RAIS WA JAMHURI YA MUUNGANO WA TANZANIA
DK JOHN MAGUFULI
OFISI YA RAIS IKULU
1 BARABARA YA BARACK OBAMA
11400 DAR ES SALAAM,TANZANIA
Ndugu Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania,Dk John Pombe Magufuli
Sisi vijana wa Chama cha ACT Wazalendo tunakusalimu katika salam ya Kizalendo.
Tunayo
heshima na taadhima kubwa kukuandikia barua hii, iliyobeba ujumbe
makhsusi wa masikitiko na malalamiko yetu vijana na jamii nzima ya umma
wa Watanzania kwa ujumla.
Masikitiko
na malalamiko yetu yametokana na sintofahamu inayozidi kuibuka katika
maeneo kadha wa kadha ya mawanda ya utawala wako tangu ulipokabidhiwa
rasmi mamlaka ya kuongoza nchi yetu kwa kiapo ulichokula mbele ya
hadhara ya Watanzania, pale Uwanja wa Uhuru mnamo tarehe 05 Novemba,
2015.
Kwa
sehemu yetu ya ngome ya Vijana wa chama cha Wazalendo, ujumbe wetu
tunaokuletea unawakilisha hisia za maelfu ya vijana wa ACT na wasio
wana-ACT nchi nzima.
Hata
hivyo, kila mwanachama wa ACT Wazalendo angali anabaki kuwa huru yeye
binafsi kukuandikia barua kama alivyoelekeza Kiongozi wa Chama chetu
Ndugu Zitto Kabwe katika waraka wake kwa wanachama
UMUHIMU WA KULINDA KIAPO CHAKO CHA KULINDA KATIBA - ISHARA ZA KUDOGOSHA BUNGE NA KUZUIWA WABUNGE WANAOTETEA HAKI ZA WANANCHI
Ndugu
Rais kabla ya kueleza kwa kina dhamira ya ujumbe wetu, Kwa unyenyekevu
mkubwa, tunaomba kukukumbusha kiapo hicho cha utii na uaminifu kwa nchi
yetu na Katiba. Ndugu rais, uliapa hivi;
i).
‘’Mimi, John Pombe Joseph Magufuli NAAPA kwamba nitakuwa mwaminifu kwa
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, na nitalinda na kuitetea KATIBA ya
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Ewe Mwenyezi Mungu, nisaidie.
ii).
Mimi John Pombe Joseph Magufuli NAAPA kwamba nitafanya kazi zangu za
Urais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa Uaminifu, kwa kutimiza
wajibu wa kazi hizo kwa bidii na moyo mkunjufu, na kwamba nitawatendea
HAKI watu wote kwa mujibu wa sheria, mila na desturi za Jamhuri ya
Muungano wa Tanzania bila woga, bila UPENDELEO, dhuluma wala chuki. Ewe
Mwenyezi Mungu nisaidie.
iii).
Mimi John Pombe Joseph Magufuli, NAAPA katika kutekeleza madaraka
niliyopewa kwa mujibu wa KATIBA ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Ewe
Mwenyezi Mungu nisaidie.’’ mwisho wa kunukuu.
Ndg.
Rais, kiapo cha kwanza hapo juu kilikuwa ni kuhusu ‘kuilinda na
kuitetea KATIBA’. Kiapo cha pili kilikutaka kutekeleza majukumu na
madaraka yako kwa uaminifu, kwa bidii, kwa kutenda Haki na kwa kufuata
SHERIA pamoja na kuepuka Upendeleo na chuki kwa yeyote. Nacho kiapo cha
tatu ulichoapa, kilikusisitiza kutekeleza majukumu yako kwa kufuata
KATIBA ya nchi.
Hata
hivyo tunasikitika kwamba, tangu ukamate madaraka ya kuongoza nchi
yetu, umekwishaonyesha Kwa dhahiri Viashiria vya Kukiuka Viapo vyote
Hivyo zaidi ya mara moja, umevunja baadhi ya sheria zetu za nchi mara
kadhaa, umetumia madaraka yako vibaya kwa lengo la kujinufaisha binafsi
kisiasa, wewe na chama chako!- kwa hakika, umekiuka KIAPO ulichokula kwa
Watanzania!
Hatua
ya kwanza iliyoonyesha dalili mbaya za ukiukaji wa Katiba, ilikuwa ni
kitendo cha serikali yako kuamua kuingilia Bunge na kulidhibiti ili
lisiwe wazi na kuwajibika ipasavyo kwa umma.
Serikali
yako kupitia kwa Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, ndugu
Nape Nnauye, ilisema inasitisha urushaji Mubashara (Live) wa matangazo
ya shughuli za vikao vya Bunge kwa hoja mbili dhaifu;
• Kwamba ni kutokana na gharama kubwa Za Kurusha Matangazo hayo ambazo ilidaiwa kuwa TBC (Televisheni ya Taifa) haizimudu tena.
• Kwamba matangazo ya Bunge yamekuwa yakiwafikia wananchi muda wa ‘kazi’.
Mbunge
wa Kigoma Mjini ambaye pia ni Kiongozi wetu wa Chama, ndugu Zitto,
alisimama BUNGENI na kupinga hatua hiyo ya kugeuza Bunge kuwa la giza,
akijenga hoja kuwa ni HAKI ya wananchi kupewa fursa ya kufuatilia moja
kwa moja Baraza lao la Wawakilishi ili wawe na ufahamu wa kutosha juu ya
masuala muhimu yanayowahusu na hivyo kuwa na uwezo wa kuwawajibisha
wabunge na serikali yao.
Ndugu
Zitto alisema kitendo cha serikali na uongozi wa Bunge kuweka vikwazo
kwa matangazo ya Bunge kuwafikia wananchi kwa wakati, kinakwenda kinyume
na Sera ya Kuendesha Serikali Kwa Uwazi (Open Government Policy),
lakini zaidi kinavunja Katiba ya nchi ibara ya 18(d) inayotoa Haki ya
kupewa taarifa wakati wote kuhusu matukio mbalimbali muhimu kwa maisha
na shughuli za wananchi na masuala muhimu kwa jamii.
Ndugu
Zitto aliieleza serikali na uongozi wa Bunge kwamba TBC inaendeshwa kwa
ruzuku ya Serikali ambayo ni kodi za watanzania, hivyo si sahihi wala
si haki kwa watanzania kunyimwa haki ya kujua kinachotokea Bungeni moja
kwa moja kupitia Televisheni yao ya Taifa.
Hata
hivyo, ilikuja kudhihirika baadaye kwamba hatua ya kuzuia matangazo ya
Bunge Mubashara (Live), sababu haikuwa suala la gharama wala matangazo
kwenda hewani muda wa kazi kama ilivyodaiwa na serikali. Televisheni
mbili binafsi za Azam tv na Startv, hazikuhitaji malipo yoyote kutoka
ofisi ya Bunge kwa ajili ya kurusha Mubashara (live) matangazo ya Bunge,
lakini nazo zilinyimwa fursa hiyo!
Wakati
hali ikiwa hivyo, Uongozi wa Bunge ulichukua hatua ya kumwadhibu Mbunge
wa chama chetu kutohudhuria vikao vya Bunge kwa kile kilichoelezwa
kwamba ni kutokana na ‘kufanya fujo’ Bungeni Siku ambayo alisimama ndani
ya Bunge Letu Tukufu la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Kupinga Hatua
hii ya Serikali yako ya Kulidhoofisha Bunge.
Baada
ya Serikali kukosa majibu ya hoja za Ndugu Zitto, hoja zilizokuwa
zimebeba Utetezi wa haki za wanachi kuonyeshwa Bunge lao, uongozi wa
Bunge Pamoja Na Serikali inayoongozwa Nawe, kupitia Kamati ya Haki na
Maadili ya Bunge, uliugeuza jina mchango wa Zitto Kabwe na kuuita ‘fujo’
ili kuhalalisha dhamira hii ovu ya Kulidogosha Bunge, Kinyume Kabisa Na
Katiba ambayo Uliapa kuilinda.
Ndugu
Rais, kwa kitendo hicho, serikali yako ilinuia kukanyaga Katiba ya nchi
kwa kuwanyima wananchi haki ya kufuatilia Mubashara (live) Bunge lao,
huku wabunge waliosimama imara kutetea haki hiyo ya wananchi, serikali
yako ilihakikisha wanadhibitiwa! Kwa Baraka zako mwenyewe, Demokrasia
ndani ya nchi yetu iliwekwa kando nao utawala wa mabavu na ghiliba
ukachukua nafasi. Matukio Haya yalikuwa Ishara thabiti Kuwa serikali
yako imeamua kutawala nje ya Misingi ya Katiba Na Demokrasia ya Nchi
yetu, Na Kuwa Wewe Binafsi umeamua kutokulinda Kiapo chako.
KUZUIA MIKUTANO YA HADHARA YA "OPERESHENI LINDA DEMOKRASIA"
Baada
ya Kiongozi wetu wa Chama kufukuzwa Bungeni, yeye na chama chetu
tuliamua kutumia haki yetu ya Kikatiba, Kufanya Mapokezi ya Kumpongeza
Kwa Kitendo Chake Cha Kizalendo Cha kusimama Imara Kulinda haki za
Wananchi BUNGENI, Pamoja na Kufanya Mikutano ya hadhara ili kuwaeleza
wananchi dhamira chafu iliyojificha kimkakati ndani ya vitendo kandamizi
vya serikali yako dhidi ya haki za wananchi na wawakilishi wa wananchi
katika Baraza lao la Kutunga Sheria na kuisimamia Serikali.
Chama
chetu kilifanya Mkutano mmoja wa Hadhara jijini Dar es Salaam katika
viwanja vya Zakhem, Mbagala mnamo tarehe 05 Juni, 2016, ambapo mikutano
mingine ilikuwa ifuate katika maeneo mengine nchini ikiwa ni utekelezaji
wa “Operesheni Linda Demokrasia”.
Katika
kufanya mkutano wetu, tulizingatia sheria na taratibu zote za nchi,
tulitumia Haki yetu ya Kikatiba Kutoa maoni yetu Na Kwa dhahiri Kupinga
Dalili Na Viashiria hivi vya kuminya demokrasia vilivyoanza kujionyesha
nchini. Ni Katika mkutano huo ambapo pia tulipinga kauli yako ya kuwaita
watoto wa Watanzania masikini kuwa Ni "VILAZA".
Lakini
mara tu baada mkutano huo wa Mbagala, uliviamuru vyombo vya dola kumtia
misukosuko Kiongozi wetu. Kiongozi wetu aliitwa polisi na kuhojiwa juu
ya mambo aliyozungumza kwenye mkutano! Ilikuwa ni baada ya Mkutano huo,
polisi walitoa tamko la kusitisha Mikutano yote ya hadhara ya vyama vya
siasa nchini!
Pamoja
na kutambua kuwa amri hii ya Jeshi la Polisi ilikuwa si amri halali na
ni kinyume na katiba, Bado Viongozi wa Chama chetu waliweza kutumia
busara na kututaka Vijana tusitishe kwa muda husika maandalizi ya
mikutano ya hadhara ya "Operesheni Linda Demokrasia" yaliyokuwa
yanaendelea.
KUZUIWA
KWA HAKI YA MAWAZO MBADALA YA KISERA DHIDI YA SERA ZA SERIKALI -
TAATHIRA ZA KUZUIA KONGAMANO LA UCHAMBUZI WA BAJETI YA SERIKALI YA
2016/17
Ndugu
Rais, Ishara ya pili ya nchi yetu kuendeshwa kinyume na katiba ni hatua
ya Serikali ya Chama chako kuzuia Kongamano la Chama Chetu Kujadili
Bajeti ya Serikali ya mwaka wa fedha wa 2016/17.
Ndugu
Rais, wewe na Chama chako, kikatiba mnayo Dhamana ya Kuongoza Taifa
hili Kwa miaka hii mitano, lakini Chama Chetu, Kikatiba Kinayo haki ya
Kunadi Sera na mawazo mbadala juu ya namna njema ya kuongoza nchi yetu,
ni haki ya Kikatiba na Kidemokrasia. Na si Ugomvi kwa Chama Chetu
kuainisha Sera mbadala dhidi ya sera za Chama Chako. Tukitambua kuwa
vyama vyote nchini vina lengo moja tu, Kujenga Tanzania njema, kwa
vizazi vya leo na Kesho - Tanzania yenye Utu, Uadilifu Na Uzalendo.
Komredi Kwame Nkrumah alipata kusema "Vita Moja, njia tofauti za
Kuikabili Vita".
Kwa
muktadha huo, Chama chetu kiliona kinao WAJIBU - JAMII wa kuchambua
Bajeti KUU ya Serikali yako Kwa mwaka 2016/17. Kwa lengo la Kushauri,
kutilia mkazo, kupendekezo vyanzo mbadala vya mapato na pia kushawishi
kuondoa kodi mbalimbali ambazo ni kikwazo kwa ukuaji wa Uchumi na
zinawakandamiza Watanzania Wanyonge.
Pamoja
na umuhimu wa Kongamano husika kwa Taifa, tuliona, nawe ukiwa Shuhuda,
Serikali yako ilizuia kwa nguvu kongamano husika na hivyo kulinyima
fursa Bunge letu tukufu, watunga Sera wetu, Serikali na Wananchi Kwa
Ujumla kuijua Kwa Undani Bajeti ya Serikali ya Mwaka 2016/17 Kiasi Cha
Bajeti iliyopitishwa na Bunge kutokueleweka na Watendaji wenyewe wa
Serikali pamoja na Wananchi Kwa Ujumla.
Mfano
Mkubwa wa hili ikiwa ni miongozo miwili tofauti ya Gavana wa Benki Kuu
ya Tanzania, Profesa Benno Ndullu na Kamishna Mkuu wa Mamlaka ya Mapato
nchini, ndugu Alfayo Kidata Juu ya Sintofamu ya Ukusanyaji wa Kodi (VAT)
ya tozo za miamala ya simu na Ile ya kibenki. Gavana akiainisha Kuwa
Kisheria VAT husika ni kodi anayotozwa mlaji (Mwananchi Mnyonge) huku
Kamishna "akilazimisha" VAT husika yatozwe Mabenki na Makampuni ya Simu.
Sote
tunajua, nawe Ndugu Rais ukiwa shahidi, Kuwa mpaka sasa suala husika
halijapatiwa ufumbumbuzi, huku gharama za Maisha Kwa wananchi Wanyonge
zikiwa juu kwa makato hayo ya Kodi.
Ni Imani yetu Sisi Vijana wa ACT Wazalendo, Kuwa Kama Kongamano letu la
Kujadili Katiba lisingezuiwa basi sintofahamu hii isingekuwepo. Ni aibu
Sana kwa Serikali, Kwa Gavana wa Benki Kuu na Kamishna Mkuu wa Mamlaka
ya Mapato Nchini kupingana Kwa Suala la Kikodi linalohusu Serikali Moja
ambayo wote wawili ni watumishi.
Jambo
hili linaonyesha kwa dhahiri kuwa Bajeti ya Serikali haikuwa
Shirikishi, hakukuwa na Mjadala Mpana wa Bajeti husika. Chama Chetu
kiliona ombwe hilo, Na ndio maana kiliona Umuhimu wa Kuandaa Kongamano
lile. Hatua ya Serikali yako kulizuia Kongamano husika imekuwa na
taathira kubwa sana kwa Taifa.
Lakini, si tu Serikali yako imesababisha athari Kubwa Kwa nchi Kwa
kuzuia Kongamano lile, Lakini pia haikuwa, na bado haina msingi wowote
wa Kisheria wa kuzuia Kongamano lile. Kwetu Vijana wa ACT Wazalendo
tunaona tukio lile kuwa Ni muendelezo wa Kuminya demokrasia nchini na
kuzuia mawazo mbadala.
ZUIO LAKO SI HALALI, UMELITIA GIZANI TAIFA
Ndugu
Rais, Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Ibara ya 19(1)
inaeleza; ‘’Kila mtu anao uhuru wa kukutana na watu wengine kwa hiari
yake na kwa amani, kuchanganyika, kushirikiana na watu wengine, na kwa
ajili hiyo kutoa mawazo yake hadharani na kuanzisha na kujiunga na vyama
au mashirika yaliyoanzishwa kwa madhumuni ya kuhifadhi au kuendeleza
imani au maslahi yake au maslahi mengineyo.”
Ibara
hii ya Katiba ndio kiini na msingi wa mfumo wa demokrasia ya vyama
vingi tunaoufuata hapa nchini. Itakumbukwa kwamba kurejeshwa kwa Mfumo
wa Vyama vingi nchini mwetu pamoja na shinikizo kubwa la wanaharakati,
kwa kiasi kikubwa ulifanikishwa kutokana na msukumo mahsusi wa hoja
aliyoweka Baba wa Taifa. Utawala wa awamu ya kwanza chini ya Mwalimu
Nyerere ndio uliofuta mfumo wa vyama vingi hapa nchini. Lakini ni
Mwalimu Nyerere yule yule aliyelitambua hitaji la mfumo wa vyama vingi
na akajisahihisha, kwa hekima ya pekee akaushawishi umma na watawala juu
ya haja ya kurejeshwa kwa mfumo wa vyama vingi.
Mwalimu
aliona mbali, akasahihisha makosa yake. Alitambua kwamba, chama
kilichoko madarakani kinahitaji kupewa changamoto kutoka kwa vyama
vingine ili kiwajibike ipasavyo kwa umma.
Mwalimu
aliamini na kuutambua ukweli wa kifalsafa kwamba, tunamnukuu "Sharti
moja la viumbe wote, hasa viumbe wenye nafsi, ni kuhitilafiana’".
Mwalimu
alifahamu ya kwamba watu wote hatuwezi kuwa sawa. Tunatofautiana
kifikra, kimawazo na hata kihisia. Kwa hiyo huwezi kumzuia mwingine
kueleza kwa uhuru hisia, fikra na mawazo yake. ni ukweli huo wa
kifalsafa ndiyo uliomfanya Baba wa Taifa letu kupigania urejeshaji wa
mfumo wa vyama vingi ili mawazo ya watu yatolewe kwa uhuru kupitia vyama
vya siasa na kwa jinsi hiyo yagongane na kuzaa mawazo na fikra bora
zaidi zitakazolifaa taifa letu kupiga hatua za maendeleo.
Ndugu
Rais, hatua zako binafsi na za serikali yako za kuminya haki na uhuru
wa vyama kuwafikia wananchi na kufanya siasa kama KATIBA na Sheria
zinavyoelekeza, inasaliti na kudharau maono ya Mwalimu Nyerere juu ya
mfumo wa vyama vingi. Wewe umekuwa ni kiongozi usiyependa changamoto ya
kifikra kutoka vyama vya upinzani. Unatumia vibaya vyombo vya dola
kuukandamiza upinzani, kinyume kabisa na dhana ya Utawala Bora na
Demokrasia.
Wakati
ukituzuia sisi vyama vya Upinzani kufanya mikutano ya hadhara, wewe na
kwa kofia zako mbili za rais wa Jamhuri na ile ya mwenyekiti wa chama
chako, umekuwa ukifanya mikutano ya hadhara sehemu yoyote ya nchi
utakavyo! Nayo televisheni ya Taifa TBC, ambayo serikali yako ilidai
haina fedha za kurusha Mubashara (live) matangazo ya Bunge, imekuwa
ikirusha matukio yako yote moja kwa moja tena mchana, siku na saa za
kazi! Hii inaleta tafsri ya wazi kwamba kwa kweli umeamua ndani ya nchi
hii usikilizwe wewe peke yako na mihimili mingine ya dola haina nafasi.
Umelitia gizani Taifa.
