Monday, January 30, 2017

WATANZANIA WAOMBWA KUMUUNGA MKONO RAIS DK.JOHN MAGUFULI

Mwenyekiti wa Baraza la Vyama vya Siasa nchini, John Shibuda (katikati), akizungumza na waandishi wa habari katika mkutano wa kuuaga mwaka wa 2016 na kuukaribisha mwaka 2017 Dar es Salaam jana. Kulia ni Msajili Msaidizi Ofisi ya Msajili wa Vyama vya Siasa Nchini, Sisty Nyahoza na Makamu Mwenyekiti wa Chama cha ADA na Waziri wa Nchi asiye na Wizara Maalum, Zanzibar.
Na Dotto Mwaibale

WATANZANIA wameombwa kumuunga mkono Rais Dk.John Magufuli kwa jitohada zake anazozifanya za kupongoza nchi.

Mwito huo umetolewa na Mwenyekiti wa Baraza la Vyama vya Siasa nchini John Shibuda wakati akizungumza na waandishi wa habari katika mkutano wa kuuaga mwaka wa 2016 na kuukaribisha mwaka 2017 Dar es Salaam jana.

Alisema Serikali ya awamu ya tano imekuwa ikifanyakazi kubwa ya kudhibiti mirija ya unyonyaji wa pato la Taifa kupitia watumishi hewa, wanafunzi hewa, kaya masikini bandia na kupitia wahujumu uchumi wa matumizi mabaya ya dhamana za Taifa mambo ambayo yalikuwa yakipigiwa kelele na vyama vya upinzani.

"Binafsi nawaomba watanzania bila ya kujali itikadi za vyama vyao kumuunga mkono Rais wetu Dk.John Magufuli na wasaidizi wake Makamu wa Rais, Waziri Mkuu na wengine wote kwa kazi kubwa wanayoifanya ya kuongoza Taifa letu la Tanzania" alisema Shibuda.

Alisema anaupongeza utumishi wa Serikali ya awamu ya tano kwa uzinduzi wa urejeshaji wa uwajibikaji wa watumishi wote kwani hivi sasa watumishi wengi wanatabia za miiko ya utiifu kwa umma.

Akizungumzia Zanzibar alisema uchaguzi umekwisha pita na Rais wa nchi hiyo ni Dk. Ali Mohammed Shein ambaye anatakiwa kuongoza nchi hiyo na wenzake waliochaguliwa ili kuiletea maendeleo Zanzibar hivyo siasa za mihemuko ziachwe.

Shibuda alitumia nafasi hiyo kuwapongeza wazanzibar hasa Chama Cha Mapinduzi (CCM) kwa ushindi walioupata Jimbo la Dimani na kuwaomba walioshindwa wasivunjike moyo kuvunjika jembe siyo mwisho wa uhunzi kwani hata timu kubwa hufungwa na timu ndogo.

Akizungumzia katazo la vyama vya siasa kutofanya mikutano hadi mwaka 2020 alisema majibu ya suala hilo yatatolewa baadae baada ya kulifanyia kazi jambo hilo. 

Katika hatua nyingine Shibuda alisema Baraza la Vyama vya Siasa litakuwa mshirika rafiki wa wadau wote wa siasa na kusimamia maslahi mapana ya jamii na Taifa yanayosimamiwa na Serikali na kuungwa mkono na Bunge mfano Azimio la EPA.

Shibuda alitoa ushauri kwa vyama vyote vya upinzani kuzingatia umakini wa mabadiliko ya Tabia nchi ya mfumo wa uwajibikaji wa Serikali ya awamu ya Tano inayoongozwa na Rais Dk. John Magufuli.

Ufilipino yaitaka Marekani iache kuingiza silaha zake nchini humo

Rais wa Ufilipino Rodrigo Duterte amesema Marekani inahatarisha usalama wa eneo kwa kuendelea kurundika silaha zake katika nchi hiyo.

Rais Duterte ameituhumu Washington kuwa inatengeneza vituo vya kudumu vya kuhifadhi silaha zake katika mikoa mitatu ya nchi hiyo. Rais wa Ufilipino amesema: "Ninatoa ilani kwa vikosi vya jeshi la Marekani, sitoruhusu muendelee kuhifadhi silaha zenu katika ardhi yetu, hata hatufahamu kama makombora ya nyuklia yanaingizwa nchini na US au la."

