yake ni Bi.Khadija, Mume wake
ni Sayyidina Ali (a.s), Watoto wake ni Imam Hassan (a.s), Imam Hussein (a.s) na
Bi.Zainab (a.s), Babu yake ni Abdallah, Bibi yake ni Amina.
Imetolewa na
Kiongozi Mkuu wa
Waislamu Shia Ithnasheriya Tanzania
Maulana Sheikh Hemed
Jalala