Maxence Melo akifikishwa mahakamani Ijumaa, Desemba 16, 2016. (Picha kwa hisani ya Michuzi Blog).
Na Daniel Mbega
HATIMAYE leo saa 5:15 asubuhi ya Jumatatu, Desemba 19, 2016 Maxence Melo ametoka kwa dhamana. Mungu ametenda.
Lakini
ni baada ya Mkurugenzi huyo Mtendaji wa kampuni ya Jamii Media Limited
inayomiliki mtandao maarufu wa JamiiForums, kusota mahabusu kwa takriban
saa 144 – yaani saa 72 katika mahabusu ya polisi na saa 72 nyingine
kwenye Gereza la Mahabusu la Keko.
Leo
amefanikiwa kutimiza masharti ya dhamana katika kesi namba 457 ya mwaka
2016 ambayo iko mbele ya Hakimu Mkazi Godfrey Mwambapa katika Mahakama
ya Hakimu Mkazi Kisutu jijini Dar es Salaam, ambayo iliitwa tu kwa ajili
ya kushughulikia dhamana.
Kesi hiyo imepangwa kuitwa Alhamisi, Desemba 29, 2016.
Upande
wa Jamhuri ukiongozwa na Wakili Msomi Mohammed Salum, uliieleza
mahakama kwamba kesi hiyo ilikuwa imeitwa kwa ajili ya dhamana baada ya
upande wa utete kushindwa kutimiza masharti ya dhamana wakati kesi hiyo
iliposomwa kwa mara ya kwanza Ijumaa, Desemba 16, 2016.
Jopo
la mawakili wa utetezi linaongozwa na Peter Kibatala, akiwa pamoja na
Jeremiah Mtobesya, Benedict Ishabakaki, Jebra Kambole, Hassan Kyangiro
na James Malenga, ambapo ilielezwa kwamba wadhamini wamepatikana na
kukidhi vigezo vya dhamana ya maneno ya Shs. 5 milioni kila mmoja.
Hakimu Mwambapa alikubali kutoa dhamana na kumtaka mshtakiwa asitoke nje ya Dar es Salaam bila kibali cha mahakama.
Melo
alikamatwa Jumanne, Desemba 13, 2016 saa 5 asubuhi – tena alikwenda
mwenyewe baada ya kupigiwa simu na Mkuu wa Upelelezi wa Polisi Kanda
Maalum ya Dar es Salaam, Camillius Wambura.
Walichoelezwa
hata waliokuwa wamekwenda naye ni kwamba, waondoke hapo polisi
watakutana mahakamani kesho yake, yaani Desemba 14, 2016. Hakupelekwa
mahakamani wala hakuchukuliwa maelezo.
Kwa
siku mbili mfululizo kati ya Desemba 14 na 15 nilishinda katika Kituo
Kikuu cha Polisi cha Kati, jijini Dar es Salaam, nikiwa na wadau
mbalimbali tukitafuta namna ya kumwekea dhamana. Haikuwezekana.
Hii ndiyo gharama ya kusimamia unachokiamini pamoja na maadili yanayokuongoza.
Na
wakati jitihada za kumpata mdhamini katika kesi mojawapo, upande wa
Jamhuri ukawa umeondoka na wakati huo huo Maxence akapelekwa mahabusu ya
Keko yapata saa 5 asubuhi. Hawakusubiri hadi saa 8 kama ilivyo kawaida
ili kuwapandisha mahabusu wote kwenye karandinga, jambo ambalo likazua
maswali mengi yasiyo na majibu.
Lakini hatimaye Max ameiona nuru, ambayo ameikosa kwa saa 144, japo kwa muda kwa sababu kesi hizi zinaendelea.
Kesi
ya kwanza, ambayo ni namba 456, iko mbele ya Hakimu Mkuu Mkazi wa
mahakama hiyo, Thomas Simba, ambapo upande wa Jamhuri ulieleza kwamba,
katika siku na tarehe tofauti kati ya Aprili 1, 2016 na Desemba 13, 2016
katika eneo la Mikocheni ndani ya Manispaa ya Kinondoni mkoani Dar es
Salaam, Melo akiwa Mkurugenzi wa Jamii Media Co. Ltd ambayo inaendesha
mtandao wa JamiiForums, wakati akijua kwamba Jeshi la Polisi Tanzania
linafanya upelelezi wa jinai kuhusiana na mawasiliano ya kimtandao
yaliyochapishwa kwenye mtandao wake, kwa nia ya kuvuruga uchunguzi,
alikaidi kwa makusudi amri ya kutoa taarifa ambazo alikuwa nazo, kinyume
na kifungu cha 22(2) cha Sheria ya Makosa ya Mtandao (Cyber Crimes Law)
namba 14 ya mwaka 2015.
Katika
namba 457, ambayo alikosa mdhamini, ilielezwa mbele ya Hakimu Mkazi
Mwambapa kwamba, katika siku na tarehe tofauti kati ya Mei 10, 2016 na
Desemba 13, 2016 katika eneo la Mikocheni ndani ya Manispaa ya Kinondoni
mkoani Dar es Salaam, Melo akiwa Mkurugenzi wa Jamii Media Co. Ltd
ambayo inaendesha mtandao wa JamiiForums, wakati akijua kwamba Jeshi la
Polisi Tanzania linafanya upelelezi wa jinai kuhusiana na mawasiliano ya
kimtandao yaliyochapishwa kwenye mtandao wake, kwa nia ya kuvuruga
uchunguzi, alikaidi kwa makusudi amri ya kutoa taarifa ambazo alikuwa
nazo, kinyume na kifungu cha 22(2) cha Sheria ya Makosa ya Mtandao
(Cyber Crimes Law) namba 14 ya mwaka 2015.
Aidha,
katika kesi namba 458, ambayo iko mbele ya Hakimu Nongwa, Melo
anakabiliwa na shtaka la kuendesha mtandao ambao haujasajiliwa nchini
Tanzania (domain) kinyume na kifungu cha 79(c) cha Sheria ya Mawasiliano
ya Kielektroniki na Posta Namba 3 ya mwaka 2010 ikisomwa pamoja na
Kanuni ya 10 na 17 (4) ya Kanuni za Mawasiliano ya Kielektroniki na
Posta Namba 428 za mwaka 2011.
Upande
wa Jamhuri ulieleza katika kesi hiyo kwamba, katika siku na tarehe
tofauti kati ya Desemba 9, 2011 na Desemba 13, 2016 katika eneo la
Mikocheni ndani ya Manispaa ya Kinondoni mkoani Dar es Salaam, Melo
akiwa Mkurugenzi wa Jamii Media Co. Ltd iliyosajiliwa chini ya Sheria ya
Usajili wa Kampuni (Sura ya 212 kama ilivyorejewa mwaka 2002) yenye
hati ya usajili Namba 66333 amekuwa akiendesha na kutumia tovuti
inayojulikana kama jamiiforums.com ambayo haijasajiliwa kwenye code za Tanzania (country code Top Level Domain - ccTLD), inayofahamika kama do-tz.
Yaliyompata
Max ni mwanzo tu wa yale ambayo yanaweza kutupata sote, hususan
waandishi wa habari wa mtandaoni na watumiaji wengine wa mitandao.
Hii
inatokana na kuwepo kwa Sheria ya Makosa ya Kimtandao (Cyber Crimes
Law) ya mwaka 2015, ambayo ilipitishwa Aprili Mosi, 2015.
No comments:
Post a Comment