Amebainisha kuwa, hatua hiyo ya Marekani ya kuingiza mashehena ya silaha nchini humo inakiuka moja kwa moja makubaliano ya ushirikiano wa kiulinzi kati ya nchi mbili hizo.
Wanajeshi wa Marekani nchini Ufilipino
Ufilipino ilisaini makubaliano ya ulinzi na Marekani ambayo yamedumu kwa zaidi ya muongo mmoja sasa mbali na makubaliano mengine mapya yaliyosainiwa baina ya pande mbili mwaka 2014.

Oktoba mwaka jana, Rais Rodrigo Duterte wa Ufilipino alitangaza kuwa anataka ndani ya kipindi cha miaka miwili ijayo vikosi vya jeshi la Marekani viwe vimekwisha ondoka katika ardhi ya nchi yake; na kama italazimu anataka pia kuvunja mkataba wa ulinzi na muitifaki huyo wa muda mrefu wa Manila.

5 wauawa kwa risasi kwenye hujuma dhidi ya msikiti Quebec, Canada

Kwa akali watu watano wameuawa katika hujuma ya kikatili dhidi ya msikiti mmoja katika mji wa Quebec nchini Canada usiku wa kuamkia leo.

Mohamed Yangui, Rais wa Kituo cha Kiutamaduni cha Kiislamu mjini Quebec amesema waumini watano wa Kiislamu waliuawa walipokuwa wakisali Sala ya Ishaa jana usiku, baada ya wavamizi kuvamia msikiti huo na kuwamiminia risasi ovyo. Ameongeza kuwa, watu kadhaa wana majeraha ya risasi kufutia hujuma hiyo ya kinyama.

Polisi katika eneo hilo inadai kuwa imewakamata washukiwa wawili wa hujuma hiyo na kwamba yumkini mmoja amefanikiwa kutoroka.
Nje ya msikiti mjini Quebec, Canada
Waziri Mkuu wa Canada Justin Trudeau amelaani shambulizi hilo dhidi ya msikiti na kulitaja kama hujuma ya kigaidi dhidi ya Waislamu. 

Katika ukurasa wake wa mtandao wa kijamii wa Twitter, Trudeau amesema: "Tunalaani hujuma hiyo dhidi ya pahala pa kutekelezea ibada na kimbilio la waumini, kitendo hiki ni cha kioga na serikali inatoa mkono wa pole kwa wahanga wa hujuma hii, na tuko tayari kutoa msaada wa aina yoyote kwa familia za wahanga hawa."

Kituo cha Kiutamaduni cha Kiislamu mjini Quebec kimekuwa kikilengwa na watu wenye misimamo ya chuki dhidi ya Uislamu mara kwa mara. Mwezi Juni mwaka jana wakati wa Ramadhani, watu wenye chuki dhidi ya Uislamu na Waislamu waliacha kichwa cha nguruwe katika mlango wa msikiti huo.

Aidha mwaka 2015, msikiti mmoja katika jimbo la Ontario nchini Canada uliteketezwa moto na watu wenye misimamo ya kurufutu ada wanaouchukia Uislamu.

Rouhani: Iran sio nchi yenye hofu na chuki kwa wageni

Rais Hassan Rouhani wa Iran amesema Jamhuri ya Kiislamu itatumia muamala na uhusiano wake mzuri na nchi zingine kwa maslahi na manufaa ya taifa hili.

Akizungumza katika kaburi la Imam Khomeini, Muasisi wa Mapinduzi ya Kiislamu kwa mnasaba wa maadhimisho ya miaka 38 ya Mapinduzi ya Kiislamu, Rais Rouhani amesema: "Wananchi wa Iran sio watu wenye chuki na hofu kwa wageni, sisi ni Waislamu na wananchi wa kimapinduzi."

Dakta Rouhani amebainisha kuwa, njia ya Imam Khomeini MA, ni njia ya kuelekea kwenye kilele cha uhuru wa kweli huku akisisitizia umuhimu wa kufuata njia hiyo.
Mosalla mjini Tehran
Kadhalika Rais Rouhani ametoa mkono wa pole kwa familia za mashahidi wa kikosi cha zimamoto waliopoteza maisha  katika tukio la kuungua na kuporomoka jengo la kibiashara la Plasco jijini Tehran hivi karibuni, ambao wanazikwa hii leo.

Shughuli za kuaga miili ya wazima moto hao 16 zinafanyika katika Msikiti wa Mosalla hapa Tehran, kabla ya kwenda kuzikwa katika maziara ya Behesht-e-Zahra.

Imam wa Sala ya Ijumaa mjini Tehran Ayatullah Mohammad Emami Kashani anatazamiwa kuongoza suala ya maiti ya mashahidi hao. Jengo la kibiashara la Plasco mjini Tehran liliungua moto na kisha kuporomoka Januari 19, ambapo makumi ya watu walipoteza maisha.