Huo
ndio Uimla tunaoulalamikia, na ambao tunapenda ukomeshwe, kwa sababu ni
hatari sana kwa mustakabali mwema wa Taifa letu. Huu ndio Uimla ambao
ulitusukuma kuanzisha "Operesheni Linda Demokrasia" ili kuupinga.
Ndugu
rais, tulisikitishwa na kufedheheshwa sana na agizo lako la kupiga
marufuku viongozi wa kisiasa nchini kufanya mikutano popote nchini na
kukutana na wanachama na wananchi kwa ujumla. Tunasema wazi, agizo lako
halifai kwa nchi kama ya kwetu inayofuata mfumo wa siasa ya vyama vingi.
Agizo lako linaifaa nchi kama Korea Kaskazini inayotawaliwa kwa uimla
wa chama kimoja. Ni heri agizo lako hilo ungelipeleka kwingineko
kunakohusika na si hapa nchini mwetu.
Ndugu
Rais, Katiba na sheria zetu za nchi zimepiga marufuku kuwa na vyama vya
kabila au eneo moja pekee ndani ya nchi. Leo hii, Chama chetu kina
mbunge mmoja tu kutoka Kigoma Mjini. Kwa agizo lako, unamaanisha kwamba
pamoja na kwamba mbunge wetu wa Kigoma mjini ndiye pia Kiongozi wetu wa
Chama Kitaifa, ana ruhusa ya kufanya mkutano Kigoma Mjini peke yake.
Haruhusiwi kwenda sehemu nyingine za nchi kuzungumza na watanzania na
kutafuta wanachama wapya.
Vivyo
hivyo na Mwenyekiti wetu wa Chama taifa, ambaye si Mbunge wala si
Diwani, haruhusiwi kwenda kukutana na wanachama wake sehemu yoyote ya
nchi maana yeye hana Jimbo wala Kata. Hii maana yake ni kwamba umeamua
ACT kiwe ni chama cha Kigoma mjini tu, kinyume na matakwa ya Katiba ya
nchi. Agizo lako litazaa vyama vya eneo moja tu na kabila fulani tu
ndani ya nchi hii!
Ndugu
Rais unaligawa Taifa na umeamua uligawe kwa nguvu zako zote
ulizokabidhiwa na watanzania walioamini ungezidisha umoja ndani ya nchi!
Katika dhamira yako hii tunakutaarifu kwamba, sisi vijana wa ACT
Wazalendo, tunalipinga agizo lako maana linalipeleka Taifa Gizani.
KWA NINI TUNAKUKUMBUSHA UMUHIMU WA DEMOKRASIA?
Mbali
na matakwa ya Katiba ya nchi, Misingi na Imani ya Chama chetu imejengwa
katika himaya ya DEMOKRASIA. Sisi ni kundi la vijana ndani ya chama,
ambao tunafunzwa na kulelewa katika maadili ya kuheshimu na kulinda
Demokrasia. Chama chetu kinaamini kwa dhati kwamba, DEMOKRASIA ndiyo
msingi wa Maendeleo, Umoja wa kitaifa na maelewano katika jamii ya watu
waliostaarabika.
ACT
Wazalendo inaamini kwamba msingi mama wa Demokrasia ni kuhakikisha kuwa
wananchi wanakuwa huru na kwamba sauti zao zinasikika na kuzingatiwa
katika mipango ya maendeleo ya nchi. Jamii isiyofuata Demokrasia haina
ustaarabu wala kuheshimiana. Maana watu wake kwa kuzuiwa kusema na
kuzungumza, wanatunza na kulimbikiza hasira na vinyongo vifuani mwao.
Hasira na vinyongo hivyo vinapojaa kupita kiasi hulipuka na kusababisha
zahama kubwa!
Jamii inayokanyaga Demokrasia, tena kwa makusudi kama unavyofanya sasa,
ni jamii inayokaribisha mvurugano na machafuko kwa watu wake.
Sisi
kama vijana tunaojitambua na kuelewa wajibu wetu kwa taifa, hatuko
tayari kuona tukishinikizwa kwa kauli na vitendo vyako kuingiza taifa
letu kwenye machafuko, kwa sababu tu ya jeuri na ubabe wako wa kutojali
Haki na Uhuru wa vyama na makundi mengine ya kijamii ndani ya nchi yetu.
Tunaamini, sote kwa umoja wetu ndani ya nchi hii, tuna dhamana ya amani
na utulivu wa nchi yetu. Ndugu Rais, tunakusihi sana, acha demokrasia
ichukue mkondo wake.
Ndugu
Rais, Miongoni mwa Malengo ya chama chetu, ni pamoja na Kupigania na
kulinda Uongozi bora na Utawala wa Sheria. Uongozi Bora na Utawala wa
Sheria hujikita kwenye Kujenga, Kukuza na Kuendeleza Demokrasia ya vyama
vingi, Kulinda Rasilimali za nchi na kuwa na Serikali inayowajibika kwa
umma wa watanzania.
Vitendo
vyako vya kukandamiza Vyama vya Upinzani, na Sauti Mbadala, vinakwenda
kinyume na Malengo hayo anuai ambayo ni muhimu na ya lazima kwa Ukombozi
wa watu wa Taifa letu Kisiasa, Kiuchumi na Kiutamaduni.
Sisi
tunaamini, hatuwezi kujenga Tanzania iliyo bora kwa kukandamiza maoni
na fikra kinzani. Hatuwezi kujenga Tanzania yenye watu werevu na
wanaoipenda nchi yao, ikiwa wamejawa na hofu mioyoni mwao kutokana na
kuminywa kwa Uhuru wao wa kuzungumza. Ni dhahiri, ukandamizaji huu wa
sauti kinzani ukiendelea tutazalisha taifa la watu wajinga wasio na
uwezo wa kuhoji.
Ndugu
Rais, tunapenda kuhitimisha barua hii kwa kukukumbusha kwamba nchi yetu
ilikwishaamua kuwa na mfumo wa vyama vingi kama njia bora na sahihi ya
kuyafikia maendeleo ya kweli na endelevu. Hatuhitaji ubabe na ghiliba
vichukue nafasi badala ya ‘uwajibikaji’ kwenda sambamba na Demokrasia.
Tutakuunga
mkono katika jitihada zote njema za kuleta mabadiliko chanya katika
nchi yetu kwa kujenga mifumo na taasisi imara za uwajibikaji na utawala
bora unaofuata sheria na katiba, kusimamia uadilifu na nidhamu katika
utumishi wa umma, kupambana na rushwa na ufisadi, kubuni mbinu muafaka
za kukuza uchumi wa nchi yetu na kutengeneza ajira kwetu vijana kwa
kutekeleza sera nzuri ambazo tumekuwa tukipendekeza kwa maeneo
mbalimbali ya uchumi.
Sanjali
na nia njema na ya dhati kabisa tuliyonayo kwako, ndugu Rais hatuko
tayari wala hatutakuwa tayari kuona unaendelea na vitendo, maagizo na
kauli zako zinazovunja Katiba na sheria na zinazolenga kunyonga
Demokrasia ya vyama vingi hapa nchini. Ili kuona kwamba una dhamira
njema ya kujenga upya mifumo na muundo wa uongozi na jamii ndani ya
taifa letu ili kuendana vyema na changamoto za karne ya leo na miaka
mingi ijayo, tunakushauri na kukusihi sana, uongoze taifa kupata KATIBA
mpya kwa kufufua mchakato wa upatikanaji wake kutoka ilipoishia
iliyokuwa Tume ya Mabadiliko ya Katiba ya Jaji Joseph Warioba. Kwa
kufanya hivyo, ni imani yetu utakuwa umelitendea haki taifa lako.
Tunakutakia
kila la heri katika majukumu yako ya utumishi kwa watanzania na ujenzi
wa Taifa. Pamoja, tunaweza kuibadilisha Tanzania kuwa mahali bora na
salama zaidi.
Edna Sunga
Katibu Ngome Ya Vijana Taifa ACT WAZALENDO
12 Agosti,2016.