Monday, January 30, 2017

Rouhani: Iran sio nchi yenye hofu na chuki kwa wageni

Rais Hassan Rouhani wa Iran amesema Jamhuri ya Kiislamu itatumia muamala na uhusiano wake mzuri na nchi zingine kwa maslahi na manufaa ya taifa hili.

Akizungumza katika kaburi la Imam Khomeini, Muasisi wa Mapinduzi ya Kiislamu kwa mnasaba wa maadhimisho ya miaka 38 ya Mapinduzi ya Kiislamu, Rais Rouhani amesema: "Wananchi wa Iran sio watu wenye chuki na hofu kwa wageni, sisi ni Waislamu na wananchi wa kimapinduzi."

Dakta Rouhani amebainisha kuwa, njia ya Imam Khomeini MA, ni njia ya kuelekea kwenye kilele cha uhuru wa kweli huku akisisitizia umuhimu wa kufuata njia hiyo.
Mosalla mjini Tehran
Kadhalika Rais Rouhani ametoa mkono wa pole kwa familia za mashahidi wa kikosi cha zimamoto waliopoteza maisha  katika tukio la kuungua na kuporomoka jengo la kibiashara la Plasco jijini Tehran hivi karibuni, ambao wanazikwa hii leo.

Shughuli za kuaga miili ya wazima moto hao 16 zinafanyika katika Msikiti wa Mosalla hapa Tehran, kabla ya kwenda kuzikwa katika maziara ya Behesht-e-Zahra.

Imam wa Sala ya Ijumaa mjini Tehran Ayatullah Mohammad Emami Kashani anatazamiwa kuongoza suala ya maiti ya mashahidi hao. Jengo la kibiashara la Plasco mjini Tehran liliungua moto na kisha kuporomoka Januari 19, ambapo makumi ya watu walipoteza maisha.  

No comments: