Monday, January 30, 2017

Ufilipino yaitaka Marekani iache kuingiza silaha zake nchini humo

Rais wa Ufilipino Rodrigo Duterte amesema Marekani inahatarisha usalama wa eneo kwa kuendelea kurundika silaha zake katika nchi hiyo.

Rais Duterte ameituhumu Washington kuwa inatengeneza vituo vya kudumu vya kuhifadhi silaha zake katika mikoa mitatu ya nchi hiyo. Rais wa Ufilipino amesema: "Ninatoa ilani kwa vikosi vya jeshi la Marekani, sitoruhusu muendelee kuhifadhi silaha zenu katika ardhi yetu, hata hatufahamu kama makombora ya nyuklia yanaingizwa nchini na US au la."

Amebainisha kuwa, hatua hiyo ya Marekani ya kuingiza mashehena ya silaha nchini humo inakiuka moja kwa moja makubaliano ya ushirikiano wa kiulinzi kati ya nchi mbili hizo.
Wanajeshi wa Marekani nchini Ufilipino
Ufilipino ilisaini makubaliano ya ulinzi na Marekani ambayo yamedumu kwa zaidi ya muongo mmoja sasa mbali na makubaliano mengine mapya yaliyosainiwa baina ya pande mbili mwaka 2014.

Oktoba mwaka jana, Rais Rodrigo Duterte wa Ufilipino alitangaza kuwa anataka ndani ya kipindi cha miaka miwili ijayo vikosi vya jeshi la Marekani viwe vimekwisha ondoka katika ardhi ya nchi yake; na kama italazimu anataka pia kuvunja mkataba wa ulinzi na muitifaki huyo wa muda mrefu wa Manila.

No comments: